The chat will start when you send the first message.
1Ndugu Theofilo, Katika kitabu cha kwanza niliandika juu ya mambo yote Yesu aliyotenda na kufundisha tangu mwanzo wa kazi yake[#1:1 Labda jina la mtu mashuhuri (jina lenyewe lina maana ya “Mpenda Mungu”), au linatumiwa hapa kumaanisha msomaji yeyote mpenda Mungu. Taz maelezo ya Luka 1:1.; #1:1 Yaani Injili iliyoandikwa na Luka (taz Luka 1:1-4).]
2mpaka siku ile alipochukuliwa mbinguni. Kabla ya kuchukuliwa mbinguni aliwapa maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua.[#1:2 Luka 24:50-52; Mate 1:6-11.; #1:2 Baada ya kufufuka kwake Yesu, namna ya kuwafundisha mitume wake inafanyika kwa mtindo mpya. Yesu anawapa maagizo kwa Roho Mtakatifu. Nao wanafunzi wake watatekeleza mafundisho yake tangu wakati huo na baadaye kwa nguvu ya Roho Mtakatifu (aya 4-5,8; taz pia Luka 24:49; Yoh 20:22). Luka anatilia mkazo kuhusika kwake Roho Mtakatifu katika shughuli yote ya kuhubiri Injili. Hata mwanzoni mwa kazi yake Yesu kulingana na Luka 4:1,14,18 nafasi muhimu ya kuhusika kwake Roho Mtakatifu inaonekana dhahiri. Taz pia Fahirisi.]
3Kwa muda wa siku arubaini baada ya kifo chake aliwatokea mara nyingi kwa namna ambazo zilithibitisha kabisa kwamba alikuwa hai. Walimwona, naye aliongea nao juu ya ufalme wa Mungu.[#1:3 Taz pengi katika Injili ambapo Yesu aliwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka: Mat 28:16-20; Marko 16:12-19; Luka 24:13-51; Yoh 20:19-21,25; na pia 1Kor 15:5-7.; #1:3 Ni jambo ambalo lilikuwa kitovu katika mahubiri ya mitume na mahubiri yake Yesu mwenyewe (taz Mat 4:17; Mate 8:12; 19:8; 20:25; 28:29,23,31). Taz pia Fahirisi.]
4Wakati alipokutana pamoja nao aliwaamuru hivi: “Msiondoke Yerusalemu, bali ngojeni ile zawadi aliyoahidi Baba, ambayo mlikwisha nisikia nikiongea juu yake.[#1:4 Au: “alipokaa pamoja nao”; au: “alipokaa kula pamoja nao”. Neno la Kigiriki lina maana mbili.; #1:4 Yaani Roho Mtakatifu (taz Yoh 14:26; 15:26-27; 16:12-13); ahadi hiyo inatimia kwa kuja kwake Roho Mtakatifu (sura ya 2).]
5Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache, nyinyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”[#1:5 Yohane Mbatizaji alikuwa ametamka na kutabiri kwamba Masiha angewabatiza watu wake kwa Roho Mtakatifu (Mat 3:11; Marko 1:8; Luka 3:16; Yoh 1:33).]
6Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, “Je, Bwana, wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?”[#1:6 Matazamio ya wanafunzi kuhusu jukumu la Masiha au Mkombozi ambaye Mungu angemleta duniani hayakuwa tofauti sana na yale ya Wayahudi wengine: walitazamia utawala wa kisiasa utakaoanzishwa na mmoja wa wazawa wa Daudi. Katika Mat 20:21 ni dhahiri kwamba wanafunzi walidhani Yesu angeanzisha utawala wa kidunia na tabaka kadha wa kadha za mamlaka.]
7Lakini Yesu akawaambia, “Nyakati na majira ya mambo hayo viko chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini.
8Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni nyinyi, mtapokea nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia.”[#1:8 Ushuhuda ambao wanafunzi watatoa juu ya Yesu, hasa ni juu ya ufufuo wake 1:22; 2:32; 3:15; 4:33; 5:32; 13:31; 22:15 na Luka 24:48; lakini pia ni ushuhuda juu ya maisha yake yote.; #1:8 Aya hii ni muhtasari wa kitabu chote cha Matendo ya Mitume. Tunaambiwa kwa kifupi sana juu ya hatua mbalimbali za kuenea kwa Injili au Habari Njema juu ya Yesu: Mitume wanahubiri huko Yerusalemu (sura 1—7), kisha Yudea na Samaria (sura 8—9) na kuendelea yaani pamoja na Kaisarea, Antiokia, Asia Ndogo, Ugiriki na Roma (sura 20—28).]
9Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena.[#1:9 Katika Agano la Kale wingu ni ishara ya kutokea au kuweko kwake Mungu (k.m.: Kut 13:21-22; 24:12-18). Taz pia Mat 17:1-8 na sehemu sambamba katika Injili.]
10Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao,[#1:10 Namna ya kawaida ya kuwaeleza malaika. Nguo nyeupe ni sare ya kitamaduni ya A.K. na A.J. ya malaika.]
11wakasema, “Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni atakuja tena namna hiyohiyo mlivyomwona akienda mbinguni.”[#1:11 Yaani katika wingu na kwa utukufu mkuu.; #1:11 Mitume wote isipokuwa tu Yuda (ambaye hapa hayupo) walitoka Galilaya.]
12Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka ule mlima uitwao Mlima wa Mizeituni ulioko karibu kilomita moja kutoka mjini.[#1:12 Huo uko karibu kilomita moja kutoka Yerusalemu, na huo ni umbali ambao iliruhusiwa kutembea siku ya Sabato.; #1:12 Neno kwa neno: umbali wa safari ya Sabato; yapata nusu maili.]
13Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo.[#1:13 Neno la Kigiriki lamaanisha “kukaa mahali kwa muda na sio daima”.; #1:13 Au, Mzalendo.; #1:13 Orodha hii ni sawa na ile ya Luka 6:14-16. Katika Mat 10:2-4 na Marko 3:16-19 tuna Thadayo badala ya Yuda mwana wa Yakobo.]
14Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake.[#1:14 Kuhusu kuweko kikundi cha ndugu zake Yesu taz 1Kor 9:5; Marko 6:3; Mat 12:46. Katika Biblia kama vile katika tamaduni za Kiswahili neno “ndugu” liliweza kutumiwa kuwataja ndugu waliozaliwa na mama mmoja na pia ndugu wa jamaa ya karibu (taz k.m. Mwa 13:8; 14:16; 29:15; Lawi 10:4; 1 Nya 23:22).]
15Siku moja baadaye, Petro alisimama kati ya wale ndugu waumini ambao walikuwa wamekusanyika, wote jumla watu 120,[#1:15 Petro ni mtu maarufu miongoni mwa wale mitume kumi na wawili, na hasa katika sura 1—12 za Matendo ya Mitume.]
16akasema, “Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi, alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu nguvuni.[#1:16 Neno hili lilitumiwa pia na Wayahudi kuwataja Wayahudi wananchi wenzao (Mate 2:29; 3:17) nao Wakristo wakalichukua na kulitumia pia kutaja uhusiano uliopo miongoni mwao wenyewe (Mate 6:3; 9:30; 1Kor 5:11; Efe 6:23).; #1:16 Yaani sehemu za Zaburi ambazo zinakaririwa katika aya ya 20. Taz pia Zab 41:9. Zaburi nyingi kabla na baada ya Kristo zilifikiriwa kuwa zenye kusema juu ya Masiha na wakati wake.]
17Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu, maana alichaguliwa ashiriki huduma yetu.”
(
18Yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na kitendo chake kiovu, akaanguka chini, akapasuka na matumbo yake yakamwagika nje.[#1:18 Kulingana na Mat 27:5 Yuda alijinyonga.; #1:18-19 Aya hizi zina maneno au habari iliyoingizwa katikati ya hotuba halisi ya Petro; taz Mat 27:3-10 ambapo tunaambiwa makuhani wakuu ndio walionunua shamba hilo la mfinyanzi.]
19Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba “Akel Dama,” maana yake, “Shamba la Damu.”)
20“Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi:
‘Makao yake yabaki mahame;
mtu yeyote asiishi ndani yake.’
Tena imeandikwa:
‘Mtu mwingine achukue nafasi yake ya huduma.’
21Basi, mtu mmoja miongoni mwa wale walioandamana nasi muda wote Bwana Yesu alipokuwa anasafiri pamoja nasi achaguliwe kujiunga nasi.
22Huyo anapaswa kuwa mmoja wa wale walioandamana nasi tangu Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa kutoka kwetu kwenda mbinguni. Huyo atashiriki pamoja nasi jukumu la kushuhudia ufufuo wake Yesu.”[#1:22 Au:]
23Hapo, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia.
24Kisha wakasali: “Bwana, wewe unaijua mioyo ya watu wote. Hivyo, utuoneshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua[#1:24 Ni vigumu kujua kama Bwana hapa yahusu Mungu au Yesu. Lakini 1:2 yaonesha zaidi kuwa Yesu ndiye aliyewachagua mitume na huenda wanamwomba sasa achague mmoja.]
25ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda mahali pake mwenyewe.”[#1:25 Tafsiri nyingine yamkini: (mahali pa adhabu; taz Luka 16:28).]
26Wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja.[#1:26 Yaonekana uchaguzi huo ulifanyika kwa namna inayofanana na ile ya matumizi ya Urimu na Thumimu katika A.K. (taz Lawi 16:8 n.k.). Majina yaliyoandikwa juu ya vijiwe yaliwekwa chomboni na kutikiswa; jiwe la kwanza kudondoka lilibainisha aliyechaguliwa. Baadaye uchaguzi unafanywa na Roho Mtakatifu (taz 6:3-6; 13:2-3).]