The chat will start when you send the first message.
1Daudi alijijengea nyumba katika mji wa Daudi. Tena akalitengenezea sanduku la Mungu mahali, akalipigia hema.[#15:1—16:43 Simulizi hili (aya 15:25—16:3 zinafanana na 2 Sam 6:12-19) ambalo lahusu ufanisi wa kuchukua tena sanduku la agano, linaeleza maagizo ambayo Daudi aliwapa Walawi kuhusu ibada.]
2Kisha akasema, “Hakuna mtu mwingine yeyote atakayelibeba sanduku la Mungu isipokuwa Walawi, maana Mwenyezi-Mungu aliwachagua wao kulibeba na kumtumikia milele.”[#15:2 Aya hii na aya 13-15 zinaonesha kwamba Daudi alilichukua sanduku la agano na kuliweka Yerusalemu kwa kufuata maagizo ya sheria ya Mose (Kut 25:12-15; Kumb 10:8; 18:5).]
3Basi, akawakusanya Waisraeli wote waje Yerusalemu, ili kulileta sanduku la Mwenyezi-Mungu mahali alipolitayarishia.
4Halafu Daudi akawaita wazawa wa Aroni na Walawi:
5kutoka katika ukoo wa Kohathi, wakaja Urieli, pamoja na ndugu zake120 chini ya usimamizi wake;
6kutoka katika ukoo wa Merari wakaja Asaya pamoja na ndugu zake 220 chini ya usimamizi wake;
7kutoka katika ukoo wa Gershomu, wakaja Yoeli pamoja na ndugu zake 130 chini ya usimamizi wake;
8kutoka katika ukoo ya Elisafani, wakaja Shemaya pamoja na ndugu zake 200 chini ya usimamizi wake;
9kutoka katika ukoo wa Hebroni, wakaja Elieli pamoja na ndugu zake 80 chini ya usimamizi wake;
10na kutoka katika ukoo wa Uzieli, wakaja Aminadabu pamoja na ndugu zake 112 chini ya usimamizi wake.
11Daudi akawaita makuhani wawili: Sadoki na Abiathari, na Walawi sita: Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu;[#15:11 Hawa walikuwa makuhani au makasisi wakuu wakati wa utawala wa mfalme Daudi. Sadoki alihudumu katika mahali patakatifu kule Gibea (16:39), hali Abiathari alihudumu kule Yerusalemu (taz 18:16). Baadaye, Solomoni alimwondoa Abiathari kwa sababu alikuwa amemuunga mkono Adonia katika harakati zake za kutaka kunyakua ufalme (1Fal 1:7; 2:26-27). Kitendo hicho kilimwacha Sadoki na wazawa wake kama familia pekee ya kikuhani kule Yerusalemu.]
12akawaambia, “Nyinyi ni viongozi wa koo za Walawi. Jitakaseni pamoja na ndugu zenu, ili mkalilete sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hadi mahali ambapo nimelitayarishia.[#15:12 Katika desturi za kidini za Agano la Kale mtu ambaye alikubalika kufanya au kushiriki katika ibada alitakiwa kuwa “safi”, au asiye “najisi”. Mtu aliyekuwa na magonjwa fulani fulani, aliyegusa maiti au aliyevunja sheria na miiko fulani fulani alichukuliwa kuwa najisi na hakustahili kushiriki kwa namna yoyote mambo ya ibada. Ili kuwa “safi” taratibu fulani za kutawadha zilifanyika. Taz Kut 30:18-21; 40:31-32.]
13Kwa sababu hamkulibeba safari ya kwanza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alituadhibu kwani hatukulitunza kama alivyoagiza.”
14Basi, makuhani na Walawi wakajitakasa ili wapate kulileta sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
15Walawi wakalibeba mabegani mwao wakitumia mipiko yake kama Mose alivyoamuru, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu.[#15:15 Taz 16:40 maelezo.]
16Daudi pia aliwaamuru wakuu wa Walawi wachague baadhi ya ndugu zao wawe wakiimba na kupiga ala za muziki: vinanda, vinubi na matoazi kwa nguvu, ili kutoa sauti za furaha.[#15:16-24 Upendeleo wa muziki kwa ajili ya ibada unaonekana mara kwa mara katika vitabu vya Mambo ya Nyakati. Taz hasa: 1Nya 6:31-47; 9:15-16,33; 18:8; 16:40-43; 23:5; 25:1-7; 2Nya 5:12-13; 7:6; 23:13; 29:25-30; 34:12. Jambo hili bila shaka lilitokana na hamu ya kurudisha tena ibada sahihi wakati Waisraeli waliporudi kutoka uhamishoni kule Babuloni.]
17Hivyo wakachagua watu wafuatao katika koo za waimbaji: Hemani mwana wa Yoeli, Asafu nduguye aliyekuwa mwana wa Berekia na wana wa Merari, ndugu zao, na Ethani mwana wa Kushaya.
18Kisha wakawachagua Walawi wafuatao wawe wasaidizi wao kwa kushika nafasi ya pili: Zekaria, Yaasieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Benaya, Maaseya, Matithia, Elifelehu na Mikneya na walinzi wa lango: Obed-edomu na Yeieli.
19Hemani, Asafu na Etani wakachaguliwa kupiga matoazi ya Shaba.
20Zekaria, Azieli, Shemiramothi, Yehieli, Uni, Eliabu, Maaseya na Benaya, walikuwa wapiga vinubi vya sauti ya Alamothi.
21Lakini Matithia, Elifelehu, Mikneya, Obed-edomu, Yeieli na Azazia waliongoza wakiwa na vinubi vya sauti ya Sheminithi.
22Naye Kenania kwa sababu ya ujuzi wa muziki aliokuwa nao, aliwekwa kuwa kiongozi wa wote.
23Berekia na Elkana walikuwa walinzi wa sanduku la agano.
24Shebania, Yoshafati, Nethaneli, Amasai, Zekaria, Benaya na Eliezeri, waliokuwa makuhani, waliwekwa kupiga tarumbeta mbele ya sanduku la Mungu. Obed-edomu na Yehiya waliwekwa pia kuwa walinzi wa sanduku.
25Basi, Daudi, wazee wa Waisraeli na makamanda wa maelfu, wakaenda kulichukua sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu kutoka nyumbani kwa Obed-edomu kwa shangwe.
26Wakamtolea tambiko Mungu: mafahali saba na kondoo madume saba kwa sababu aliwasaidia wale Walawi waliolibeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.[#15:26 Tambiko hilo lilikuwa la kumshukuru Mungu. Idadi saba ilifikiriwa kuwa ni idadi kamilifu.]
27Daudi alikuwa amevaa joho la kitani safi, hali kadhalika na Walawi wote waliobeba sanduku, waimbaji na Kenania kiongozi wa waimbaji. Mbali na joho hilo, Daudi alikuwa amevaa kizibao cha kitani.[#15:27 Kiebrania ni “efodi”, vazi ambalo lilivaliwa kama sketi (kutoka kiunoni mpaka magotini), au kama vesti ambayo ilivaliwa tu na makuhani. Taz Kut 28:31-43.]
28Hivyo, Waisraeli wote walijumuika pamoja kwa shangwe kulichukua sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu hadi Yerusalemu. Walilisindikiza kwa mlio wa baragumu, tarumbeta, matoazi, na sauti kubwa za vinanda na vinubi.
29Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipokuwa linaingia katika mji wa Daudi, Mikali, binti Shauli, alichungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi akicheza na kushangilia, basi akamdharau moyoni mwake.[#15:29 Alikuwa mmoja wa wake za Daudi. Alifikiri kwamba kitendo cha Daudi cha kucheza na kushangilia hakikuwa sawa kwa mtu ambaye aliteuliwa kuwa mfalme.]