The chat will start when you send the first message.
1Nitamhimidi BWANA kila wakati,[#1 Sam 21:13-15]
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
2Katika BWANA nafsi yangu itajisifu,[#Yer 9:24; 1 Kor 1:31]
Wanyenyekevu wasikie na kufurahi.
3Mtukuzeni BWANA pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
4Nilimtafuta BWANA, naye akanijibu,[#Zab 18:6; Yon 2:2; Mt 7:7; Lk 11:9]
Akaniokoa kutoka kwa hofu zangu zote.
5Mwelekezeeni macho, mpate kufurahi,
Na nyuso zenu hazitaaibishwa kamwe.
6Maskini huyu aliita, BWANA akasikia,[#Zab 3:4; 2 Sam 22:1]
Akamwokoa na taabu zake zote.
7Malaika wa BWANA huwazungukia,[#Dan 6:22; Mwa 32:1; 2 Fal 6:17; Ebr 1:14]
Wamchao na kuwaokoa.
8Onjeni muone ya kuwa BWANA yu mwema;[#1 Pet 2:3]
Heri mtu yule anayemtumainia.
9Mcheni BWANA, enyi watakatifu wake,[#Flp 4:19]
Maana, wamchao hawapungukiwi kitu.
10Wanasimba hutindikiwa, na kuona njaa;
Bali wamtafutao BWANA hawapungukiwi kitu chochote kilicho chema.
11Njoni, enyi wana, mnisikilize,
Nami nitawafundisha kumcha BWANA.
12Ni nani atamaniye uzima na atakaye kuishi,[#1 Pet 3:10-12]
Siku nyingi afurahie mema?
13Uuzuie ulimi wako na mabaya,[#1 Pet 2:22]
Na midomo yako na kusema hila.
14Uache mabaya ukatende mema,
Utafute amani ukaifuatie.
15Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki,[#Ayu 36:7]
Na masikio yake hukielekea kilio chao.
16Uso wa BWANA ni juu ya watenda mabaya,[#Law 17:10; Yer 44:11; Mit 10:7]
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
17Walilia, naye BWANA akasikia,
Akawaponya kutoka kwa taabu zao zote.
18BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na huwaokoa waliopondeka roho.
19Mateso ya mwenye haki ni mengi,
Lakini BWANA kutoka kwayo yote.
20Huihifadhi mifupa yake yote,[#Yn 19:36]
Usivunjike hata mmoja.
21Uovu utamwua asiye haki,[#Zab 94:23]
Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa.
22BWANA huzikomboa nafsi za watumishi wake,[#2 Sam 4:9; Zab 103:4]
Wote wamkimbiliao hawatahukumiwa.