2 Samueli 21

2 Samueli 21

Wazawa wa Shauli wanauawa

1Wakati mmoja kulitokea njaa kali nchini Daudi akiwa mfalme. Njaa hiyo ilidumu miaka mitatu mfululizo. Daudi alimwomba Mwenyezi-Mungu shauri. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Shauli na jamaa yake wana hatia ya kumwaga damu kwa sababu aliwaua Wagibeoni.”[#21—24 Sura hizi za 21—24 zina visehemu sita vinavyosimama peke yake na vyenye umbo na muundo wa pekee: Kisehemu cha kwanza na kile cha sita ni masimulizi (21:1-14 na 24:1-25); kisehemu cha pili na cha tano ni orodha ya watu (21:15-22 na 23:8-39); na katikati ni kisehemu cha tatu na cha nne ambavyo ni vya kishairi (22:1-51 na 23:1-7).; #21:1 Huko Palestina kutokea kwa njaa ilikuwa ni jambo la kawaida kutokana na kuweko ukame au mvua ya upepo mkali vyote ambavyo vilitokea mara kwa mara na kuathiri mavuno (Mwa 12:10; 26:1; Rut 1:1-2; 1Fal 17:1; Luka 15:14; Mate 11:28). Hapa lakini inasemwa dhahiri kwamba ilikuwa ni adhabu kutoka kwa Mungu kwa sababu ya dhambi (Kumb 28:48; Yer 14:12; Eze 14:21).; #21:1 Wagibeoni waliishi katika mji wa Gibeoni na kandokando yake. Gibeoni ulikuwa mji yapata kilomita nane Kaskazini-Magharibi ya Yerusalemu. Jambo la Shauli kuwaua Wagibeoni halipatikani mahali pengine katika Biblia ila inawezekana kulihusisha na lile la kuwaua makuhani (taz 1Sam 22:6-23). Katika Yos 9:3-27 Yoshua aliahidi kwa kiapo kuwalinda Wagibeoni.]

2Hivyo, mfalme Daudi akawaita Wagibeoni (Wagibeoni hawakuwa Waisraeli ila walikuwa mabaki ya Waamori. Ingawa watu wa Israeli walikuwa wameapa kuwaacha hai, lakini Shauli alijaribu kuwaua wote kwani alikuwa na bidii ya upendeleo kwa watu wa Israeli na wa Yuda).

3Daudi akawauliza Wagibeoni, “Niwatendee nini? Nitalipaje kwa maovu mliyotendewa ili mpate kuibariki nchi hii na watu wake Mwenyezi-Mungu?”

4Wagibeoni wakamwambia, “Kisa chetu na Shauli pamoja na jamaa yake si jambo la fedha au dhahabu. Wala si juu yetu kumwua yeyote katika nchi ya Israeli.” Mfalme akawauliza tena, “Sasa mnasema niwatendee nini?”

5Wao wakamwambia mfalme, “Shauli alikusudia kutuua sisi na kutuangamiza, asiache mtu wetu yeyote katika eneo lote la Israeli.

6Basi, tukabidhi watu saba kati ya wanawe wa kiume, nasi tuwanyonge mbele ya Mwenyezi-Mungu mlimani Gibea, kwa Shauli aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu.” Mfalme akasema, “Nitawakabidhi kwenu.”[#21:6 Tafsiri yamkini ya makala ngumu ya Kiebrania.]

7Lakini mfalme alimnusuru Mefiboshethi mwana wa Yonathani kwa sababu ya kiapo ambacho Daudi na Yonathani mwana wa Shauli walikuwa wamekula kati yao kwa jina la Mwenyezi-Mungu.

8Lakini mfalme aliwachukua wana wawili ambao Rispa binti Ahiya alimzalia Shauli, Armoni na Mefiboshethi, pamoja na watoto wote watano wa kiume wa Mikali, binti Shauli ambao alimzalia Adrieli mwana wa Barzilai Mmeholathi.[#21:8 “Rispa” alikuwa suria wa Shauli ambaye Abneri, kamanda wa majeshi ya Shauli, alilala naye baada ya kifo cha Shauli (2Sam 3:7-11). “Merabu” alikuwa bintiye Shauli ambaye Shauli aliahidi kumpa Daudi awe mke wake lakini badala yake akaolewa na Adrieli, Mmeholathi (1Sam 18:19). Daudi alimwoa Mikali, dada yake Merabu, lakini Mikali hakupata watoto (6:23).]

9Watoto hao saba wa kiume Daudi aliwakabidhi kwa Wagibeoni, nao wakawatundika mlimani mbele ya Mwenyezi-Mungu, wote saba wakafa pamoja. Watoto hao waliuawa mwanzoni mwa mavuno ya shayiri.[#21:9 Wakati huo ungekuwa mwishoni mwa mwezi Aprili.]

10Kisha, Rispa binti Aya alichukua nguo ya gunia, akajitandikia mwambani. Alikaa hapo tangu mwanzo wa mavuno mpaka wakati wa mvua ulipowadia na kuinyeshea maiti. Wakati huo wote, aliwafukuza ndege wa angani na wanyama wa porini, usiku na mchana, ili wasifikie maiti hizo.[#21:10 Kutumia nguo hiyo ilikuwa ishara ya maombolezo.]

11Daudi aliposikia yale aliyofanya Rispa binti Aya, suria wa Shauli,

12alikwenda na kuichukua mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe kutoka wakazi wa Yabesh-gileadi, waliokuwa wameiiba kutoka mtaani huko Beth-sheani, ambako Wafilisti walikuwa wamemtundika Shauli na Yonathani siku ile Wafilisti walipomuua Shauli mlimani Gilboa.

13Basi, Daudi akairudisha mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe kutoka huko; halafu wakakusanya mifupa ya vijana saba waliotundikwa.

14Basi, watu wa Daudi wakaizika mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe katika nchi ya Benyamini, huko Sela katika kaburi la Kishi baba yake Shauli. Walifanya kila kitu ambacho mfalme aliamuru. Baada ya hayo, Mungu akayasikiliza maombi kuhusu nchi yao.[#21:13-14 Maneno hayo yanaonesha kwamba walau jambo la haki lilifanyika na kwamba baada ya kuzika mifupa ya Shauli na Yonathani muda ule wa miaka mitatu ya ukame ulikwisha (aya 1).]

Vita dhidi ya majitu ya Wafilisti

(1 Nya 20:4-8)

15Kisha Wafilisti walifanya vita tena na Waisraeli. Naye Daudi na watu wake wakaenda kupigana na Wafilisti. Daudi alichoka sana siku hiyo.

16Ishbi-benobu, mmojawapo wa wazawa wa majitu ambaye mkuki wake wa shaba ulikuwa na uzito wa karibu kilo tatu na nusu na aliyekuwa amejifunga upanga mpya alisema atamuua Daudi.[#21:16: Hao wanajulikana kama “Warefai” (taz Kumb 2:11). Kama inavyoelezwa hapa, walikuwa watu wakubwa ambao waliishi katika eneo hilo kabla ya Waisraeli kuiteka nchi ya Kanaani.]

17Lakini Abishai mwana wa Seruya, alikwenda kumsaidia Daudi. Abishai alimshambulia yule Mfilisti na kumwua. Hivyo, watu wakamwapia Daudi wakisema, “Hutakwenda tena nasi vitani, la sivyo utaizima taa ya ufalme katika Israeli.”

18Baada ya hayo, kulitokea tena mapigano na Wafilisti huko Gobu. Huko Sibekai, Mhushathi, alimuua Safu aliyekuwa mmojawapo wa wazawa wa Warefai.

19Kulitokea tena mapigano na Wafilisti huko Gobu. Naye Elhanani mwana wa Yaareo-regimu, Mbethlehemu, alimuua Goliathi Mgiti, ambaye mpini wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumanguo.[#21:19 Kadiri ya 1Sam 17 Daudi ndiye aliyemwua jitu moja lililoitwa kwa jina hilo na ambalo liliwafedhehesha Waisraeli. Hapa huyu Goliathi yamkini ni mtu mwingine. Wengine wanafikiri, kadiri ya 1 Nya 20:5 huyu alikuwa ndugu yake yule Goliathi wa kisa cha Daudi.; #21:19 Taz pia 1Sam 17:7 ambamo neno hilo hilo linatumiwa. Huo ulikuwa mti mkubwa alioutumia mfumanguo katika kusokotea nyuzi za kufuma nguo.]

20Baadaye kulitokea tena vita huko Gathi ambako kulikuwa na mtu mmoja alikuwa mkubwa kwa kimo, na mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu, jumla yake vidole ishirini na vinne. Yeye pia alikuwa mzawa wa majitu.

21Alipowadhihaki Waisraeli, Yonathani mwana wa Shimei, nduguye Daudi, alimuua.

22Hao wanne walikuwa wazawa wa majitu huko Gathi, nao waliuawa na Daudi pamoja na watumishi wake.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania