The chat will start when you send the first message.
1Katika mwezi wa nane, mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema,[#Hag 1:1; Ezr 4:24—5:1; 6:14]
2BWANA amewakasirikia sana baba zenu.
3Basi, uwaambie, BWANA wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema BWANA wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi.[#Yer 25:5; Mik 7:19; Mal 3:7; Lk 15:20]
4Msiwe ninyi kama baba zenu, ambao manabii wa zamani waliwalilia, wakisema, BWANA wa majeshi asema hivi, Rudini sasa, na kuziacha njia zenu mbovu, na matendo yenu maovu; lakini hawakusikia, wala kunitii, asema BWANA.[#Isa 1:16,17; Yer 3:12; Eze 33:11; Hos 14:1; Mt 3:8,9; Mdo 3:19]
5Je, Baba zenu wako wapi? Je, manabii nao wanaishi milele?
6Lakini maneno yangu, na amri zangu nilizowaagiza hao manabii, watumishi wangu, je, Hazikuwapata baba zenu? Nao wakatubu na kusema, BWANA wa majeshi ametutenda kulingana na njia zetu, na matendo yetu, kama alivyokusudia kutenda.[#Isa 55:1; Omb 1:18]
7Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani, mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema,
8Niliona wakati wa usiku, na tazama, mtu amepanda farasi mwekundu, akasimama kati ya miti ya mihadasi iliyokuwa mahali penye uvuli; na nyuma yake walikuwapo farasi wengine wekundu, na wa rangi ya kijivujivu, na weupe.[#Yos 5:13; Zek 6:2; Ufu 6:2-4]
9Ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, ni nini hawa? Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Nitakuonesha ni nini hawa.
10Na yule mtu aliyesimama kati ya mihadasi akajibu, akasema, Hawa ndio BWANA aliowatuma, waende huku na huko duniani.[#Zab 91:11; Ebr 1:14]
11Nao wakamjibu yule malaika wa BWANA aliyesimama kati ya mihadasi, wakasema, Tumekwenda huku na huko duniani, na tazama, dunia yote inatulia, nayo imestarehe.[#Zab 102:20]
12Ndipo yule malaika wa BWANA akajibu, akasema, Ee BWANA wa majeshi, hadi lini utakataa kuurehemu Yerusalemu, na miji ya Yuda uliyoikasirikia miaka hii sabini?[#Zab 103:13; Ufu 6:10; Dan 9:2; Zek 7:5]
13Naye BWANA akamjibu yule malaika aliyesema nami kwa maneno mazuri, maneno yenye faraja.[#Isa 40:1,2; Yer 29:10]
14Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Haya, piga kelele na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Naona wivu kwa ajili ya Yerusalemu, na kwa ajili ya Sayuni; naona wivu mkuu sana.[#Yoe 2:18; Zek 8:2]
15Nami ninayakasirikia sana mataifa yanayostarehe; kwa maana mimi nilikuwa nimekasirika kidogo tu, nao wakayazidisha maafa.[#Isa 47:6]
16Kwa sababu hiyo BWANA asema hivi, Ninaurudia Yerusalemu kwa rehema nyingi; nyumba yangu itajengwa ndani yake, asema BWANA wa majeshi, na kamba itanyoshwa juu ya Yerusalemu.[#Isa 12:1; Zek 2:1,2]
17Piga kelele tena, na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Miji yangu itajawa na ufanisi tena; naye BWANA ataufariji Sayuni tena, atauchagua Yerusalemu tena.[#Isa 51:3; Zek 3:2]
18Nami nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, pembe nne.
19Nami nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Nini hizi? Naye akanijibu, Hizi ndizo pembe zilizowatawanya watu wa Yuda, na Israeli, na Yerusalemu.[#Ezr 4:1; Hab 3:14]
20Kisha BWANA akanionesha wafua chuma wanne.
21Ndipo nikauliza, Hawa wanakuja kufanya nini? Akasema, Hizi ndizo pembe zilizowatawanya watu wa Yuda, hata ikawa hakuna mtu aliyeinua kichwa chake; lakini hawa wamekuja kuzifukuza, kuziangusha pembe za mataifa, walioinua pembe yao juu ya nchi ya Yuda, ili kuwatawanya watu wake.[#Zab 75:4,5]