Zaburi 7

Zaburi 7

Ombi la msaada juu ya watesaji

1BWANA, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe,

Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.

2Asije akaipapura nafsi yangu kama simba,[#1 Pet 5:8]

Akaniburura hadi pasipokuwa na wa kuniponya.

3BWANA, Mungu wangu, ikiwa nimetenda haya,[#2 Sam 16:7]

Ikiwa mna uovu mikononi mwangu,

4Ikiwa nimemlipa mabaya[#1 Sam 24:7]

Yeye aliyekaa kwangu salama;

(Hasha! Nimemponya yeye

Aliyekuwa mtesi wangu bila sababu;)

5Basi adui na anifuatie,

Na kuikamata nafsi yangu;

Naam, aukanyage uzima wangu,

Na kuulaza utukufu wangu mavumbini.

6BWANA uondoke kwa hasira yako;[#Zab 94:2]

Ujiinue Juu ya ujeuri wa watesi wangu;

Uamke kwa ajili yangu;

Umeamuru hukumu.

7Kusanyiko la mataifa na likuzunguke,

Na juu yake uketi utawale.

8BWANA atawaamua mataifa,

BWANA, unihukumu mimi,

Kwa kadiri ya haki yangu,

Kulingana na unyofu nilio nao.

9Ubaya wao wasio haki na ukome,[#Ufu 2:23; 1 Sam 16:7]

Lakini umthibitishe mwenye haki.

Kwa maana mjaribu mioyo na fikira

Ndiye Mungu aliye mwenye haki.

10Ngao yangu ina Mungu,

Awaokoaye wanyofu wa moyo.

11Mungu ni mwamuzi mwenye haki,

Naam, Mungu akasirikiaye waovu kila siku.

12Mtu asipoongoka ataunoa upanga wake;

Ameupinda uta wake na kuuweka tayari;

13Naye amemtengenezea silaha za kuua,

Akifanya mishale yake kuwa mipini ya moto.

14Tazama, huyu ametunga uovu,

Amechukua mimba ya madhara, amezaa uongo.

15Amechimba shimo, amelichimba chini sana,[#Est 7:10; Mit 5:22]

Akatumbukia katika handaki aliyoichimba!

16Madhara yake yatamrejea kichwani pake,[#1 Fal 2:32]

Na dhuluma yake itamshukia utosini.

17Nitamshukuru BWANA kwa kadiri ya haki yake;

Nitaliimbia jina la BWANA aliye juu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya