The chat will start when you send the first message.
1Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu atautwaa upanga wake mkubwa, mkali na imara, na kuliadhibu dude Lewiyathani joka lirukalo na danganyifu; Mwenyezi-Mungu ataliua joka liishilo baharini.[#27:1 Joka la kutisha katika hadithi za kale; hapa latumika kuyataja mataifa yaliyowakandamiza Waisraeli.; #27:1-13 Sehemu hii inashughulikia dhamira kadha wa kadha zisizo na uhusiano maalumu kati yake: Katika aya ya 1 mataifa mengine yatahukumiwa; Waisraeli ni shamba la mzabibu la Mungu (aya 2-6), lazima ya kuteseka (aya 7-11) lakini Waisraeli watakaosalia wataachana na uovu wao (aya 12-13).]
2Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu atasema hivi:
“Imbeni utenzi wa shamba langu zuri la mizabibu!
3Mimi, Mwenyezi-Mungu, ni mkulima wake;
nalimwagilia maji kila wakati.
ninalilinda usiku na mchana,
lisije likaharibiwa na mtu yeyote.
4Silikasirikii tena shamba hili;
kama miiba na mbigili ingelilivamia,
mimi ningepambana nayo na kuichoma moto.
5Maadui za watu wangu wakitaka ulinzi wangu,
basi, na wafanye amani nami;
naam, wafanye amani nami.”
6Itakuja siku wazawa wa Yakobo watashika mizizi;[#27:6 Maneno yanayotaja kitu kilekile (Isa 5:7).]
naam, watu wa Israeli watachanua na kuchipua,
na kuijaza dunia yote kwa matunda.
7Mungu hakuwaadhibu Waisraeli vikali
kama alivyowaadhibu maadui wake;
Waisraeli waliopotea vitani,
ni wachache kuliko wale wa maadui zake.
8Aliwaadhibu watu wake kwa kuwapeleka uhamishoni.
Wakati wa upepo mkali wa mashariki,
aliwaondoa kwa kipigo kikali.
9Hivi ndivyo uovu wa wazawa wa Yakobo utakavyoondolewa,
hivi ndivyo dhambi yake itakavyofutwa kabisa:
ataziharibu madhabahu za miungu;
mawe yake yatasagwasagwa kama chokaa;
Ashera, wala madhabahu za kufukizia ubani hazitabaki.
10Mji ule wa ngome sasa umekuwa mtupu,[#27:10 Yahusu mji fulani ambao ulikuwa adui wa Yerusalemu (rejea Isa 24:10; 26:5).]
umeachwa na kuhamwa kama jangwa,
humo ndama wanalisha na kupumzika.
11Matawi ya miti yamekauka na kuvunjika;
kina mama huyaokota wakawashia moto.
Watu hawa hawajaelewa kitu,
kwa hiyo Mungu, Muumba wao, hatawahurumia,
yeye aliyewafanya, hatawafadhili.
12Siku hiyo, kutoka mto Eufrate hadi mpakani mwa Misri, Mwenyezi-Mungu ataipura nafaka yake, nanyi Waisraeli mtakusanywa mmojammoja.[#27:12 Maneno “Kutoka mto Eufrate … hadi mpakani mwa Misri” yanamaanisha eneo lote lililochukuliwa kuwa eneo la Waisraeli.]
13Siku hiyo, tarumbeta kubwa itapigwa na watu wote wa Israeli waliopotea nchini Ashuru au waliotawanywa nchini Misri watarudi na kumwabudu Mwenyezi-Mungu juu ya mlima mtakatifu huko Yerusalemu.[#27:13 Zab 2:6 maelezo.; #27:12-13 Kuhusu picha na vielelezo kadha wa kadha vya kurudi kwa Waisraeli kutoka uhamishoni taz Isa 11:11-16; mavuno (Yoe 3:13; Mat 13:39; Ufu 14:15-16); kusanyiko linaloitwa kwa mlio wa tarumbeta (Hes 10:2-10; Yoe 2:15; rejea Mat 24:31; 1Thes 4:16).]