2 Wakorintho 13

Maonyo ya mwisho na salamu

1Hii ni mara yangu ya tatu kuja kwenu. “Kila tatizo litatatuliwa kwa ushahidi wa watu wawili au watatu,” yasema Maandiko.[#13:1 Safari ya kwanza ilikuwa wakati Paulo alipolianzisha kanisa huko Korintho (taz Mate 18:1-18) na ya pili ilikuwa ile inayotajwa katika 2:1.]

2Nilikwisha sema, na kama ilivyokuwa safari ya pili, sasa nasema tena nikiwa mbali: wale wote waliotenda uovu bila kutubu, na pia wale wengine, nitakapokuja, sitakuwa na huruma.[#13:2 Au, “wakati nilipowatembelea mara ya pili”. Safari hiyo ya pili ilisababisha huzuni; taz 2:1.]

3Mtajionea wenyewe kwamba Kristo anasema ndani yangu. Kwenu Kristo si dhaifu; bali nguvu yake yafanya kazi miongoni mwenu.

4Maana hata kama alisulubiwa kwa sababu ya udhaifu, lakini sasa anaishi kwa uwezo wa Mungu. Sisi pia tu dhaifu kwa kuungana naye lakini tutaishi naye kwa uwezo wa Mungu kwa ajili yenu.[#13:4 Yahusu udhaifu wake Kristo kama mtu; yaani alikuwa mdhaifu kwa kuwa alikuwa binadamu.]

5Jichunguzeni nyinyi wenyewe mpate kujua kama kweli mnayo imani. Jichunguzeni nyinyi wenyewe. Je, hamjui kwamba Kristo Yesu yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi nyinyi mmeshindwa.[#13:5 Taz Rom 8:10; Gal 2:20; Kol 1:27.]

6Lakini natumaini kwamba nyinyi mnajua kuwa sisi hatukushindwa.

7Tunamwomba Mungu msifanye uovu wowote, lakini si kusudi tuonekane kama watu waliokwisha faulu, bali mpate kutenda mema, hata kama sisi tunaonekana kuwa tumeshindwa.

8Maana hatuwezi kuupinga ukweli; uwezo tulio nao ni wa kuuendeleza ukweli.

9Tunafurahi kwamba sisi tu dhaifu, lakini nyinyi mna nguvu; kwa hiyo tunaomba mpate kuwa wakamilifu.

10Basi, ninaandika barua hii nikiwa mbali, ili nitakapofika kwenu nisilazimike kuwa mkali kwenu kwa kutumia ule uwezo alionipa Bwana; naam, uwezo wa kujenga na si wa kubomoa.

11Kwa sasa, ndugu, kwaherini! Muwe na ukamilifu, shikeni mashauri yangu, muwe na nia moja; kaeni kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.

12Salimianeni kwa ishara ya upendo. Watu wote wa Mungu huku wanawasalimuni.[#13:12 Neno kwa neno: “Kwa busu takatifu”. Kusalimiana kwa kubusu shavuni ilikuwa kawaida kwa watu wa jamaa moja au marafiki (Rom 16:16; 1Kor 16:20; 1Thes 5:26; 1Pet 5:14).]

13Neema ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na umoja wa Roho Mtakatifu, viwe nanyi nyote.[#13:13 Hapa pana maneno ya baraka yaliyotumika katika siku za mwanzo za kanisa na ambayo yajumuisha nafsi tatu za Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu (ling Mat 28:19; Mate 2:32-33; 1Kor 12:4-6; Efe 2:18; 4:4-6; 2Thes 2:13-14; 1Pet 1:2; 1Yoh 3:23-24).]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania