Isaya 64

Isaya 64

1Laiti ungalizipasua mbingu ukashuka chini,[#64:1 Kutokea kwake Mwenyezi-Mungu mara nyingine kunafananishwa na ngurumo na umeme na mtetemeko wa nchi kama inavyoelezwa katika Kut 19:16-19; taz pia Zab 18:7-9.]

milima ikakuona na kutetemeka kwa hofu!

2Ingeteketea kama moto uchomavyo kichaka,

kama vile moto uchemshavyo maji.

Njoo upate kuwajulisha maadui zako jina lako

nayo mataifa yatetemeke kwa kuwako kwako!

3Wakati ulipotenda maajabu ambayo hatukutazamia,

ulishuka chini nayo milima ikatetemeka ilipokuona.

4Tangu kale hakuna aliyepata kuona

wala kusikia kwa masikio yake;

hakuna aliyepata kumwona Mungu aliye kama wewe

atendaye mambo kwa ajili ya wale wanaomtegemea!

5Wewe waja kuwasaidia watendao haki kwa furaha,

wanaokukumbuka na kuzingatia njia zako.

Ulitukasirikia tulipokuwa wenye dhambi;

sisi tumeasi kwa muda mrefu.

6Sote tumekuwa kama watu walio najisi;

matendo yetu yote mema ni kama nguo chafu.

Sote tunanyauka kama majani,

uovu wetu watupeperusha kama upepo.

7Hakuna hata mmoja anayekuja kukuomba;

hakuna anayejishughulisha kukutafuta.

Wewe unauficha uso wako mbali nasi,

umetuacha tukumbwe na maovu yetu.

8Hata hivyo, ee Mwenyezi-Mungu, wewe ni Baba yetu.

Sisi ni kama udongo, wewe ni mfinyanzi.

Sisi sote ni kazi ya mikono yako.

9Usitukasirikie mno, ee Mwenyezi-Mungu,

usiukumbuke uovu wetu daima!

Ukumbuke kwamba sisi sote ni watu wako!

10Miji yako mitakatifu imekuwa nyika;

Siyoni umekuwa mahame,

Yerusalemu umekuwa uharibifu.

11Nyumba yetu takatifu na nzuri,

ambamo wazee wetu walikusifu,

imeteketezwa kwa moto.

Mahali petu pote pazuri pamekuwa magofu.

12Je, kwa hayo yote utajizuia usifanye kitu?

Je, utaendelea kunyamaza tu, ee Mwenyezi-Mungu,

na kututesa kupita kiasi?

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania