Zekaria 9

Zekaria 9

Hukumu kwa adui za Israeli

1Ufunuo wa neno la BWANA, lililosemwa juu ya nchi ya Hadraki, na Dameski itakuwa mahali pake pa kustarehe; kwa maana jicho la mwanadamu na la kabila zote za Israeli linamwelekea BWANA;[#Zab 145:15; Isa 17:1-3; Yer 49:23-27; Amo 1:3-5; #Isa 23:1-18; Eze 26:1—28:26; Yoe 3:4-8; Amo 1:9-10; Mt 11:21-22; Lk 10:13-14]

2na Hamathi pia iliyo mpakani mwake; na Tiro, na Sidoni, kwa maana ana akili nyingi.[#Yer 49:23; Amo 1:9; Oba 1:20; Eze 28:3]

3Na Tiro alijijengea ngome, akakusanya fedha kama mchanga, dhahabu safi kama matope ya njia kuu.

4Tazama, Bwana atamwondolea mali zake, naye ataupiga uwezo wake alio nao baharini, naye mwenyewe atateketezwa kwa moto.[#Eze 26:17]

5Ashkeloni ataona haya na kuogopa; Gaza pia, naye atafadhaika sana; na Ekroni, kwa maana matarajio yake yatatahayarika; na mfalme ataangamia toka Gaza, na Ashkeloni atakuwa hana watu.[#Isa 14:29-31; Yer 47:1-7; Eze 25:15-17; Yoe 3:4-8; Amo 1:6-8; Sef 2:4-7; Mdo 8:26]

6Na mwana wa haramu atatawala huko Ashdodi, nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti.

7Nami nitaondoa damu yake kinywani mwake, na machukizo yake nitayatoa katika meno yake; yeye naye atakuwa ni mabaki kwa Mungu wetu; naye atakuwa kama mtu mkuu katika Yuda, na Ekroni kama Myebusi.

8Nami nitapiga kambi yangu pande zote za nyumba yangu ili kuwapinga adui, mtu awaye yote asipite ndani yake wala kurudi; wala mtu aoneaye hatapita tena kati yao; kwa maana sasa nimeona kwa macho yangu.[#Kum 33:27; Zab 34:7; Kut 3:7]

Mtawala ajaye wa watu wa Mungu

9Furahi sana, Ee binti Sayuni;[#Mt 21:5; Yn 12:15; Zab 2:6; Yn 1:49; Lk 19:38; Isa 45:21; Mdo 22:14; 1 Pet 3:18]

Piga kelele, Ee binti Yerusalemu;

Tazama, mfalme wako anakuja kwako;

Ni mwenye haki, naye ana wokovu;

Ni mnyenyekevu, amepanda punda,

Naam, mwanapunda, mtoto wa punda.

10Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiria mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia.[#Zab 72:3,8; Isa 11:10; Efe 2:14; Kol 1:20,21; Zab 72:8; Isa 9:6,7; Mik 5:4; Ufu 11:15]

11Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji.[#Isa 61:1; Kut 24:8]

12Rudini katika ngome yenu, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu.

13Maana nimejipindia Yuda, nimeujaza upinde wangu Efraimu; nami nitawachochea wana wako, Ee Sayuni, wapigane na wana wako, Ee Ugiriki, nami nitakufanya wewe kuwa kama upanga wa shujaa.

14Naye BWANA ataonekana juu yao,

Na mshale wake utatoka kama umeme;

Na Bwana MUNGU ataipiga tarumbeta,

Naye atakwenda kwa pepo za kisulisuli za kusini.

15BWANA wa majeshi atawalinda;[#Law 4:25]

Nao watakula na kuyakanyaga mawe ya teo;

Nao watakunywa na kufanya kelele kama kwa divai;

Nao watajazwa kama mabakuli, kama pembe za madhabahu.

16Na BWANA, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo,[#Eze 37:23; Mal 3:17; Isa 11:12]

Kama kundi la watu wake;

Kwa maana watakuwa kama vito vya taji,

Vikimetameta juu ya nchi yake.

17Maana wema wake, jinsi ulivyo mwingi!

Na uzuri wake, jinsi ulivyo mwingi!

Nafaka itawasitawisha vijana wanaume,

Na divai mpya vijana wanawake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya