Zaburi 99

Zaburi 99

Mungu mtawala mkuu

1Mwenyezi-Mungu anatawala,

mataifa yanatetemeka!

Ameketi juu ya viumbe vyenye mabawa,

nayo dunia inatikisika!

2Mwenyezi-Mungu ni mkuu katika Siyoni;

ametukuka juu ya mataifa yote.

3Wote na walisifu jina lake kuu la kutisha.

Mtakatifu ndiye yeye!

4Ee mfalme mkuu, mpenda uadilifu!

Umethibitisha haki katika Israeli;

umeleta uadilifu na haki.

5Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu;

angukeni kifudifudi mbele zake.

Mtakatifu ndiye yeye!

6Mose na Aroni walikuwa makuhani wake;

Samueli alikuwa miongoni mwa waliomlilia.

Walimlilia Mwenyezi-Mungu naye akawasikiliza.

7Alisema nao katika mnara wa wingu;

waliyazingatia matakwa yake na amri alizowapa.

8Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wewe uliwasikiliza;

kwao ulikuwa Mungu mwenye kusamehe,

ingawa uliwaadhibu kwa makosa yao.

9Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu;

abuduni katika mlima wake mtakatifu!

Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ni mtakatifu.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania