Warumi 16

Warumi 16

Paulo Anayo Mambo ya Mwisho ya Kusema

1Napenda mjue kuwa mnaweza kumwamini dada yetu Foebe. Ni mtumishi maalum wa kanisa la kule Kenkrea.

2Nawaomba mmkaribishe kama yule aliye wa Bwana. Mkaribisheni kwa jinsi ambayo watu wa Mungu wanapaswa. Msaidieni kwa chochote atakachohitaji kutoka kwenu. Yeye amekuwa kiongozi anayeheshimika ambaye amewasaidia watu wengine wengi, pamoja na mimi.

3Mpeni salamu Priska na Akila, ambao wametumika pamoja nami kwa ajili ya Kristo Yesu.

4Waliyahatarisha maisha yao wenyewe ili wayaokoe maisha yangu. Nawashukuru hao, na makanisa yote ya wasio Wayahudi yanawashukuru wao.

5Vilevile, fikisheni salamu katika kanisa linalokusanyikia nyumbani mwao.

Msalimuni rafiki yangu mpendwa Epaineto. Alikuwa mtu wa kwanza kumfuata Kristo kule Asia.

6Pia msalimieni Mariamu ambaye alifanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili yenu.

7Pia msalimieni Androniko na Yunia. Hao ni jamaa zangu, na walikuwa gerezani pamoja nami. Walikuwa wafuasi wa Kristo kabla yangu. Nao ni miongoni mwa wale walio muhimu sana waliotumwa na Kristo kuifanya kazi yake.[#16:7 Kwa maana ya kawaida, “muhimu miongoni (au kwa) mitume”.]

8Msalimuni Ampliato, rafiki yangu mpendwa miongoni mwa watu wa Bwana,

9na kwa Urbano. Aliyefanya kazi pamoja nasi kwa ajili ya Kristo. Pia fikisheni salamu kwa rafiki yangu mpendwa Stakisi

10na Apele, aliyejithibitisha kuwa yeye ni mfuasi wa kweli wa Kristo.

Nisalimieni watu wote katika nyumba ya Aristobulo

11na Herodioni, jamaa yangu.

Wasalimieni nyumba nzima ya Narkiso aliye wake Bwana

12na Trifaina na Trifosa, wanawake wanaofanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili ya Bwana. Nisalimieni rafiki yangu mpendwa Persisi. Dada huyu amefanya kazi kwa juhudi kubwa kwa ajili ya Bwana.

13Pia msalimieni Rufo, mmoja wa wateule wa Bwana, na mama yake, ambaye amefanyika mama yangu pia.

14Fikisheni salamu kwa Asinkrito, Flegoni, Hermesi, Patroba, Herma na waamini wote walio pamoja nao.

15Msalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, Olimpa na watu wote wa Mungu walio pamoja nao.

16Mpeni kila mmoja ile salamu maalum ya watu wa Mungu.[#16:16 Kwa maana ya kawaida, “busu takatifu”.]

Makanisa yote yaliyo ya Kristo yanatuma salamu zao kwenu.

17Kaka na dada zangu, ninataka muwe macho na wale wanaosababisha mabishano na kuumiza imani za watu kwa kufundisha mambo ambayo ni kinyume cha yale mliyojifunza. Mjitenge nao.

18Watu wa namna hiyo hawamtumikii Kristo Bwana wetu. Wanajifurahisha wenyewe tu. Wanatumia mazungumzo matamu na kusema mambo yanayopendeza ili kuwadanganya wale wasiojua kuhusu uovu.

19Kila mtu amesikia juu ya utii wenu kwa Bwana, nami nafurahi sana juu ya hilo. Lakini ninataka muwe werevu kuhusu yaliyo mema na kutokujua lolote kuhusu yaliyo maovu.

20Mungu mwenye kuleta amani atamwangamiza Shetani mapema na kuwapa nguvu juu yake.

Neema ya Bwana wetu Yesu iwe pamoja nanyi.

21Timotheo, mtumishi pamoja nami, anawatumieni salamu. Pia Lukio, Yasoni na Sosipatro (hawa ni jamaa zangu) wanawatumieni salamu.

22Mimi Tertio, ninayeandika barua hii kwa ajili ya Paulo. Ninawasalimu kama mmoja aliye wa Bwana.

23Gayo ameniruhusu na kanisa lote hapa kuitumia nyumba yake. Anawatumia salamu zake. Erasto na kaka yetu Kwarto pia wanatuma salamu. Erasto ndiye mtunza hazina wa mji hapa.

25Atukuzwe Mungu! Yeye ndiye anayeweza kuzitumia Habari Njema ninazozifundisha kuwaimarisha katika imani. Ni ujumbe ninaowaambia watu kuhusu Yesu Kristo. Ujumbe huo ni siri ya ukweli iliyofichwa kwa karne nyingi sana lakini sasa imefunuliwa.

26Na kweli hiyo sasa imeonyeshwa kwetu. Ilijulishwa kwa yale ambayo manabii waliandika katika Maandiko, kama Mungu wa milele alivyoagiza. Na sasa imejulikana kwa mataifa yote ili waweze kuamini na kumtii yeye.

27Utukufu wa milele ni kwa Mungu mwenye hekima pekee kwa njia ya Yesu Kristo. Amina.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International