Maombolezo 2

Maombolezo 2

Adhabu ya Yerusalemu

1Mwenyezi-Mungu, kwa hasira yake,

amewaweka watu wa Siyoni gizani.

Fahari ya Israeli ameibwaga chini.

Siku ya hasira yake

alilitupilia mbali hata hekalu lake.

2Mwenyezi-Mungu ameharibu bila huruma

makazi yote ya wazawa wa Yakobo.

Kwa ghadhabu yake amezibomoa ngome za watu wa Yuda.

Ufalme wao na watawala wake

ameuporomosha chini kwa aibu.

3Nguvu yote ya Israeli ameivunja kwa hasira.

Hakunyosha mkono kuwasaidia

walipokutana na adui;

amewawakia watu wa Yakobo kama moto,

akateketeza kila kitu.

4Amevuta upinde wake kama adui,

na kuuweka mkono wake wa kulia tayari,

amewaua wote tuliowaonea fahari

katika maskani yetu watu wa Siyoni.

Ametumiminia hasira yake kama moto.

5Mwenyezi-Mungu amekuwa kama adui,

ameangamiza watu wa Israeli;

majumba yake yote ameyaharibu,

ngome zake amezibomoa.

Amewazidishia watu wa Yuda

matanga na maombolezo.

6Hekalu lake amelibomoa kama kitalu bustanini,

maskani yake ameiharibu.

Amefutilia mbali sikukuu na Sabato huko Siyoni,

kwa hasira yake kuu amewakataa mfalme na makuhani.

7Mwenyezi-Mungu ameipuuza madhabahu yake

na hekalu lake amelikataa.

Kuta za majumba mjini amewaachia maadui wazibomoe,

wakapiga kelele humo nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu

kama kelele za wakati wa sikukuu.

8Mwenyezi-Mungu alipania kuubomoa ukuta wa mji wa Siyoni;

aliupima na kuhakikisha kila kitu kimeharibiwa;

minara na kuta za nje ya mji akazifanya ukiwa,

zote kwa pamoja zikaangamia.

9Malango yake yameanguka chini,

makomeo yake ameyaharibu na kuyavunjavunja.

Mfalme na wakuu wake wako uhamishoni kati ya mataifa.

Mwongozo wa sheria umetoweka kabisa,

manabii wake hawapati tena maono

kutoka kwake Mwenyezi-Mungu.

10Wazee wa Siyoni wameketi chini kimya,

wamejitia mavumbi vichwani

na kuvaa mavazi ya gunia.

Wasichana wa Yerusalemu wameinamisha vichwa.

11Macho yangu yamevimba kwa kulia,

roho yangu imechafuka.

Moyo wangu una huzuni nyingi

kwa sababu ya kuangamizwa kwa watu wangu

kwa sababu watoto wachanga wanazirai katika barabara za mji.

12Wanawalilia mama zao:

“Wapi chakula, wapi kinywaji?”

Huku wanazirai kama majeruhi

katika barabara za mjini,

na kukata roho mikononi mwa mama zao.

13Nikuambie nini ee Yerusalemu?

Nikulinganishe na nini?

Nikufananishe na kitu gani

ili niweze kukufariji,

ee Siyoni uliye mzuri?

Maafa yako ni mengi kama bahari.

Ni nani awezaye kukuponya?

14Manabii wako wamekuonea maono madanganyifu,

hawakufichua wazi uovu wako

ili wapate kukurekebisha,

bali walikuonea kauli ya uongo na ya kupotosha.

15Wapita njia wote wanakudhihaki;

wanakuzomea, ee Yerusalemu,

wakitikisa vichwa vyao kwa dharau na kusema:

“Je, huu ndio ule mji uliofikia upeo wa uzuri,

mji uliokuwa furaha ya dunia nzima?”

16Maadui zako wote wanakuzomea,

wanakufyonya na kukusagia meno,

huku wakisema, “Tumemwangamiza!

Kweli, siku ile tuliyoingojea kwa hamu

sasa imefika na tumeiona!”

17Mwenyezi-Mungu amefanya yale aliyokusudia,

ametekeleza yale aliyotishia;

kama alivyopanga tangu kale

ameangamiza bila huruma yoyote;

amewafanya maadui wafurahie adhabu yako,

amewakuza mashujaa wa maadui zako.

18Kuta zako, ee mji wa Siyoni, zimlilie Mwenyezi-Mungu!

Machozi na yatiririke kama mto mchana na usiku!

Lia na kuomboleza bila kupumzika!

19Usiku kucha uamkeamke ukalie.

Mfungulie Mwenyezi-Mungu yaliyo moyoni mwako.

Mwinulie mikono yako kuwaombea watoto wako,

watoto wanaozirai kwa njaa popote barabarani.

20Tazama ee Mwenyezi-Mungu uone!

Je, kuna yeyote uliyemtendea ulivyotutendea sisi?

Je, hata kina mama wawale watoto wao?

Je, nao makuhani wauawe hekaluni mwako?

21Maiti za vijana na wazee zimelala vumbini barabarani,

wasichana na wavulana wangu wameuawa kwa upanga;

umewaua bila huruma siku ya hasira yako.

22Umewaalika kama kwenye sikukuu

maadui zangu walionitisha kila upande.

Katika siku ya hasira yako ee Mwenyezi-Mungu,

hakuna aliyetoroka au kunusurika.

Wale niliowazaa na kuwalea

adui zangu wamewaangamiza.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania