The chat will start when you send the first message.
1Malkia Esta alimwomba Mungu kwa siku tatu. Kisha akavua mavazi aliyokuwa amevaa wakati huo, akavalia mavazi yake ya kifahari.
2Akajiremba kimalkia. Baada ya kumwomba Mungu Mwokozi, aonaye yote, akawachukua vijakazi wake wawili, akaondoka chumbani mwake,[#D:2 Taz Yud 10:1-4; 12:15.]
3amejiegemeza na mmoja wao amtegemeze,
4hali mjakazi mwingine aliwafuata nyuma akiwa ameshika mwisho wa shela la malkia Esta.
5Malkia alionekana mwenye uso unaong'aa kwa uzuri. Alionekana mwenye furaha kama mwanamke anayependwa, lakini moyoni alijaa hofu kubwa.
6Alipokwisha kupita milango yote, alisimama mbele ya mfalme. Mfalme alikuwa ameketi kwenye kiti chake cha enzi, akiwa amevaa mavazi yake rasmi ya kifalme ambayo yalikuwa yametariziwa kwa dhahabu na vito vya thamani. Alionekana wa kutisha sana.
7Basi, mfalme aliinua macho yake yaliyojaa fahari, akamwangalia malkia Esta kwa hasira kali. Esta akanyong'onyea na rangi yake ikageuka; na karibu azimie, hivyo akalazimika kuinamisha kichwa chake kwenye bega la mtumishi mwanamke.
8Hapo, Mungu akaibadili roho ya mfalme yenye hasira kuwa yenye huruma kwa Esta. Haraka, mfalme akanyanyuka kutoka kwenye kiti chake cha enzi, akamshika Esta mkono mpaka Esta alipoweza kusimama wima mwenyewe. Mfalme akamtuliza Esta kwa maneno matamu na laini,
9akamwuliza, “Una nini Esta? Mimi ni mumeo, usiniogope.
10Sheria zetu zinawahusu raia wa kawaida tu; wewe hutauawa. Njoo karibu.”[#D:10 Yahusu sheria ya kifalme ambayo iliagiza mtu yeyote auawe kama atamwendea mfalme bila kualikwa kufanya hivyo. Taz pia 4:11 maelezo.]
11Kisha mfalme akainua fimbo yake ya dhahabu ya kifalme na kumgusa nayo malkia shingoni.
12Akamkumbatia na kumwambia, “Niambie unachotaka.”
13Malkia akasema, “Nilipokutazama ee bwana wangu, nilijiona kama natazama malaika wa Mungu, na moyo wangu ukanidunda kwa hofu kwa sababu ya utukufu wako.
14Kweli unastaajabisha sana na uso wako umejaa neema.”
15Lakini malkia alipokuwa anaongea akazimia tena.
16Mfalme akafadhaika sana kwa hali hiyo ya Esta, na matowashi wote wa mfalme wakajaribu kumfariji Esta.