Tobiti 2

Tobiti 2

Sikukuu ya jamaa

1Basi niliporejea nyumbani kwangu na kupatiwa tena mke wangu Ana na mwanangu Tobia, niliandaliwa karamu kubwa wakati wa sikukuu ya Pentekoste, iliyo sikukuu takatifu ya majuma saba. Nilipokuwa nimekaa mezani na kuona vyakula vingi mezani,

2nikamwambia Tobia, “Mwanangu, nenda nje ukaangalie kama kuna maskini Myahudi mwenzetu mcha Mungu, umlete hapa. Haya! Nakungojea.”

Mauaji mjini Ninewi

3Basi, Tobia akarudi na habari hii: “Baba! Kuna mtu mmoja wa taifa letu amenyongwa, akatupwa sokoni!”

4Papo hapo, hata bila kuonja chakula changu, niliondoka kwa haraka nikamchukua huyo maiti kumficha kibandani ili nimzike saa za jioni.

5Kisha nilirudi nyumbani, nikaoga, nikala chakula changu kwa majonzi.

6Nikakumbuka maneno ya nabii Amosi:

“Sikukuu zenu zitageuka kuwa maombolezo,

na nyimbo zenu kilio.”

Nami sikuweza kuyazuia machozi yangu.

7Jua lilipotua nilitoka nje, nikachimba kaburi na kumzika marehemu.

8Lakini jirani zangu wakanidhihaki wakisema, “Mtazameni huyu! Haogopi tena! Safari ile alinusurika kuuawa kwa sababu ya kufanya hayohayo. Bahati yake alichopoka. Lakini sasa anarudia mambo yaleyale!”

Tobiti apofuka

9Jioni hiyo nilirudi nikaoga; kisha nikaenda kulala nje uani, kando ya ukuta. Kwa kuwa kulikuwa na joto sana sikujifunika uso.

10Wala sikujua ya kwamba kulikuwapo mbayuwayu ukutani juu yangu. Basi wakanidondoshea machoni mavi yao yenye moto, vigamba vyeupe vikaziba macho yangu. Niliwaendea waganga mbalimbali, lakini hakuna aliyeweza kuniponya; mwisho nikawa kipofu kabisa. Kwa miaka minne sikuweza kuona chochote. Ndugu zangu walinishughulikia sana, na Ahika alinitunza kwa miaka miwili, kisha akaenda zake nchini Elamu.

11Wakati huo ikambidi mke wangu Ana kufanya kibarua: Kufuma nguo, kama wanawake wengine.

12Mara kwa mara aliwapelekea waajiri wake nguo alizotengeneza. Siku moja, baada ya kumlipa ujira wake walimzawadisha mwanambuzi.

13Ana alipowasili nyumbani, mwanambuzi huyo akaanza kulia. Mimi nikamwuliza mke wangu, “Mbuzi huyo ametoka wapi? Umemwiba sivyo? Mrudishe kwa mwenyewe! Si halali kula vitu vilivyoibiwa!”

14Ana akaniambia: “Sivyo! Huyu mwanambuzi nimepewa zawadi pamoja na mshahara wangu.” Lakini mimi sikumwamini; nikaona haya kwa kitendo hicho alichofanya. Nilimwamuru amrudishe huyo mbuzi kwa wenyewe. Ndipo aliponijibu: “Haya basi! Wewe uliwasaidia maskini au sivyo? Matendo yako yamekupatia nini? Yaliyokupata ni dhahiri!”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania