The chat will start when you send the first message.
1Kauli ya Mungu dhidi ya nchi ya Moabu.[#15:1--16:14 Taz Isa 25:10-12; Yer 48:1-47; Eze 25:8-11; Amosi 2;1-3; Sef 2:8-11]
Mji wa Ari nchini Moabu umeangamizwa usiku;
mji wa Kiri nchini Moabu umeteketezwa usiku.
2Watu wa Diboni wamepanda hekaluni, hadi mahali pa juu kuomboleza,
watu wa Moabu wanalia kwa ajili ya Nebo na Medeba;
vichwa vyote vimenyolewa upara,
ndevu zao zote zimekatwa kabisa.
3Wanapita njiani wamevaa mavazi ya gunia.
Kwenye paa za nyumba na viwanja vya mji
watu wanalia na kukauka kwa machozi.
4Watu wa Heshboni na Eleale wanalia,
sauti zao zinasikika hadi Yahazi.
Hata askari wa Moabu wanalia kwa sauti;
mioyo yao inatetemeka.
5Moyo wangu unasononeka juu ya nchi ya Moabu;
wakimbizi wake wanakimbilia Soari,
wanakimbia mpaka Eglath-shelishiya.
Wanapanda njia ya kwenda Luhithi wakilia,
njiani kwenda Horonaimu wanatoa kilio cha maangamizi.
6Kijito cha Nimrimu kimekauka;
nyasi zimekauka, majani mabichi yamenyauka,
hakuna chochote kinachoota hapo.
7Watu wanavuka kijito cha Mierebi
wamebeba mali yao yote waliyochuma,
na kila walichojiwekea kama akiba.
8Kilio kimezuka pote nchini Moabu,
maombolezo yao yamefika Eglaimu,
naam, yamefika mpaka Beer-elimu.
9Maji ya Diboni yamejaa damu,
lakini Mungu ataongeza msiba wa Diboni.
Hao wachache watakaobaki hai
na kukimbia kutoka nchini Moabu,
watapelekewa simba wa kuwaua.