Zaburi 44

Zaburi 44

Kilio cha kitaifa na sala kwa ajili ya msaada

1Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu

Baba zetu wametuambia,

Matendo uliyoyatenda siku zao, siku za kale.

2Wewe kwa mkono wako uliwafukuza mataifa,[#Kut 15:17; Kum 7:1; Yos 10:42]

Ukawakalisha wao.

Wewe uliwatesa watu wa nchi,

Ukawafanikisha wao.

3Maana hawakuitwaa nchi kwa upanga wao,[#Yos 24:12; Kum 4:37]

Wala hawakupata ushindi kwa mkono wao;

Bali mkono wako wa kulia, naam, mkono wako,

Na nuru ya uso wako, kwa kuwa ulipendezwa nao.

4Ee Mungu, Wewe ndiwe mfalme wangu,[#Zab 74:12]

Uagize mambo ya wokovu kwa Yakobo.

5Kwa nguvu zako tutawaangusha watesi wetu;[#Dan 8:4]

Kwa jina lako tutawakanyaga watupingao.

6Maana sitautumainia upinde wangu,[#Zab 33:16]

Wala upanga wangu hauwezi kuniokoa.

7Bali Wewe ndiwe uliyetuokoa kutoka kwa watesi wetu;

Na watuchukiao umewaaibisha.

8Tumejisifia Mungu mchana kutwa,[#Zab 34:2; Rum 2:17; 1 Kor 1:31]

Na jina lako tutalishukuru milele.

9Lakini umetutupa, umetufedhehesha,

Wala huendi na majeshi yetu.

10Waturudisha nyuma tukampa mtesi kisogo,[#Law 26:17; Kum 28:25]

Na watuchukiao wanajipatia mateka.

11Umetutoa kama kondoo tuwe chakula,[#Kum 4:27; 2 Fal 17:6; Zab 60:1; Yer 32:37; Lk 21:24]

Na kututawanya kati ya mataifa.

12Wawauza watu wako bila kupata mali,[#Isa 52:3,4]

Wala hukupata faida kwa thamani yao.

13Umetufanya kuwa lawama kwa jirani zetu,

Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.

14Umetufanya kuwa mithali kwa mataifa,

Sababu ya kutikisa kichwa kwa watu wa nchi.

15Mchana kutwa fedheha yangu i mbele yangu,

Na aibu imeufunika uso wangu,

16Kwa sauti ya mwenye kulaumu na kukufuru,[#Zab 8:2]

Kwa sababu ya adui na mjilipiza kisasi.

17Haya yote yametupata, bali hatukukusahau,[#Dan 9:13]

Wala hatukulivunja agano lako.

18Hatukuiacha mioyo yetu irudi nyuma,

Wala hatua zetu hazikuiacha njia yako,

19Japo ulituponda katika pango la mbwamwitu,[#Isa 34:13]

Na kutufunika kwa uvuli wa mauti.

20Ikiwa tumelisahau jina la Mungu wetu,

Au kumnyoshea mungu mgeni mikono yetu;

21Je! Mungu hangegundua jambo hilo?[#Ayu 31:14; Zab 139:1; 1 Sam 16:7; Mhu 12:14; Yn 2:25; Mdo 1:24; Rum 2:16; Ebr 4:12; Ufu 2:23]

Maana ndiye azijuaye siri za moyo.

22Hasha! Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;[#Rum 8:36]

Tunafanywa kama kondoo waendao kuchinjwa.

23Amka, Bwana, mbona umelala?

Ondoka, usitutupe milele.

24Mbona unatuficha uso wako,

Na kusahau kuonewa na kudhulumiwa kwetu?

25Maana nafsi yetu imeinama mavumbini,

Tumbo letu limegandamana na nchi.

26Uinuke, uwe msaada wetu,

Utukomboe kwa ajili ya fadhili zako.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya