The chat will start when you send the first message.
1Mwishowe hatukuweza kuvumilia zaidi. Basi, tuliamua kubaki kule Athene peke yetu,[#3:1-4 Kisehemu hiki kina umoja wake wa kimaandishi. Aya hizi zahusu kwa jumla kisa cha Paulo kumpeleka Timotheo kule Thesalonike. Aya ya tano inarudia kama muhtasari aya 1-4. Paulo anataka kumpeleka Timotheo kule Thesalonike kwa sababu ya maneno ya wasiwasi na upendo ambayo ameeleza katika sura iliyotangulia. Kuhusu shughuli za Paulo kule Athene, taz Mate 17:16—18:1.]
2na kumtuma kwenu ndugu yetu Timotheo, ambaye ni mfanyakazi mwenzetu kwa ajili ya Mungu katika kuhubiri Habari Njema ya Kristo. Tulimtuma ili awaimarisheni na kuwafarijini,
3kusudi imani ya mtu yeyote miongoni mwenu isije ikafifia kwa sababu ya taabu hizo. Nyinyi mnajua kwamba tunapaswa kupata mateso.
4Maana, tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwaambieni kwamba tutateswa; na kama mjuavyo, ndivyo ilivyotukia.
5Ndio maana nilimtuma Timotheo kwenu. Sikuweza kungoja zaidi, na hivyo nilimtuma nipate habari za imani yenu. Isije ikawa labda Mshawishi aliwajaribuni na kazi yote tuliyofanya miongoni mwenu ikapotea bure!
6Sasa Timotheo amekwisha rudi, naye ametupa habari za kufurahisha kuhusu imani na upendo wenu. Ametuarifu kwamba mnatukumbuka daima, na kwamba mna hamu ya kutuona sisi kama nasi tulivyo na hamu ya kuwaoneni.[#3:6 Aya hii ina uhusiano na aya 1-5 kwa vile inaanza hali mpya: Timotheo alikuwa ametumwa na Paulo kwa sababu ya wasiwasi aliokuwa nao kuhusu Wathesalonike na hali yao; sasa lakini Timotheo amekwisha rudi; tena alikuwa na habari za kufurahisha. Rejea Mate 18:5.]
7Basi, habari za imani yenu zimetutia moyo katika taabu na mateso yetu yote,
8kwani sasa tunaishi kweli ikiwa nyinyi mnasimama imara katika kuungana na Bwana.
9Sasa tunaweza kumshukuru Mungu wetu kwa ajili yenu. Tunamshukuru kwa furaha tuliyo nayo mbele yake kwa sababu yenu.
10Tunazidi kumwomba Mungu usiku na mchana kwa moyo wetu wote ili atupatie fursa ya kuwaoneni uso kwa uso ili tuweze kurekebisha chochote kilichopungua katika imani yenu.[#3:10 Yaonekana kwamba Paulo aliwahi kurudi huko Thesalonike miaka kadhaa baadaye (Mate 20:1-2).]
11Tunamwomba Mungu, Baba yetu mwenyewe, na Bwana wetu Yesu, atutayarishie njia ya kuja kwenu.[#3:11-13 Katika aya hizi kuna maombi matatu ya Paulo: kwa ajili yake mwenyewe aweze kuwatembelea Wathesalonike (aya 11), Mungu aukuze upendo wa waumini (12) na awaimarishe wawe wakamilifu hata wakati wa kuja kwake Yesu (13). Kwa hilo ombi la mwisho taz Fil 1:10.]
12Bwana awawezeshe nyinyi kupendana na kuwapenda watu wote zaidi na zaidi, kama vile sisi tunavyowapenda nyinyi.
13Hivyo ataiimarisha mioyo yenu, nanyi mtakuwa wakamilifu na watakatifu mbele ya Mungu na Baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na wote walio wake.