The chat will start when you send the first message.
1Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika mahali pamoja.[#2:1 Neno kwa neno: (majuma saba baada ya sikukuu ya Pasaka. Taz pia fahirisi). Siku hiyo iliadhimishwa siku ya 6 ya mwezi Sivani (yapata tarehe 20 mwezi Mai kalenda yetu) kukumbuka agano alilofanya Mungu na Waisraeli mlimani Sinai. Huko Yerusalemu walikusanyika watu makundi kwa makundi ya Wayahudi waliotoka nchi mbalimbali.]
2Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikaijaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa.[#2:2 Upepo au pumzi (Kiebrania na Kigiriki hutumia neno moja tu lenye maana zote mbili) ni kielezo kinachotumika kuelezea kuweko au kutokea kwake Roho wa Mungu (taz k.m. Eze 37:9,14; Yoh 3:8).]
3Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao.[#2:3 Habari au picha tunayopewa hapa k.m. inatangulia kueleza kile kitakachotokea na kutajwa katika aya ya 4. Yafaa kutaja hapa kwamba moto ni ishara ya: kuweko kwake Mungu (Kut 3:2), au: ishara ya hukumu (Mat 3:12) na muundo wa mioto hiyo (ndimi Isa 5:24) hapa unahusiana na kipaji cha lugha.]
4Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha.[#2:4 Katika Luka 24:49 Yesu alisema kwamba atawapelekea yule ambaye Mungu aliahidi kuwapelekea wanafunzi wake. Kwa hiyo kitendo hicho ni kukamilishwa kwa ahadi hiyo. Tukio hilo la kuongea lugha mbalimbali ladhihirisha kwa kielezo kwamba Injili au Habari Njema itawafikia watu wote wa lugha zote duniani.]
5Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani.[#2:5-6 Wanaohusika hapa ni Wayahudi waliotoka sehemu mbalimbali za dunia ya wakati ule, wakakaa huko Yerusalemu; wengi wao waliongea au kufahamu lugha nyingine, licha ya Kiaramu ambacho kilikuwa lugha ya kawaida huko Yerusalemu wakati huo.]
6Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
7Walistaajabu na kushangaa wakisema, “Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya?
8Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe?
9Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelamu; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia,[#2:9-11 Nchi zinazotajwa hapa ni kuanzia eneo la Persia, upande wa mashariki, mpaka Libia, upande wa magharibi; na sehemu hiyo yote ndio ulimwengu uliojulikana wakati huo.]
10Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libia karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma,
11Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu.”[#2:11 Watu wasio Wayahudi ambao waliingizwa katika dini ya Kiyahudi kwa kutolea sadaka hekaluni na wa kiume kutahiriwa.]
12Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, “Hii ina maana gani?”
13Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, “Watu hawa wamelewa divai mpya!”[#2:13 Au:]
14Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: “Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu.[#2:14-40 Hotuba ya Petro ni mtindo wa mahubiri ya kitume au ya mitume wakati wanapowahubiria Wayahudi, na jambo hilo ladhihirika wakati Petro analazimika kuongea (3:13-26; 4:10-12; 5:30-32; 10:36-43). Hapa tuna mojawapo ya muhtasari na kitovu cha ujumbe ambao mitume waliutangaza. (Taz pia Mate 13:23-41; 1Kor 15:1-8).]
15Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi?[#2:15 Wayahudi walihesabu vipindi vya siku kuanzia asubuhi, jua linapoanza kuchomoza; saa hiyo ilikuwa wakati wa kusali asubuhi, wakati ambapo Myahudi hangekuwa amekula wala kunywa kitu.]
16Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli:
17‘Katika siku zile za mwisho, asema Bwana,[#2:17-18 Watu wote, bila kujali tofauti kati ya mwanamume na mwanamke, watoto na wazee, watakumbwa na karama au kipaji cha unabii yaani cha kutangaza mambo ambayo Mungu amesema.]
nitawamiminia binadamu wote Roho wangu.
Watoto wenu wa kiume na wa kike watatoa unabii,
vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18Naam, hata watumishi wangu wa kiume na kike,
nitawamiminia Roho wangu siku zile,
nao watatoa unabii.
19Nitatenda miujiza juu angani,
na ishara chini duniani;
kutakuwa na damu, moto na moshi mzito;
20jua litatiwa giza,
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana.
21Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.’[#2:17-21 Sehemu hii imekaririwa kutoka kitabu cha Yoeli 3:1-5 kulingana na tafsiri ya Kigiriki ya Agano la Kale, pamoja na mageuzi madogo. Maneno ya aya 17 hayapo katika A.K.]
22“Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua.[#2:22 Yafuata mafundisho kiini ambayo yalikuwa msingi wa mahubiri ya kawaida ya mitume. Mahubiri haya yanatolewa hapa kwa mara ya kwanza kwa kifupi. Taz 2:14-39; 3:12-26; 4:8-12; 5:29-32; 10:34-43.; #2:22 Hatujui chanzo cha maana halisi ya msemo huo ambao Yesu anatajwa hivyo mara nyingi katika Matendo ya Mitume (2:22; 3:6; 4:10; 6:14; 22:8; 24:5; 26:9). Katika 24:5 Wakristo wa kwanza wanasemwa kuwa kikundi cha Wanazareti, na Yesu ni kiongozi wao.; #2:22 Maneno mawili ambayo yanamaanisha miujiza aliyotenda Yesu na ambayo kwayo Mungu alithibitisha kwamba alikuwa amemtuma. Maajabu na ishara, yaani miujiza, itaambatana na mahubiri ya mitume vilevile na hivyo kuthibitisha utume wao (2:43; 4:30; 5:12; 6:8; 14:3; 15:12).]
23Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe.
24Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge.[#2:24 Taz Mat 28:5-6 na sehemu sambamba; Mate 4:10; 5:30.; #2:24 Msemo ambao yamkini unamaanisha kile ambacho Zaburi 18:4 inakiita “kamba za kifo” (makala ya Kiebrania) ambapo tafsiri ya Septuajinta ina “maumivu ya kifo”, shina la neno la Kiebrania lina maana ya “maumivu” na pia “kamba”.]
25Maana Daudi alisema juu yake hivi:
‘Nilimwona Bwana mbele yangu daima;
yuko nami upande wangu wa kulia hata sitatikisika.
26Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi;
tena nilipiga vigelegele vya furaha.
Mwili wangu utakaa katika tumaini,
27maana hutaiacha roho yangu kuzimu,
wala kumruhusu mtakatifu wako aoze.
28Umenionesha njia za uhai,
umenijaza furaha kwa kuwako kwako!’
29“Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya mambo yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake liko papa hapa petu mpaka leo.
30Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu alimwapia kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake.[#2:30 Ni hapa tu katika Biblia ambapo Daudi anatajwa kama nabii. Petro aliposema kwamba Daudi alikuwa nabii, alimaanisha kwamba alisema ujumbe wa Mungu katika Zaburi na kwamba Yesu alifufuliwa kutoka kwa wafu ni kielelezo cha kile alichosema Daudi karne nyingi zilizopita.]
31Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: ‘Hakuachwa kuzimu, mwili wake haukuoza.’
32Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo.
33Yesu alipokwisha pandishwa na kuwekwa na Mungu upande wake wa kulia, akapokea kutoka kwake Baba yule Roho Mtakatifu ambaye alituahidi, ametumiminia huyo Roho. Hicho ndicho mnachoona sasa na kusikia.[#2:33 Yaani mahali pa heshima na uwezo pamoja na Mungu (Zab 110:1 ambayo imekaririwa katika aya 34).]
34Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema:
‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
Keti upande wangu wa kulia,
35hadi niwafanye adui zako kiti cha miguu yako.’
36“Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulubisha, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana na Kristo.”
37Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: “Ndugu zetu, tufanye nini?”
38Petro akajibu, “Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile ahadi ya Roho Mtakatifu.[#2:38 Yaani kumtambua Yesu kama Masiha na kuomba kwa jina lake.; #2:38 Taz Mat 3:2,11 na sehemu sambamba; vilevile Mat 4:17; Marko 1:14-15; Luka 24:47, na Mate 3:19; 20:21; 26:20.]
39Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake.”[#2:39 Hapa yahusu watu wasio Wayahudi, Isa 57:19.]
40Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na kuwahimiza watu akisema, “Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu.”
41Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao 3,000 wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo.[#2:41 Luka anarudiarudia, tena kwa makusudi maalumu, jambo la kukua kwa Kanisa: 2:47; 4:4; 5:14; 6:1,7; 11:21,24; 13:48-49; 16:5. Taz utangulizi.]
42Hawa wote waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kindugu, kumega mkate na kusali.[#2:42 Kadiri ya matumizi hapa yaonekana kwamba yahusu kitendo ambacho ni cha kidini na tofauti labda na wakati wa kumega mkate (aya 40) ambapo yawezekana pia kuelewa kama “Kula chakula pamoja”; chakula cha pamoja kilijumuisha pia kukumbuka au kuadhimisha Karamu ya Bwana. Yesu alitumia mkate na divai kuonesha kwamba angetolewa sadaka kuondoa dhambi za watu jambo ambalo ni la msingi katika kufanya agano kati ya Mungu na watu wake (Mat 26:26-29; Luka 22:14-22; 1Kor 11:23-26) Wakristo huadhimisha tukio hili katika chakula kile kiitwacho Karamu ya Bwana, Komunyo takatifu au Ekaristi.]
43Miujiza na maajabu mengi yalifanyika kwa njia ya mitume hata kila mtu akajawa na hofu.
44Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawiana.
45Walikuwa wakiuza mali na vitu vyao kisha wakagawana fedha kadiri ya mahitaji ya kila mmoja.
46Waliendelea kukutana pamoja kila siku hekaluni. Lakini wakati wa kumega mkate, walikutana katika nyumba zao na wakakishiriki chakula hicho kwa furaha na moyo mkunjufu.[#2:46 Fungu la maneno lililotokana na desturi ya Kiyahudi ya kuomba baraka kabla ya kula na baadaye kumega mkate rasmi. Maneno hayo yalikuja kutumiwa kwa maaana ya pekee baadaye na Wakristo juu ya kuadhimisha Karamu ya Bwana (Mate 2:42; 20:7,11; 27:35; 1Kor 10:16).]
47Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa.