2 Nya 3

Sulemani Ajenga Hekalu

1Ndipo Sulemani akaanza kuijenga nyumba ya BWANA huko Yerusalemu, juu ya mlima Moria, pale BWANA alipomtokea Daudi babaye alipotengeza mahali pale alipoagiza Daudi, katika kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi.[#1 Fal 6:1; 1 Nya 29:19; Yn 2:19-21; 1 Kor 6:19; Mwa 22:2; 1 Nya 22:1; #3:1 Au, Ornani.]

2Akaanza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili katika mwaka wa nne wa kutawala kwake.

3Basi hii ndiyo misingi ya majengo ya nyumba ya Mungu aliyoiweka Sulemani. Urefu wake kwa mikono ya cheo cha kwanza ulikuwa mikono sitini, na upana wake mikono ishirini.[#1 Fal 6:2]

4Na ukumbi uliokuwa mbele yake, urefu wake kadiri ya upana wa nyumba ulikuwa mikono ishirini, na kwenda juu kwake mia na ishirini; akaufunikiza ndani kwa dhahabu safi.[#1 Fal 6:3]

5Nayo nyumba kubwa akaifunika miti ya miberoshi, aliyoifunikiza kwa dhahabu safi, akaifanyizia mitende na minyororo.[#1 Fal 6:17]

6Akaipamba nyumba kwa vito iwe na uzuri; nayo dhahabu ilikuwa dhahabu ya Parvaimu.

7Tena, akaifunikiza kwa dhahabu nyumba, na boriti, na vizingiti, na kuta zake, na milango yake; akachora makerubi kutani.

8Akaifanya nyumba ya patakatifu pa patakatifu; urefu wake kadiri ya upana wa nyumba, ulikuwa mikono ishirini, na upana wake mikono ishirini; akaifunikiza kwa dhahabu safi, ya talanta mia sita.

9Na uzani wa misumari ulikuwa shekeli hamsini za dhahabu. Akazifunikiza orofa zake za juu kwa dhahabu.

10Na ndani ya nyumba ya patakatifu pa patakatifu akafanyiza makerubi mawili ya kuchonga; wakayafunikiza kwa dhahabu.[#1 Fal 6:23]

11Na mabawa ya makerubi hayo urefu wake ulikuwa mikono ishirini; bawa moja mikono mitano, likiufikilia ukuta wa nyumba; na bawa la pili mikono mitano, likishikana na bawa la kerubi la pili.

12Na bawa la kerubi la pili lilikuwa mikono mitano, likiufikilia ukuta wa nyumba; na bawa la pili mikono mitano, likishikana na bawa la kerubi la kwanza.

13Yakaenea mabawa ya makerubi hayo mikono ishirini; yakasimama juu ya miguu yao, na nyuso zao ziliielekea nyumba.

14Akalifanya pazia la samawi na urujuani na nyekundu, na kitani safi, akaifanyizia makerubi.[#Kut 26:31; Mt 27:51; Ebr 9:3]

15Tena akafanya mbele ya nyumba nguzo mbili za mikono thelathini na tano kwenda juu kwake, na taji iliyokuwa juu yake moja moja ilikuwa mikono mitano.[#1 Fal 7:15; Yer 52:21]

16Akafanya minyororo ndani ya chumba cha ndani, akaiweka juu ya vichwa vya nguzo; akafanya makomamanga mia, akayaweka juu ya hiyo minyororo.

17Akazisimamisha nguzo hizo mbele ya hekalu, moja upande wa kuume, na ya pili upande wa kushoto; akaliita jina la ile ya kuume Yakini, na jina la ile ya kushoto Boazi.[#3:17 maana yake imedhaniwa kuwa Atathibitisha.; #3:17 maana yake imedhaniwa kuwa Imo nguvu.]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania