Zaburi 42

Zaburi 42

Hamu ya kusaidiwa na Mungu katika dhiki

1Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji.

Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu.

2Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai,[#Yn 7:37; 1 The 1:9]

Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu?

3Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku,

Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako?

4Nayakumbuka mambo haya kwa uchungu moyoni mwangu,[#Isa 30:29]

Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano,

Na kuwaongoza hadi katika nyumba ya Mungu,

Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu.

5Nafsi yangu, kwa nini kuinama,[#Zab 56:3,11; Isa 50:10; Omb 3:24]

Na kufadhaika ndani yangu?

Umtumainie Mungu;

Kwa maana nitakuja kumsifu,

Aliye afya ya uso wangu,

Na Mungu wangu.

6Nafsi yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo nitakukumbuka,

Toka nchi ya Yordani, na Mahermoni, na toka kilima cha Mizari.

7Kilindi chapigia kelele kilindi kwa sauti ya maporomoko ya maji yako,[#Eze 7:26]

Gharika zako zote na mawimbi yako yote yamepita juu yangu.

8Mchana BWANA ataagiza fadhili zake, na usiku wimbo wake utakuwa nami,[#Kum 28:8]

Naam, maombi kwa Mungu aliye uhai wangu.

9Nitamwambia Mungu, mwamba wangu, Kwa nini umenisahau?

Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea?

10Watesi wangu hunitukana mithili ya kuniponda mifupa yangu,

Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako?

11Nafsi yangu, kwa nini kuinama,

Na kufadhaika ndani yangu?

Umtumaini Mungu;

Kwa maana nitakuja kumsifu,

Aliye afya ya uso wangu,

Na Mungu wangu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya