Isaya 23

Isaya 23

Angamizo la Tiro na Sidoni

1Kauli ya Mungu dhidi ya Tiro.

Ombolezeni, enyi mabaharia wa mbali baharini,

maana Tiro mji wenu umeharibiwa,

humo hamna tena makao wala bandari.

Mtazipokea habari hizo mtakaporejea kutoka Kupro.

2Nyamazeni kwa mshangao enyi wakazi wa pwani,

naam, tulieni enyi wafanyabiashara wa Sidoni,

ambao wajumbe wenu wanapita baharini,

3wakasafiri katika bahari nyingi.

Mapato yenu yalikuwa nafaka ya Misri,

mkaweza kufanya biashara na mataifa.

4Aibu kwako ewe Sidoni,

mji wa ngome kando ya bahari!

Bahari yenyewe yatangaza:

“Sijapata kuwa na uchungu wa kuzaa,

wala sijawahi kuzaa;

sijawahi kulea wavulana,

wala kutunza wasichana!”

5Habari zitakapoifikia Misri

kwamba Tiro imeangamizwa,

Wamisri watafadhaika sana.

6Ombolezeni enyi wenyeji wa Foinike!

Jaribuni kukimbilia Tarshishi.

7Je, huu ndio mji wa furaha wa Tiro,

mji ambao ulijengwa zamani za kale,

ambao wakazi wake walikwenda kumiliki nchi za mbali?

8Ni nani aliyepanga mambo haya dhidi ya Tiro,

mji uliowatawaza wafalme,

wafanyabiashara wake walikuwa wakuu,

wakaheshimiwa duniani kote?

9Ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi!

Yeye ndiye aliyeyapanga haya yote.

Alifanya hivyo akiharibu kiburi chao

na kuwaaibisha waheshimiwa wake.

10Limeni sasa ardhi yenu enyi wakazi wa Tarshishi;

maana hamna tena bandari kwa ajili ya meli kubwa.

11Mwenyezi-Mungu ameunyosha mkono wake juu ya bahari,

amezitetemesha falme;

ametoa amri kuziharibu ngome za Kanaani.

12Alisema: “Ewe binti Sidoni

hutaweza kufanya sherehe tena;

hata ukikimbilia Kupro,

huko nako hutapata pumziko!”

13(Ni Wakaldayo, wala si Waashuru, waliowaacha wanyama wa porini wauvamie mji wa Tiro. Wao ndio waliouzungushia mji huo minara ya kuushambulia, wakayabomoa majumba yake na kuufanya magofu.)[#23:13 aya 13 makala ya Kiebrania si dhahiri.]

14Pigeni yowe enyi meli za Tarshishi,

maana kimbilio lenu limeharibiwa.

15Hapo mji wa Tiro utasahaulika kwa muda wa miaka sabini, muda wa maisha ya mfalme. Baada ya miaka hiyo sabini, mji wa Tiro utakumbwa na kile watu wanachoimba juu ya malaya:

16“Twaa kinubi chako

uzungukezunguke mjini,

ewe malaya uliyesahaulika!

Imba nyimbo tamutamu.

Imba nyimbo nyinginyingi

ili upate kukumbukwa tena.”

17Baada ya miaka hiyo sabini, Mwenyezi-Mungu atauadhibu mji wa Tiro, nao utarudia kufanya uzinzi kwa kujiuza kwa mataifa yote ya dunia.

18Fedha utakayopata itawekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Mji wenyewe hautafaidika kwa fedha hiyo ila wale wanaomwabudu Mwenyezi-Mungu wataitumia kununulia chakula kingi na mavazi mazuri.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania