Matendo 6

Matendo 6

Wasaidizi saba wa mitume

1Baadaye, idadi ya wanafunzi ilipokuwa inazidi kuongezeka, kulitokea manung'uniko kati ya waumini walioongea Kigiriki na wale walioongea Kiebrania. Wale walioongea Kigiriki walinung'unika kwamba wajane wao walikuwa wanasahauliwa katika ugawaji wa mahitaji ya kila siku.[#6:1 Luka anatumia neno hili hapa kwa mara ya kwanza baada ya Luka 22:45. Katika Matendo neno hili linatumiwa kuwataja waumini kwa jumla na sio mitume peke yao.; #6:1 Yaani Wayahudi walioongokea Ukristo na ambao walisema lugha ya Kigiriki (wengine wao walizaliwa nje ya Palestina) na waliitwa “Waheleni” na Wayahudi walioongokea Ukristo lakini walisema Kiaramu au Kiebrania na kufuata desturi na mila za Kiebrania (Ling Mate 21:20).]

2Kwa hiyo, mitume kumi na wawili waliita jumuiya yote ya wanafunzi, wakasema, “Si vizuri sisi tuache kulihubiri neno la Mungu ili tushughulikie ugawaji wa mahitaji.[#6:2 Neno kwa neno ni “kuhudumu mezani”. Lakini neno la Kigiriki “meza” linaweza kuwa na maana ya mahitaji au hata shughuli zinazoambatana na fedha.]

3Hivyo, ndugu zetu, chagueni miongoni mwenu watu saba wenye sifa njema, waliojawa na Roho na wenye hekima; nasi tutawakabidhi jukumu hilo.

4Sisi, lakini, tutashughulika na sala na kazi ya kuhubiri neno la Mungu.”

5Jambo hilo likaipendeza jumuiya yote ya waumini. Wakawachagua Stefano, mtu mwenye imani kubwa na mwenye kujaa Roho Mtakatifu, Filipo, Prokoro, Nikanori, Timona, Parmena na Nikolao wa Antiokia ambaye wakati mmoja alikuwa ameongokea dini ya Kiyahudi.[#6:5 Ya Siria; taz Mate 11:19 maelezo.; #6:5 Tunazo habari yingine zaidi juu ya huyo katika Mate 6:8—7:60 na juu ya katika Mate 8:4-13,26-40; 21:8-9; huyu Filipo si yule Filipo, mmoja wa wale Mitume kumi na wawili. Naye Stefano, kutokana na hotuba yake katika sura 7, inaonekana kwamba hakuwa Myahudi.]

6Wakawaweka mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono.[#6:6 Kuwawekea watu mikono katika Matendo ya Mitume kunafanywa katika mazingira mbalimbali: kumpatia mtu mamlaka kuhusu jukumu fulani au wadhifa fulani (kama hapa katika 6:6; Hes 27:23; na 1Tim 4:14); kumpatia mtu zawadi au kipaji cha Roho Mtakatifu (Mate 8:17; 19:5-6); kumpeleka mtu kwa ziara fulani hasa ya kuhubiri n.k. (Mate 13:3); na kwa kumponya mtu mgonjwa (Mate 9:12,17; 28:8).]

7Neno la Mungu likazidi kuenea na idadi ya waumini huko Yerusalemu ikaongezeka zaidi, na kundi kubwa la makuhani wakaipokea imani.

Stefano anatiwa nguvuni

8Mungu alimjalia Stefano neema tele, akampa nguvu nyingi hata akawa anatenda miujiza na maajabu kati ya watu.[#6:8 Shahidi wa kwanza Mkristo (Mate 7:54-60). Stefano, kama vile Bwana Yesu, alifanya na na pia, na kama vile Yesu, alishtakiwa kwamba alisema maneno ya kumkashifu Mungu na hekalu (aya 13-14). Maneno yake ya mwisho (Mate 7:59-60) yanatukumbusha pia yale maneno ya Yesu.]

9Lakini watu fulani wakatokea ili wabishane na Stefano. Baadhi ya watu hao walikuwa wa sunagogi moja lililoitwa “Sunagogi la Watu Huru”, nao walitoka Kurene na Aleksandria; wengine walitoka Kilikia na Asia.[#6:9 Hao walikuwa watumwa wa Kiyahudi ambao walipewa uhuru; wengi wao walikuwa wamerudi kutoka nchi za nje ya Palestina na waliongea Kigiriki.]

10Lakini hawakuweza kumshinda kwa sababu ya hekima yake na kwa sababu ya yule Roho aliyemwongoza wakati aliposema.

11Kwa hiyo waliwahonga watu kadhaa waseme: “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kumkashifu Mose na kumkashifu Mungu.”

12Kwa namna hiyo, waliwachochea watu, wazee na waalimu wa sheria. Basi, wakamjia Stefano, wakamkamata na kumleta mbele ya Baraza Kuu.

13Walileta Barazani mashahidi wa uongo ambao walisema, “Mtu huyu haachi kamwe kusema maneno ya kupakashifu mahali hapa patakatifu na sheria ya Mose.[#6:13-14 Ling na Mat 26:59-61; Marko 14:57-58, ambapo yasemwa kwamba Yesu alishtakiwa mashtaka kama hayohayo mbele ya Baraza Kuu hilohilo.]

14Kwa maana tulikwisha msikia akisema eti huyo Yesu wa Nazareti atapaharibu kabisa mahali hapa na kufutilia mbali desturi zile tulizopokea kutoka kwa Mose.”

15Wote waliokuwa katika kile kikao cha Baraza walimkodolea macho Stefano, wakauona uso wake umekuwa kama wa malaika.[#6:15 Uso wa Stefano unaonekana hivyo kudhihirisha kwamba hana hatia na baadaye katika 7:55-56 atajaliwa maono ya mbinguni.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania