The chat will start when you send the first message.
1Mungu wenu asema:
“Wafarijini watu wangu,
nendeni mkawafariji.
2Semeni na wenyeji wa Yerusalemu kwa upole,
waambieni kwamba utumwa wao umekwisha,
wamesamehewa uovu wao.
Mwenyezi-Mungu amewaadhibu maradufu
kwa sababu ya dhambi zao zote.”
3Sauti ya mtu anaita jangwani:[#40:3 Hapa haisemwi moja kwa moja kwamba anayeita ni nabii ila neno hilo la Mungu linakuja kwa njia ya mtu ambaye ni kama fumbo. Baadhi ya wafafanuzi wanafikiri yahusu sauti kutoka kwa malaika au wajumbe wa kimbingu au wa mbinguni ambao walikwisha kuweko katika mkutano wa ushauri au halmashauri ya kimungu na hivyo wanaweza kuwasilisha kwa nabii ujumbe ambao itambidi naye kuupeleka kwa niaba ya Mwenyezi-Mungu (rejea 1Fal 22:19-23; Yobu 1:6; 2:1; Isa 6:2). Lakini wengine wanadhani hapa yahusu mtindo wa kimaandishi ambao shabaha yake ni kumweka Mwenyezi-Mungu katika hali yake inayopita mazingira ya binadamu. Hata hivyo jambo muhimu ni kutambua hatua au mwendo wa neno au ujumbe wa Mungu ambao unawafikia walengwa kwa kupitia mtu mmoja hadi hata mwingine (Zab 19:1-4). Maneno “sauti … jangwani” yanatafsiri vilivyo katika tafsiri ya Kigiriki ya Septuajinta (LXX) na kama inavyokaririwa katika Agano Jipya katika Mat 3:3; Marko 1:3; Yoh 1:23.]
“Mtayarishieni Mwenyezi-Mungu njia,
nyosheni barabara kuu kwa ajili ya Mungu wetu.
4Kila bonde litasawazishwa,
kila mlima na kilima vitashushwa;
ardhi isiyo sawa itafanywa sawa,
mahali pa kuparuza patalainishwa.
5Kisha utukufu wa Mwenyezi-Mungu utafunuliwa,[#40:5 Maana ya kibiblia ni kuonekana kwa uwezo au nguvu na ukuu na utakatifu wake Mungu kuwaokoa watu wake (Kut 33:18-23; Zab 19:1; Isa 6:3; Eze 1:28; 10:4; taz Yoh 1:14 maelezo). “Na watu wote watauona”: Kuokolewa uhamishoni Babuloni kutafanya utukufu na ukuu wake Mungu utambuliwe na watu wote. Rejea Isa 42:8; Yer 2:11.]
na watu wote pamoja watauona.
Mwenyezi-Mungu mwenyewe ametamka hayo.”
6Sikiliza! Kuna sauti inasema, “Tangaza!”[#40:6 Taz Isa 40:3 maelezo. Na kuhusu maneno “binadamu wote ni kama majani”, rejea Zab 103:15-16.]
Nami nikauliza, “Nitangaze nini?”
Naye: “Tangaza: binadamu wote ni kama majani;
uthabiti wao ni kama ua la shambani.
7Majani hunyauka na ua hufifia,[#40:7 Yobu 14:2.]
Mwenyezi-Mungu avumishapo upepo juu yake.
Hakika binadamu ni kama majani.
8Majani hunyauka na ua hufifia,
lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”
9Nenda juu ya mlima mrefu,
ewe Siyoni, ukatangaze habari njema.
Paza sauti yako kwa nguvu,
ewe Yerusalemu, ukatangaze habari njema.
paza sauti yako bila kuogopa.
Iambie miji ya Yuda:
“Mungu wenu anakuja.”
10Bwana Mungu anakuja na nguvu,
kwa mkono wake anatawala.
Zawadi yake iko pamoja naye,
na tuzo lake analo.
11Atalilisha kundi lake kama mchungaji,
atawakusanya wanakondoo mikononi mwake,
atawabeba kifuani pake,
na kondoo wanyonyeshao atawaongoza polepole.
12Nani awezaye kupima maji ya bahari kwa konzi yake,
kuzipima mbingu kwa mikono yake?
Nani awezaye kuutia udongo wa dunia kikombeni;
kuipima milima kwa mizani
au vilima kwa kipimo cha uzani?
13Nani awezaye kuiongoza akili ya Mwenyezi-Mungu,
au kuwa mshauri wake na kumfunza?
14Mwenyezi-Mungu alimtaka nani shauri,
ndipo akapata kuwa mwenye ujuzi?
Nani aliyemfunza njia za haki?
Nani aliyemfundisha maarifa,
na kumwonesha namna ya kuwa na akili?
15Kwake mataifa ni kama tone la maji katika ndoo,
ni kama vumbi juu ya mizani.
Kwake visiwa ni vyepesi kama vumbi laini.
16Kuni zote za Lebanoni
na wanyama wake wote
havitoshi kwa sadaka ya kuteketezwa mbele yake.
17Mataifa yote si kitu mbele yake;
kwake ni vitu duni kabisa na batili.
18Mtamlinganisha Mungu na nini basi,
au ni kitu gani cha kumfananisha naye?
19Je, anafanana na kinyago?
Hicho, fundi hukichonga,
mfua dhahabu akakipaka dhahabu,
na kukitengenezea minyororo ya fedha!
20Au ni sanamu ya mti mgumu?
Hiyo ni ukuni mtu anaochagua,
akamtafuta fundi stadi,
naye akamchongea sanamu imara!
21Je, nyinyi bado hamjui?
Je, hamjapata kusikia?
Je, hamkuambiwa tangu mwanzo?
Je, hamjafahamu mwanzo wa dunia?
22Dunia iliumbwa na huyo aketiye juu ya mbingu;
kutoka huko wakazi wa dunia ni kama panzi!
Yeye amezitandaza mbingu kama pazia,
na kuzikunjua kama hema la kuishi.
23Yeye huwaporomosha wakuu wenye nguvu,
watawala wa dunia huwafanya kuwa si kitu.
24Mara tu wanaposimikwa na kuanza kuota,
hata kabla hawajatoa mizizi kama miti udongoni,
Mwenyezi-Mungu akiwapulizia hunyauka,
kimbunga huwapeperusha kama makapi!
25Mungu Mtakatifu auliza hivi:
“Nani basi, mtakayemlinganisha nami?
Je, kuna mtu aliye kama mimi?”
26Inueni macho yenu juu mbinguni!
Je, ni nani aliyeziumba nyota hizo?
Ni yule aziongozaye kama jeshi lake,
anayeijua idadi yake yote,
aziitaye kila moja kwa jina lake.
Kwa sababu yeye ni mwenye nguvu nyingi,
hakuna hata moja inayokosekana.
27Enyi watu wa Israeli wazawa wa Yakobo,
kwa nini mnalalamika na kusema:
“Mwenyezi-Mungu hatujali sisi!
Mungu wetu hajali haki yetu!”
28Je, nyinyi bado hamjui?
Je, hamjapata kusikia?
Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu wa milele;
yeye ndiye Muumba wa kila kitu duniani.
Yeye hafifii kamwe wala kuishiwa nguvu.
Maarifa yake hayachunguziki.
29Yeye huwapa uwezo walio hafifu,
wanyonge huwapa nguvu.
30Hata vijana watafifia na kulegea;
naam, wataanguka kwa uchovu.
31Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu,[#40:31 Rejea Zab 25:3; 33:20-21; Isa 49:23.]
watapata nguvu mpya.
Watapanda juu kwa mabawa kama tai;
watakimbia bila kuchoka;
watatembea bila kulegea.