Matendo 20

Matendo 20

Paulo anakwenda tena Makedonia na Ugiriki

1Ile ghasia ya Efeso ilipokwisha tulia Paulo aliwaita pamoja wale waumini, akawatia moyo. Kisha akawaaga, akasafiri kwenda Makedonia.

2Alipitia sehemu za nchi zile akiwatia watu moyo kwa maneno mengi. Halafu akafika Ugiriki

3ambako alikaa kwa miezi mitatu. Alipokuwa anajitayarisha kwenda Siria, aligundua kwamba Wayahudi walikuwa wanamfanyia mpango mbaya; hivyo aliamua kurudi kwa kupitia Makedonia.[#20:3 Labda wakati wa masika ya mwaka 56-57 B.K. Wakati ambapo Paulo aliandika barua kwa Waroma (Rom 15:25-28).]

4Sopatro, mwana wa Pirho, kutoka Berea, aliandamana naye; pia Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike, Gayo kutoka Derbe, Timotheo, Tukiko na Trofimo wa mkoa wa Asia.[#20:4 Walioandamana na Paulo walikuwa wawakilishi wa makanisa yaliyopeleka zawadi zao kule Yerusalemu (1Kor 16:3-4). Huenda Sopatro alikuwa mtu yule yule anayetajwa katika Rom 16:29 hali Trofimo anatajwa pia katika 21:29 na 2Tim 4:20.]

5Hao walitutangulia na kutungojea kule Troa.[#20:5 Hapa habari inaanza tena kusimuliwa kwa kutumia wingi (sisi tu…).]

6Sisi, baada ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, tulipanda meli kutoka Filipi na baada ya siku tatu tukawafikia kule Troa. Huko tulikaa kwa muda wa juma moja.[#20:6 Taz Mate 12:3-4 maelezo.]

Kukutana na waumini wa Troa kwa mara ya mwisho

7Jumamosi jioni tulikutana ili kumega mkate. Kwa vile Paulo alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliwahutubia watu na kuendelea kuongea nao hadi usiku wa manane.[#20:7 Neno kwa neno: Wayahudi walihesabu siku ya kwanza ya juma mara Sabato ilipokwisha, yaani jioni yapata saa 9-10 alasiri. Hapo ndipo ilipoanza siku ya kwanza ya Juma, yaani Jumapili. Basi kwa kukumbuka siku ya ufufuo wa Yesu (Mat 28:1; Marko 16:1-2,9; Luka 24:1; Yoh 20:1,19) hiyo siku ilikuwa kwa waumini wa kwanza siku maalumu ya kukutana. Hapa na katika 1Kor 16:2 na tena mara nyingi katika maandishi ya karne ya kwanza B.K. yahusu kile walichokiita “Siku ya Bwana” (Ufu 1:10). Siku hiyo ya Jumapili walikutana (taz 2:42), yaani kuadhimisha Karamu ya Bwana, ambayo ilikwisha adhimishwa kule Yerusalemu (2:42,46).]

8Katika chumba tulimokuwa, ghorofani, kulikuwa na taa nyingi zinawaka.

9Kijana mmoja aitwaye Eutuko alikuwa ameketi dirishani wakati Paulo alipokuwa anaendelea kuhutubu. Eutuko alianza kusinzia kidogokidogo na hatimaye usingizi ukambana, akaanguka chini kutoka ghorofa ya tatu. Wakamwokota amekwisha kufa.

10Lakini Paulo alishuka chini, akainama, akamkumbatia na kusema, “Msiwe na wasiwasi maana kuna uhai bado ndani yake.”

11Kisha akapanda tena ghorofani, akamega mkate, akala. Aliendelea kuhubiri kwa muda mrefu hadi alfajiri, halafu akaondoka.

12Wale watu walimchukua yule kijana hadi nyumbani akiwa mzima kabisa, wakapata kitulizo kikubwa.

Safari kutoka Troa kwenda Mileto

13Sisi tulipanda meli tukatangulia kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Ndivyo alivyopanga; maana alitaka kufika huko kwa kupitia nchi kavu.

14Basi, alitukuta kule Aso, tukampandisha melini, tukaenda Mitulene.[#20:14 Bandari ya kisiwa cha Lesbo, pwani ya mashariki ya Asia Ndogo.]

15Kutoka huko tulisafiri tukafika Kio kesho yake. Siku ya pili, tulitia nanga Samo na kesho yake tukafika Mileto.[#20:15 Kisiwa kusini mwa Lesbo, mkabala na pwani ya Smurna.; #20:15 Bandari kusini mwa Efeso.]

16Paulo alikuwa amekusudia kuendelea na safari kwa meli bila kupitia Efeso ili asikawie zaidi huko Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kwa sikukuu ya Pentekoste kama ingewezekana.[#20:16 Taz 2:1 maelezo.]

Paulo anawaaga wazee wa Efeso

17Kutoka Mileto Paulo alituma ujumbe kwa wazee wa Efeso wakutane naye.

18Walipofika kwake aliwaambia, “Mnajua jinsi nilivyokaa nanyi siku zote tangu siku ile ya kwanza nilipofika Asia.[#20:18 Efeso ulikuwa mji wa kwanza wa mkoa wa Asia ambao Paulo aliutembelea; taz 18:19, na pia maelezo ya 19:10.]

19Mnajua jinsi nilivyomtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, kwa machozi na matatizo yaliyonipata kutokana na mipango ya hila ya Wayahudi.

20Mnajua kwamba sikusita hata kidogo kuwahubiria hadharani na nyumbani mwenu na kuwafundisha chochote ambacho kingewasaidieni.

21Niliwaonya wote — Wayahudi, kadhalika na watu wa mataifa, wamgeukie Mungu na kumwamini Bwana wetu Yesu.

22Sasa, sikilizeni! Mimi, nikiwa ninamtii Roho, nakwenda Yerusalemu bila kufahamu yatakayonipata huko.[#20:22 Ling na aya 23 na Mate 16:6-7; 19:21. tafsiri nyingine yamkini, ingawaje hafifu zaidi: au:]

23Ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu ananithibitishia katika kila mji kwamba vifungo na mateso ndivyo vinavyoningojea.

24Lakini, siuthamini uhai wangu kuwa kitu sana kwangu mradi tu nikamilishe ule utume wangu na ile kazi aliyonipa Bwana Yesu niifanye, yaani nishuhudie Habari Njema ya neema ya Mungu.

25“Nimepita miongoni mwenu nyote nikiuhubiri ufalme wa Mungu. Sasa lakini, najua hakuna hata mmoja wenu atakayeniona tena.

26Hivyo, leo hii ninawathibitishieni rasmi kwamba ikijatokea akapotea mmoja wenu, mimi sina lawama yoyote.

27Kwa maana sikusita hata kidogo kuwatangazieni azimio lote la Mungu.

28Jihadharini wenyewe; lilindeni lile kundi ambalo Roho Mtakatifu amewaweka nyinyi muwe walezi wake. Lichungeni kanisa la Mungu ambalo amejipatia kwa damu ya Mwanae.[#20:28 Yaani, au: Neno la Kigiriki “Episkopos” limetupatia neno letu Kwa kutaja watu haohao neno (Kigiriki: “presbuteros”) linatumiwa pia katika aya 17. Ling Fil 1:1; na angalia Tito 1:6-7.; #20:28 Maneno: yaweza kueleweka kama]

29Nafahamu vizuri sana kwamba baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali watawavamieni, na hawatakuwa na huruma kwa kundi hilo.[#20:29-30 Waalimu wa uwongo ambao watajiingiza katika kundi (Mat 7:15 Ling na Marko 13:22; 2Pet 2:1; pia Kumb 31:29). Watu wanaotajwa katika aya ya 30 watazuka kutoka ndani ya jumuiya. Ling na 1Tim 1:2-3 na Ufu 2:2-7, ujumbe waliopelekewa baadaye watu haohao wa Efeso.]

30Hata kutoka miongoni mwenu watatokea watu ambao watasema mambo ya uongo ili kuwapotosha watu na kuwafanya wawafuate wao tu.

31Kwa hiyo, muwe macho mkikumbuka kwamba kwa muda wa miaka mitatu, usiku na mchana, sikuchoka kumwonya kila mmoja wenu kwa machozi.[#20:31 Kwa kukadiria; Ling na 19:8,10.]

32“Na sasa basi, ninawaweka nyinyi chini ya ulinzi wa Mungu na ujumbe wa neema yake. Yeye anao uwezo wa kuwajenga na kuwawezesha mzipate zile baraka alizowawekea watu wake.

33Mimi sikutamani hata mara moja fedha, wala dhahabu, wala nguo za mtu yeyote.[#20:33-34 Ling na 1Sam 12:3-5.]

34Mnajua nyinyi wenyewe kwamba nimefanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe, ili kujipatia mahitaji yangu na ya wenzangu.

35Nimekuwa nikiwapeni daima mfano kwamba kwa kufanya kazi mithili hiyo tunapaswa kuwasaidia walio dhaifu, tukikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe: ‘Heri zaidi kutoa kuliko kupokea.’”[#20:35 Maneno ya Yesu ambayo hayakuandikwa katika Injili (lakini angalia Luka 6:38).]

36Baada ya kusema hayo, Paulo alipiga magoti pamoja nao wote, akasali.

37Wote walikuwa wanalia, na kumwaga kwa kumkumbatia na kumbusu.

38Jambo lililowahuzunisha zaidi lilikuwa neno alilosema kwamba hawangemwona tena. Basi, wakamsindikiza hadi melini.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania