2 Timotheo 1

2 Timotheo 1

1Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu. Ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alivyotaka. Yeye alinituma kwa sababu Mungu alipenda niwaeleze watu juu ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu.[#1:1 Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32; Lk 23:2. Tazama pia na katika Orodha ya Maneno.]

2Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa:

Neema, rehema na amani iwe kwako kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.

Shukrani na Kutia Moyo

3Daima namshukuru Mungu katika maombi yangu ninapokukumbuka usiku na mchana kwa ajili yako. Ni Mungu wa mababu zangu na daima nimemtumikia kwa dhamiri safi.

4Nikiyakumbuka machozi yako kwa ajili yangu, ninatamani kukuona, ili niweze kujazwa na furaha.

5Nimekumbuka imani yako ya kweli ambayo mwanzoni ilikuwa kwa bibi yako Loisi na kwa mama yako Eunike. Nami nashawishika hiyo iko kwako.

6Kwa sababu hii ninakukumbusha karama ya Mungu ambayo uliipokea wakati nilipokuwekea mikono. Sasa nataka uitumie karama hiyo na ikue zaidi na zaidi kama mwali wa moto mdogo uwakavyo ndani ya moto.

7Kwani Roho ambaye Mungu alitupa sisi ni chanzo cha ujasiri wetu, ni nguvu, upendo na fikra safi.

8Hivyo usione aibu kushuhudia juu ya Bwana wetu Yesu au kunionea aibu mimi, niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali aliteseka pamoja nami kwa ajili ya Habari Njema na Mungu hutupa nguvu.

9Alituokoa na kutuita katika maisha ya utakatifu, sio kwa sababu ya kitu cho chote tulichokifanya wenyewe, bali kwa kusudi lake mwenyewe na neema, ambayo ametupa sisi kwa Kristo Yesu kabla ya mwanzo wa wakati,

10na ambayo sasa imeonyeshwa kwetu kwa kuja kwake Kristo Yesu, Mwokozi wetu. Yeye Kristo aliiharibu mauti na kuleta uzima na kutokufa kwenye nuru kwa njia ya Habari Njema.

11Niliteuliwa na Mungu kutangaza Habari Njema kama mtume na mwalimu.

12Na ni kwa kazi hii ninateseka lakini sioni haya kwa sababu namjua yeye niliyemwekea imani yangu, na nina uhakika kuwa anaweza kukilinda kile nilichokikabidhi kwake hadi Siku ile.

13Yale uliyoyasikia nikiyafundisha yawe mfano kwako wa mafundisho utakayofundisha wewe. Uyafuate na yawe kielelezo cha mafundisho ya kweli na uzima kwa uaminifu na upendo ule ule ambao Kristo Yesu ametuonesha.

14Kwa msaada wa Roho Mtakatifu anayeishi ndani yako, uyalinde mafundisho haya ya mazuri na yenye thamani mliyopewa dhamana kwayo.

15Unajua kwamba kila mtu aliyeko Asia ameniacha. Hata Figelo na Hermogene nao wameniacha.

16Ninaomba kwamba Bwana ataonesha rehema wa familia ya Onesiforo, amekuwa faraja yangu mara nyingi, na hakuona haya kwa ajili yangu kuwa gerezani.

17Kinyume chake, alipofika Rumi, alinitafuta kwa bidii hadi aliponiona.

18Bwana Yesu na amjalie kupata rehema kutoka kwa Bwana Mungu katika siku ile ya hukumu ya mwisho! Unafahamu vema ni kwa njia ngapi alinihudumia wakati nilipokuwa Efeso.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International