Mathayo 3

Mathayo 3

Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu

(Mk 1:1-8; Lk 3:1-9,15-17; Yh 1:19-28)

1Baadaye, kabla ya miaka mingi kupita, Yohana Mbatizaji alianza kuwahubiri watu ujumbe uliotoka kwa Mungu. Naye alihubiri kutokea maeneo ya nyikani huko Uyahudi.

2Yohana alisema, “Tubuni na kuibadili mioyo yenu, kwa sababu ufalme wa Mungu umekaribia.”

3Nabii Isaya alisema kuhusu habari za Yohana Mbatizaji pale aliposema,

“Kuna mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani:

‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;

nyoosheni njia kwa ajili yake.’”

4Huyo Yohana alivaa mavazi yaliyofumwa kutokana na manyoya ya ngamia. Naye alijifunga mkanda wa ngozi kuzunguka kiuno chake, na alikula nzige na asali mbichi.

5Watu kutoka Yerusalemu na maeneo yote ya Uyahudi na wale kutoka maeneo yote yaliyo kando ya Mto Yordani walikwenda kwa Yohana Mbatizaji;

6huko waliungama matendo yao mabaya kwake naye akawabatiza katika Mto Yordani.

7Mafarisayo na Masadukayo wengi walikwenda kwa Yohana ili wabatizwe. Yohana alipowaona, akasema, “Enyi ninyi nyoka! Ni nani amewaonya kuikimbia hukumu ya Mungu inayokuja?

8Muibadili mioyo yenu! Na muoneshe kwa vitendo kuwa mmebadilika.

9Ninajua mnachofikiri. Mnataka akasema kuwa, ‘lakini Abrahamu ni baba yetu!’ Hiyo haijalishi. Ninawaambia Mungu anaweza kumzalia Abrahamu watoto kutoka katika mawe haya.

10Shoka limewekwa tayari kukata shina la mti katika mizizi yake. Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa vivyo hivyo na kutupwa motoni.[#3:10 Watu wasiomtii Mungu ni kama “miti” itakayokatwa.]

11Mimi ninawabatiza kwa maji kuonesha kuwa mmebadilika mioyoni mwenu na pia maishani mwenu. Lakini yupo mwingine anayekuja baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, huyo atafanya mengi zaidi yangu. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Yeye huyo atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

12Naye atakuja akiwa tayari kwa ajili ya kuisafisha nafaka. Atatenganisha nafaka nzuri kutoka kwenye makapi, na kisha ataiweka nafaka nzuri kwenye ghala yake. Kisha atayachoma makapi kwa moto usiozimika.”[#3:12 Inamaanisha kuwa Yesu atawatenganisha watu wema na waovu.]

Yohana Ambatiza Yesu

(Mk 1:9-11; Lk 3:21-22)

13Ndipo Yesu alitoka Galilaya na kwenda Mto Yordani. Alikwenda kwa Yohana, akitaka kubatizwa.

14Lakini Yohana alijaribu kumzuia. Yohana akamwambia Yesu, “Kwa nini unakuja kwangu ili nikubatize? Mimi ndiye ninayepaswa kubatizwa na wewe!”

15Yesu akajibu, “Acha iwe hivyo kwa sasa. Tunapaswa kuyatimiza mapenzi ya Mungu.” Ndipo Yohana akakubali.

16Hivyo Yesu akabatizwa. Mara tu aliposimama kutoka ndani ya maji, mbingu zilifunguka na akamwona Roho Mtakatifu akishuka kutoka mbinguni kama hua na kutua juu yake.[#3:16 Ndege mfano wa njiwa, aendaye kwa kasi au “njiwa pori”, “tetere”.]

17Sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu, nimpendaye. Ninapendezwa naye.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International