2 Nya 22

Utawala wa Ahazia

1Nao wenyeji wa Yerusalemu walimfanya Ahazia mwanawe mdogo awe mfalme mahali pake; maana wakubwa wote wamekwisha kuuawa na kikosi cha watu waliokuja matuoni pamoja na Waarabu. Hivyo akatawala Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda.[#2 Fal 8:24; 2 Nya 21:17]

2Ahazia alikuwa na umri wa miaka arobaini na miwili alipoanza kutawala; akatawala mwaka mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Athalia binti Omri.[#2 Fal 8:26; 1 Fal 16:28; 2 Nya 21:6]

3Yeye naye akaziendea njia za nyumba ya Ahabu; kwa kuwa mamaye alikuwa mshauri wake katika kufanya maovu.

4Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kama nyumba ya Ahabu; kwa kuwa hao walikuwa washauri wake, alipokwisha kufa babaye, hata aangamie.[#2 Nya 24:17,18; Mit 1:10; 19:27]

5Naye akaenda kwa mashauri yao, akafuatana na Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli ili kupigana na Hazaeli mfalme wa Shamu huko Ramoth-gileadi; nao Washami wakamjeruhi Yoramu.[#2 Fal 8:28; #22:5 Au, Yehoramu.]

6Akarudi Yezreeli ili aponye jeraha walizomjeruhi huko Rama, alipopigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda, akashuka amtazame Yoramu mwana wa Ahabu, katika Yezreeli, kwa sababu alikuwa hawezi.[#2 Fal 9:15; #22:6 Au, Azaria.]

7Basi kuangamia kwake Ahazia kulitokana na Mungu, kwa vile alivyomwendea Yoramu; kwa kuwa alipofika, akatoka pamoja na Yoramu juu ya Yehu mwana wa Nimshi, ambaye BWANA alimtia mafuta ili awakatilie mbali nyumba ya Ahabu.[#Amu 14:4; 1 Fal 12:15; 2 Nya 10:15; Zab 5:10; 9:16; Amo 3:6; Mdo 2:23; 1 Fal 19:16; 2 Fal 9:6,7,21]

8Ikawa, Yehu alipokuwa akiwafanyia hukumu nyumba ya Ahabu, aliwakuta wakuu wa Yuda, na wana wa nduguze Ahazia, wakimtumikia Ahazia, akawaua.[#2 Fal 10:10,11]

9Akamtafuta Ahazia, wakamkamata, (naye alikuwa amejificha Samaria,) wakamleta kwa Yehu, wakamwua; wakamzika, kwa maana wakasema, Huyu ni mwana wa Yehoshafati, huyo aliyemtafuta BWANA kwa moyo wake wote. Wala nyumba ya Ahazia hawakuwa na uwezo wa kuushika ufalme.[#2 Fal 9:27]

Athalia Akivamia Kiti cha Ufalme

10Basi Athalia, mama wa Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaangamiza wazao wote wa kifalme wa nyumba ya Yuda.

11Ila Yehosheba, binti mfalme, akamtwaa Yoashi, mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa wana wa mfalme waliouawa, akamweka yeye na yaya wake katika chumba cha kulala. Basi Yehosheba, binti mfalme Yehoramu, mkewe Yehoyada kuhani, (naye alikuwa umbu lake Ahazia,) akaficha usoni pa Athalia, asimwue.[#2 Fal 11:2]

12Akawako pamoja nao, amefichwa nyumbani mwa Mungu, miaka sita. Na Athalia akaitawala nchi.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania