Zaburi 41

Zaburi 41

Sala ya mgonjwa

1Heri mtu anayewajali maskini;

Mwenyezi-Mungu atamwokoa wakati wa shida.

2Mwenyezi-Mungu atamlinda na kumweka hai,

naye atafanikiwa katika nchi;

Mungu hatamwacha makuchani mwa maadui zake.

3Mwenyezi-Mungu atamsaidia awapo mgonjwa,

atamponya maradhi yake yote.

4Nami nilisema: “Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu,

unihurumie maana nimekukosea wewe.”

5Madui zangu husema vibaya juu yangu:

“Atakufa lini na jina lake litoweke!”

6Wanitembeleapo husema maneno matupu;

wanakusanya mabaya juu yangu,

na wafikapo nje huwatangazia wengine.

7Wote wanichukiao hunongonezana juu yangu;

wananiwazia mabaya ya kunidhuru.

8Husema: “Maradhi haya yatamuua;

hatatoka tena kitandani mwake!”

9Hata rafiki yangu wa moyoni niliyemwamini,[#Taz Mat 26:23; Marko 14:18; Luka 22:21; Yoh 13:18]

rafiki ambaye alishiriki chakula changu,

amegeuka kunishambulia!

10Ee Mwenyezi-Mungu, unionee huruma!

Unipe nafuu, nami nitawalipiza.

11Hivyo nitajua kwamba unapendezwa nami,

maadui zangu wasipopata fahari juu yangu.

12Wewe umenitegemeza kwani natenda mema;

waniweka mbele yako milele.

13Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli,[#Taz Zab 106:48]

tangu milele na hata milele!

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania