The chat will start when you send the first message.
1Kutatokea chipukizi katika kisiki cha Yese,[#11:1 Taz Ufu 5:5; 22:16]
tawi litachipua mizizini mwake.
2Roho ya Mwenyezi-Mungu itakaa kwake,
roho ya hekima na maarifa,
roho ya shauri jema na nguvu,
roho ya ujuzi na ya kumcha Mwenyezi-Mungu.
3Atafurahia kumcha Mwenyezi-Mungu.
Hatahukumu kadiri ya mambo ya njenje,
wala kuamua kufuatana na yale anayosikia.
4Atawapatia haki watu maskini,[#11:4 Taz 2Thes 2:8]
atawaamulia sawasawa wanyonge nchini.
Kwa neno lake ataiadhibu dunia,
kwa tamko lake atawaua waovu.
5Haki itakuwa kama mkanda wa kujifunga,[#11:5 Taz Efe 6:14]
uaminifu utakaa naye kama mkanda kiunoni.
6Mbwamwitu ataishi pamoja na mwanakondoo,[#11:6-9 Taz Isa 65:25]
chui watapumzika pamoja na mwanambuzi.
Ndama na wanasimba watakula pamoja,
na mtoto mdogo atawaongoza.
7Ngombe na dubu watakula pamoja,
ndama wao watapumzika pamoja;
na simba atakula majani kama ng'ombe.
8Mtoto mchanga atacheza kwenye shimo la nyoka
mtoto ataweza kutia mkono shimoni mwa nyoka wa sumu.
9Katika mlima mtakatifu wa Mungu[#11:9 Taz Hab 2:14]
hakutakuwa na madhara wala uharibifu.
Maana kumjua Mwenyezi-Mungu kutaenea pote nchini,
kama vile maji yajaavyo baharini.
10Siku ile chipukizi wa Yese atakuwa ishara kwa mataifa; mataifa yatamtafuta na makazi yake yatatukuka.[#11:10 Taz Roma 15:12]
11Siku hiyo, Bwana ataunyosha mkono wake tena kuwarejesha watu wake waliosalia huko Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Shinari, Hamathi na sehemu za pwani.
12Naye atatweka bendera kuwaashiria mataifa,
kuwakusanya Waisraeli waliodharauliwa,
kuwaleta pamoja watu wa Yuda waliotawanywa,
na kuwarudisha toka pembe nne za dunia.
13Wivu wa Efraimu juu ya Yuda utakoma,
hakutakuwa tena na uadui kati ya Yuda na Efraimu.
14Wote pamoja watawavamia Wafilisti walio magharibi,
pamoja watawapora watu wakaao mashariki.
Watawashinda Waedomu na Wamoabu,
nao Waamoni watawatii.
15Mwenyezi-Mungu atakausha ghuba ya bahari ya Shamu,[#11:15 Kiebrania: Bahari ya Misri.]
kwa pumzi yake ichomayo atakausha mto Eufrate,
nao utagawanyika katika vijito saba,
watu wavuke humo miguu mikavu.
16Tena, kutakuwa na barabara kuu toka Ashuru
kwa ajili ya watu wake waliobaki humo
kama ilivyokuwa kwa Waisraeli
wakati walipotoka nchini Misri.