The chat will start when you send the first message.
1Sasa yahusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanywa kwetu pamoja, tukae naye. Ndugu, tunawaombeni sana
2msifadhaike upesi moyoni, na wala msitiwe wasiwasi kwa sababu ya madai kwamba siku ya Bwana imekwisha fika. Labda inadhaniwa kwamba jambo hili limetokana na uaguzi fulani, mahubiri au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu.[#2:2 Baadhi wanafikiri kulikuwa na barua fulani ambayo iliiga kwa kudanganya mtindo wa kuandika wa Paulo na ambayo ilisema kwamba kurudi kwake Yesu kulikwisha tukia. Wengine wanafikiri ilikuwa barua ya kweli ya Paulo aghalabu 1Thes ambayo waliielewa visivyo.]
3Msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa namna yoyote ile. Maana siku hiyo haitakuja mpaka kwanza ule uasi utokee na yule Mwovu aonekane, ambaye mwisho wake ni kuangamizwa kabisa.[#2:3 Neno ambalo limetafsiriwa hapa kama “uasi” hutumika kwa maana ya uasi dhidi ya serikali na pia kwa maana ya kukana imani kwa Mungu. Katika sehemu hii ya 2:2-12 mwandishi anatumia dhana au mawazo kutoka A.K. (taz Dan 11:36-37 na Eze 28:2) ambazo zinafanana na “chukizo haribifu” la Dan 9:27; 11:31; 12:11. Picha hiyo hapa yahusu mtu atakayetokea nyakati za mwisho kama mpinzani wa Mungu na wa Yesu Kristo. Rejea 1Yoh 2:18; na taz pia Ufu 13:1-2 maelezo.]
4Yeye hujikuza yeye mwenyewe juu ya kila kitu wanachokiona watu kuwa ni mungu, au wanachokiabudu; hata ataingia na kuketi ndani ya hekalu la Mungu akijidai kuwa Mungu.
5Je, hamkumbuki kwamba niliwaambieni haya yote wakati nilipokuwa pamoja nanyi?
6Lakini kuna kitu kinachomzuia sasa, nanyi mwakijua kitu hicho. Basi, huyo Mwovu ataonekana wakati wake ufaao.[#2:6-9 Maneno “kitu kinachomzuia”, “mtu anayemzuia” yanafafanuliwa kwa maana mbalimbali ingawaje ukweli ni kwamba si yamkini ni kitu au mtu gani.]
7Hata hivyo, Mwovu huyo aliyefichika anafanya kazi sasa, lakini hataonekana mpaka yule anayemzuia aondolewe.
8Hapo ndipo Mwovu atakapotokea; lakini Bwana Yesu anapokuja atamuua kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kwa mng'ao wa kuja kwake.[#2:8 Isa 11:4. Katika A.K. pumzi ya Mungu kila mara inafikiriwa kuwa na nguvu. Katika Yobu 4:8-9 tunasoma jinsi watu waovu wanavyoangamizwa kwa pumzi ya Mungu. Taz pia Ufu 19:11-16.]
9Huyo Mwovu atakuja na nguvu za Shetani na kufanya kila namna ya miujiza na maajabu ya uongo,[#2:9 Rejea Mat 24:24. Hapa Shetani ndiye anayemsaidia au kumtumia yule Mwovu kuwadanganya watu.]
10na kutumia udanganyifu wa kila namna kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea. Hao watapotea kwa sababu hawakuupokea na kuupenda ule ukweli ili waokolewe.
11Ndiyo maana Mungu amewaweka chini ya nguvu ya upotovu, wauamini uongo.
12Matokeo yake ni kwamba wote wasioamini ukweli, bali wanafurahia dhambi, watahukumiwa.
13Tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu nyinyi ndugu, nyinyi mnaopendwa na Bwana, kwa maana Mungu amewateua tangu mwanzo mpate kuokolewa kwa nguvu ya Roho, mfanywe watu wake watakatifu kwa imani yenu katika ukweli.[#2:13 Rejea Rom 8:29-30; Efe 1:4-5,11.; #2:13-15 Paulo anamshukuru Mungu hapa, lakini tofauti na shukrani zake katika 1:3-4 ambapo anamshukuru Mungu kwa sababu ya mambo ambayo Wathesalonike wametenda, hapa anamshukuru Mungu kwa sababu ya mambo ambayo Mungu mwenyewe amewatendea.]
14Mungu aliwaitieni jambo hili kwa njia ya Habari Njema tuliyowahubirieni; aliwaiteni mpate kupokea sehemu yenu katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.
15Basi, ndugu, simameni imara na kuzingatia yale mafundisho tuliyowafundisheni kwa mahubiri yetu na barua yetu.
16Tunamwomba Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu ambaye alitupenda na kwa neema yake akatujalia faraja ya milele na tumaini jema,[#2:16 Neno “faraja” hapa linatumika kwa maana ya utulivu katika dhiki; Paulo analitumia mara nyingi zaidi kuliko waandishi wengine wa A.J. na kila mara katika mazingira ya shida au mateso. Vilevile, kama vile katika 1Thes 4:13-18, jambo la kurudi kwake Yesu Kristo ni sababu mwafaka kabisa ya kuwa na matumaini na kutia moyo. Nalo neno “milele” linatumika kwa maana ya kudumu daima au isiyo na mwisho.]
17aifariji mioyo yenu na kuwaimarisheni ili muweze daima kutenda na kusema yaliyo mema.