The chat will start when you send the first message.
1Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Basi, simameni imara wala msikubali tena kuwa chini ya nira ya utumwa.[#5:1 Paulo anatumia neno “nira” ambalo lahusu kipande cha mti ambacho ng'ombe hufungwa shingoni kumdhibiti alimapo, kama picha kamili ya utumwa (wa sheria na dhambi).]
2Sikilizeni! Ni mimi Paulo ninayesema nanyi! Kama mkikubali kutahiriwa, Kristo hatawafaidia chochote.[#5:2-4 Kukubali kutahiriwa kama sharti la kupata wokovu (taz Gal 1:6-9 maelezo) ilifuata kwamba ni lazima matakwa yote ya sheria yafuatwe, hali ambayo ingemaanisha kwamba imani kwa Kristo haina maana, nayo neema ya Mungu ni bure (Gal 2:21).]
3Nasema tena wazi: kila anayekubali kutahiriwa itambidi kuishika sheria yote.
4Kama mnatazamia kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria, basi, mmejitenga mbali na Kristo; mko nje ya neema ya Mungu.
5Kwa upande wetu, lakini, sisi tunangojea kwa matumaini kwa nguvu ya Roho tufanywe waadilifu kwa njia ya imani.
6Maana ikiwa tumeungana na Kristo Yesu, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana; cha maana ni imani ifanyayo kazi kwa mapendo.[#5:6 Imani, kadiri ya Paulo, si shauri la orodha ya ujuzi wa mambo fulani ya dini au hata nia tu. Imani inaungana na utii (Rom 1:5; 6:16) na hujidhihirisha kwa njia ya upendo. Taz pia Yak 2:14 maelezo.]
7Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi, aliyewazuia kuuzingatia ukweli?
8Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni.
9“Chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!”[#5:9 Taz 1Kor 5:6 maelezo. Maneno hayo ni msemo au methali inayoashiria uovu mkubwa unaosababishwa na kitu kinachoonekana hakina madhara.]
10Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba nyinyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni — awe nani au nani — hakika ataadhibiwa.
11Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote.[#5:11 Rejea 1Kor 1:23. Kwa wale ambao Paulo anawashutumu, wazo la kupata wokovu kwa kumwamini Yesu aliyesulubiwa, bila kuwa na haja ya kutahiriwa na kujiweka chini ya sheria ya Mose, lilikuwa jambo la aibu.]
12Laiti hao wanaowavurugeni wangejihasi wenyewe![#5:12 Inaonekana kwamba Paulo anashauri kwamba hao wapinzani wake waendelee hata zaidi, wajikate viungo vyao vinavyohusika. Baadhi wanafikiri hii inadokezea ibada fulani ya kipagani iliyofanyika katika Galatia. Kufanya hivyo, kama inavyotajawa katika Kumb 23:1 kungewatenga kabisa na watu wa Mungu. Taz Fil 3:2 maelezo.]
13Nyinyi ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo.
14Maana sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”
15Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana kama wanyama, jihadharini msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe!
16Basi, nasema hivi: mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia.[#5:16—6:10 Sehemu hii ya mwisho ya barua kwa Wagalatia ni mafundisho kuhusu matumizi ya uhuru katika maisha ya shughuli mbalimbali.]
17Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka nyinyi wenyewe.
18Kama mkiongozwa na Roho, basi, hamko tena chini ya sheria.
19Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: uzinzi, uasherati, ufisadi;[#5:19-21 Neno kwa neno “matunda ya mwili”, “mwili” hapa linatumika kwa maana ya eneo ambalo Roho wa Mungu hahusiki. Kuhusu orodha ya matendo ya kidunia au matendo mabaya, taz Rom 1:29-32 maelezo.]
20kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano;
21husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: watu wanaotenda mambo hayo hawataupata ufalme wa Mungu uwe wao.
22Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu,[#5:22-23 Neno kwa neno “matunda ya Roho”. Rejea Efe 5:9; Kol 3:12-15. Orodha hii ni kinyume cha orodha ya aya 19-21, upendo ukichukua nafasi ya kwanza (aya 13-14).]
23upole na kiasi. Hakuna sheria inayoweza kupinga mambo hayo.
24Wale walio na Kristo wameisulubisha hali yao ya kidunia pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
25Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake.
26Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu.