The chat will start when you send the first message.
1Kisha Daudi aliambiwa, “Sikiliza, Wafilisti wanaushambulia mji wa Keila na wanapora nafaka kwenye viwanja vya kupuria.”[#23:1 Mji huu ulikuwa kusini mwa Adulamu (taz 22:1 maelezo), mahali ambapo Daudi alikuwa anakaa. Kulingana na aya ya 3 Keila haukuwa chini ya Waisraeli wala Wafilisti.; #23:1 Ingawa kule kwa Wafilisti kuiba nafaka kunaweza kueleweka kwamba walikuwa wanaihitaji, inawezekana pia kwamba walitaka, kwa kufanya hivyo, kuwafanya Waisraeli wakose chakula na hivyo wasipate nguvu ya kupigana nao.]
2Basi, Daudi akamwomba Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti hawa?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Ndiyo, nenda ukawashambulie Wafilisti na kuuokoa mji wa Keila.”
3Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Kama tukiwa hapahapa Yuda tunaogopa, itakuwaje basi, tukienda Keila na kuyashambulia majeshi ya Wafilisti?”
4Daudi akamwomba tena shauri Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Inuka uende Keila kwani nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”
5Basi, Daudi akaenda Keila pamoja na watu wake, na huko akapigana na Wafilisti, akawaua Wafilisti wengi na kuteka nyara ng'ombe wengi. Hivyo Daudi aliwaokoa wakazi wa Keila.
6Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipokimbilia kwa Daudi huko Keila, alikwenda na kizibao cha kuhani.[#23:6 Hapa kizibao cha kuhani si sawa na vazi la kuhani bali ni namna ya kifuko au kasha ambamo kulikuwa na yale mawe ya kauli (Urimu na Thumimu). Taz Kut 28:30 maelezo; rejea pia Kumb 32:8; 1Sam 14:41.]
7Shauli alipoambiwa kuwa Daudi amekwisha fika Keila, akasema, “Mungu amemtia mikononi mwangu kwani amejifungia mwenyewe kwa kuingia katika mji wenye malango yenye makomeo.”
8Hivyo, Shauli aliyaita majeshi yaende Keila na kufanya mashambulizi, ili kumzingira Daudi pamoja na watu wake.
9Daudi aliposikia mipango miovu ya Shauli dhidi yake, akamwambia kuhani Abiathari, “Kilete hapa hicho kizibao cha kuhani.”
10Kisha Daudi akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa hakika mimi mtumishi wako, nimesikia kwamba Shauli anapanga kuja kuangamiza mji wa Keila kwa sababu yangu.
11Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli? Je, Shauli atakuja kweli kama nilivyosikia mimi mtumishi wako? Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nakuomba unijibu mimi mtumishi wako.”
Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Shauli atakuja.”
12Daudi akamwuliza, “Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli, mimi pamoja na watu wangu?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Watakutia mikononi mwake.”[#23:9-12 Maswali ya Daudi kwa Mwenyezi-Mungu na majibu ya Mwenyezi-Mungu hasa baada ya Daudi kumtaka Abiathari ampatie kile kizibao yanadokezea kwamba huenda hapa palitumika ile Urimu na Thumimu. Taz pia 14:1-3; 10:20-21 na 14:36-42 maelezo.]
13Kisha, Daudi na watu wake ambao walikuwa kama 600, waliondoka na kwenda popote walipoweza kwenda. Shauli aliposikia kwamba Daudi amekwisha kimbia kutoka Keila, akaiacha mipango yake yote.
14Basi, Daudi alibaki ngomeni jangwani, katika nchi ya milima ya mbuga za Zifu. Shauli alimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia Daudi mikononi mwa Shauli.
15Daudi alijua kuwa Shauli alitaka kuyaangamiza maisha yake. Daudi akawa katika mbuga za Zifu, huko Horeshi.
16Yonathani mwana wa Shauli alimfuata Daudi huko Horeshi akamtia moyo kwamba Mungu anamlinda.
17Yonathani alimwambia, “Usiogope, baba yangu Shauli hatakupata. Wewe utakuwa mfalme wa Israeli, mimi nitakuwa wa pili wako. Hata Shauli baba yangu anajua jambo hili.”[#23:16-17 Taz 18:4 maelezo. Yonathani yuko tayari kumtumikia Daudi kama kaimu wake mwaminifu.]
18Hao wote wawili, wakafanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu. Daudi akabaki mjini Horeshi na Yonathani akaenda zake nyumbani.
19Shauli alipokuwa bado huko Gibea, Wazifu wakamwendea na kumwambia, “Daudi anajificha katika nchi yetu kwenye ngome huko Horeshi, kwenye mlima Hakila, ulio upande wa kusini wa Yeshimoni.[#23:19 Taz Zab 54 (Maneno yanayotangulia Zaburi yenyewe au “kichwa cha Zaburi” katika Kiebrania).]
20Sasa, mfalme, njoo ili utekeleze yaliyomo moyoni mwako, na kwa upande wetu, jukumu letu litakuwa kumtia Daudi mikononi mwako.”
21Shauli akawajibu, “Nyinyi kweli mnanionea huruma; Mwenyezi-Mungu na awabariki.
22Nendeni, mkahakikishe tena, mjue mahali anapojificha, na ni nani amemwona mahali hapo; maana nimeambiwa kwamba yeye ni mjanja sana.
23Chunguzeni kila upande mjue mahali anapojificha, kisha mniletee habari kamili. Halafu nitakwenda pamoja nanyi na ikiwa bado atakuwa yuko huko, basi, mimi nitamsaka miongoni mwa maelfu yote ya watu wa Yuda.”
24Basi, wakaondoka kwenda Zifu, wakimtangulia Shauli.
Wakati huo, Daudi na watu wake walikuwa katika jangwa la Maoni, katika bonde la Araba kusini mwa Yeshimoni.
25Shauli na watu wake wakaanza kumtafuta Daudi. Lakini Daudi alipoambiwa habari hizo, alikwenda kujificha kwenye miamba, iliyoko katika mbuga za Maoni na kukaa huko. Shauli aliposikia habari hizo, alimfuatilia Daudi huko kwenye mbuga za Maoni.
26Shauli na watu wake walikuwa upande mmoja wa mlima, na Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima. Daudi alipokuwa anaharakisha kukimbia, Shauli naye alikuwa anamkaribia kumkamata Daudi.
27Hapo mtu mmoja akamwendea Shauli na kumwambia, “Njoo haraka; Wafilisti wanaishambulia nchi.”
28Hivyo, Shauli akaacha kumfuatilia Daudi, akaenda kupigana na Wafilisti. Ndio maana mahali hapo pakaitwa “Mwamba wa Matengano.”
29Daudi aliondoka mahali hapo, akaenda kuishi kwenye ngome ya mji wa Engedi.[#23:29 Mahali penye chemchemi, upande wa magharibi wa Bahari ya Chumvi. Palikuwa mahali muhimu palipopatikana maji mazuri ya kunywa.]