Zaburi 55

Zaburi 55

Kusalitiwa na rafiki

1Ee Mungu, uisikilize sala yangu,

Wala usijifiche nikuombapo rehema.

2Unisikilize na kunijibu,

Nimetangatanga nikilalama na kuugua.

3Kwa sababu ya sauti ya adui,

Kwa sababu ya dhuluma yake yule mwovu.

Kwa maana wananitupia uovu,

Na kwa ghadhabu wananiudhi.

4Moyo wangu unaumia ndani yangu,[#Zab 102:3-5; Mt 26:37,38; Yn 12:27; 2 Kor 1:8-10]

Na hofu za mauti zimeniangukia.

5Hofu na tetemeko limenijia,

Na hofu kubwa imeniingia.

6Nikasema, Ningekuwa na mbawa kama njiwa,

Ningeruka mbali na kustarehe.

7Ningekwenda zangu mbali,

Ningetua jangwani.

8Ningefanya haraka kuzikimbia

Dhoruba na tufani.

9Ee Bwana, uwaangamize, uzivuruge ndimi zao,

Maana nimeona dhuluma na fitina katika mji.

10Mchana na usiku huzunguka kutani mwake;

Uovu na taabu zimo ndani yake;

11Tamaa mbaya zimo ndani yake;

Dhuluma na hila haziondoki mitaani mwake.

12Kwa maana si adui aliyenitukana;

Kama ndivyo, ningevumilia.

Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye;

Kama ndivyo, ningejificha asinione.

13Bali ni wewe, mtu mwenzangu,[#2 Sam 15:12]

Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana.

14Tumehusiana vizuri; na kutembea

Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano.

15Mauti na iwapate kwa ghafla,[#Hes 16:30]

Na washuke kuzimu wangali hai,

Maana uovu uko nyumbani mwao moyoni mwao.

16Nami nitamwita Mungu,

Na BWANA ataniokoa;

17Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua,[#Dan 6:10; Lk 18:1; Mdo 3:1]

Naye ataisikia sauti yangu.

18Ameiokoa nafsi yangu iwe salama, asinikaribie mtu,[#2 Nya 32:7]

Maana walioshindana nami walikuwa wengi.

19Mungu atawalaye tangu milele atanisikia;[#Kum 33:27]

Na kuwaadhibu,

maana hawajirekebishi,

Wala kumcha Mungu.

20Mwenzangu amenyosha mkono awadhuru waliopatana naye,

Amelivunja agano lake.

21Kinywa chake ni laini kuliko siagi,

Bali moyo wake ni vita.

Maneno yake ni mororo kuliko mafuta,

Lakini yanakata kama upanga mkali.

22Umtwike BWANA mzigo wako naye atakutegemeza,[#Zab 37:24]

Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.

23Nawe, Ee Mungu, utawateremsha,

Wafikie shimo la uharibifu;

Watu wa damu na hila hawataishi nusu ya siku zao,

Bali mimi nitakutumaini Wewe.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya