2 Wathesalonike 3

2 Wathesalonike 3

Tuombee nasi

1Na sasa, ndugu zangu, mtuombee. Ombeni kwamba mafundisho ya Bwana yaendelee kuenea haraka na kwamba watu watayaheshimu, kama ilivyotokea kwenu.

2Mtuombee tupate ulinzi kutokana na watu wabaya na waovu. Mnafahamu, siyo wote wanamwamini Bwana.

3Lakini Bwana ni mwaminifu. Atawapa nguvu na ulinzi dhidi ya Mwovu.

4Tuna uhakika kwa sababu ya Bwana mnayemtumikia na mtaendelea kuyafanya yale tunayowaamuru.

5Tunaomba kwamba Bwana atasababisha mjisikie upendo wa Mungu na kukumbuka subira ya ustahimilivu wa Kristo.

Wajibu wa Kufanya kazi

6Kwa mamlaka ya Bwana wetu Yesu Kristo tunawaambia kukaa mbali na mwamini yeyote anayekataa kufanya kazi. Watu kama hao wanaokataa kufanya kazi hawafuati mafundisho tuliyowapa.

7Ninyi wenyewe mnafahamu kwamba mnatakiwa kuishi kwa kuiga mfano wetu. Hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi wala hatukuishi pasipo utaratibu unaofaa.

8Hatukupokea chakula kutoka kwa yeyote bila ya kukilipia. Tulifanya kazi ili tusiwe mzigo kwa yeyote. Tulifanya kazi usiku na mchana.

9Tulikuwa na haki ya kuomba mtusaidie. Lakini tulifanya kazi ili tuwe mfano wa kuigwa nanyi.

10Tulipokuwa nanyi, tuliwapa kanuni hii: “Yeyote asiyefanya kazi asile.”

11Tunasikia kwamba watu wengine katika kundi lenu wanakataa kufanya kazi. Hawashughuliki kufanya kazi badala yake wanashughulika kwa kuyafuatilia maisha ya wengine.

12Maagizo yetu kwao ni kuwakataza kuwasumbua wengine, waanze kufanya kazi na kupata chakula chao wenyewe. Ni kwa mamlaka ya Bwana Yesu Kristo tuwaagize kufanya hivi.

13Msichoke kabisa kutenda wema.

14Wakiwapo wengine huko wanaokataa kufanya tunayowaambia katika barua hii, basi mkumbuke wao ni kina nani. Msichangamane nao. Ndipo pengine wanaweza kujisikia aibu.

15Lakini msiwafanye kama adui. Washaurini waachane na tabia hiyo kama watu wa nyumbani mwake Mungu.

Maneno ya Mwisho

16Tunaomba kwamba Bwana wa amani awape amani wakati wote na kwa njia yoyote. Bwana atakuwa pamoja nanyi nyote.

17Hizi ni salamu zangu kwa mwandiko wangu: Paulo . Ninafanya hivi katika barua zangu zote kuonesha zinatoka kwangu. Hivi ndivyo ninavyoandika.

18Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International