Mathayo 23

Mathayo 23

Yesu anawalaumu waalimu wa sheria na Mafarisayo

(Marko 12:38-39; Luka 11:43,46; 20:45-46)

1Kisha Yesu akauambia umati wa watu pamoja na wanafunzi wake,

2“Waalimu wa sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kufafanua sheria ya Mose.[#23:2 Maneno hayo yanatafsiri maneno machache katika Kigiriki ambayo neno kwa neno ni “wanaketi juu ya kiti cha Mose” maana yake ni kwamba wanayo mamlaka rasmi ya kutoa mwongozo kuhusu sheria ya Mose.]

3Kwa hiyo shikeni na kutekeleza chochote watakachowaambieni. Lakini msiyaige matendo yao, maana hawatekelezi yale wanayoyahubiri.

4Hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, lakini wao wenyewe hawataki kunyosha hata kidole wapate kuibeba.[#23:4 Neno ambalo latumiwa hapa kwa maana ya jumla ya maagizo ya kisheria magumu kuyatekeleza ambayo Mafarisayo walisisitiza yafuatwe.]

5Wao hufanya matendo yao yote ili watu wawaone. Huvaa tepe zenye maandishi ya sheria juu ya panda la uso na mikononi na hupanua pindo za makoti yao.[#23:5 Msingi wa desturi hii ni Kut 13:1-16 (hasa aya 9 na 16); Kumb 6:4-9 (hasa aya 8), na 11:18. Mafarisayo na Wayahudi wengine walizoea kuwa na tepe zilizoshonewa maandishi fulanifulani muhimu ya sheria na tepe hizo ziitwazo “filakteria” walizifunga juu ya panda la uso au katika mkono wa kulia.; #23:5 Wayahudi wenye dini sana walipanua pindo hizo kuonesha kwamba wao walishika sheria kikamilifu zaidi.]

6Hupenda nafasi za heshima katika karamu na viti vya heshima katika masunagogi.

7Hupenda kusalimiwa kwa heshima sokoni na kupendelea kuitwa na watu: ‘Mwalimu.’

8Lakini nyinyi msiitwe kamwe ‘Mwalimu,’ maana mwalimu wenu ni mmoja tu, nanyi nyote ni ndugu.

9Wala msimwite mtu yeyote ‘Baba’ hapa duniani, maana Baba yenu ni mmoja tu, aliye mbinguni.

10Wala msiitwe ‘Viongozi,’ maana kiongozi wenu ni mmoja tu, ndiye Kristo.[#23:8-10 Majina yote hayo ni ya sifa. Lakini sifa wanayotakiwa wafuasi wa Yesu kuwa nayo ni ile ya “watumishi” (23:11). Taz pia 20:26-27; Marko 9:35; 10:43-44 na Luka 22:26 na onyo la Yak 3:1. Jina “Baba” ni jina la heshima na katika A.K. lilitumika pia kumtaja Mkuu au Mwalimu (1Sam 10:12; 2Fal 2:12). Katika Agano Jipya linatumika hasa kwa Mungu (Mat 6:9 maelezo).]

11Aliye mkubwa miongoni mwenu ni lazima awe mtumishi wenu.

12Anayejikweza atashushwa, na anayejishusha atakwezwa.

Yesu analaumu unafiki

(Marko 12:40; Luka 11:39-42,44,52; 20:47)

13“Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnaufunga mlango wa ufalme wa mbinguni mbele ya macho ya watu. Nyinyi wenyewe hamwingii ndani, wala hamwaruhusu wanaotaka kuingia waingie.[#23:13 Lugha ya onyo na tangazo la hukumu, sawa kama inavyotumiwa na manabii (rejea k.m. Yer 22:13; Amo 6:1; na pia Mat 11:21; 18:7). Maneno makali ya aya 13-28 hayana sambamba katika Injili nyingine.; #23:13 Hati nyingine za kale zina aya 14: “Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo wanafiki! Mnawanyonya wajane na kujisingizia kuwa watu wema kwa kusali sala ndefu. Kwa sababu hiyo mtapata adhabu kali zaidi” (taz Marko 12:40).]

15“Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumpata mtu mmoja afuate dini yenu. Mnapompata, mnamfanya astahili maradufu kwenda katika moto wa Jehanamu kuliko nyinyi wenyewe.

16“Ole wenu viongozi vipofu! Nyinyi mwasema ati mtu akiapa kwa hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini akiapa kwa dhahabu ya hekalu, kiapo hicho kinamshika.

17Enyi vipofu wapumbavu! Kipi kilicho cha maana zaidi: dhahabu au hekalu linalofanya hiyo dhahabu kuwa takatifu?

18Tena mwasema ati mtu akiapa kwa madhabahu si kitu; lakini akiapa kwa zawadi iliyowekwa juu ya madhabahu, kiapo hicho humshika.

19Enyi vipofu! Ni kipi kilicho cha maana zaidi: ile zawadi, au madhabahu ambayo hufanya hiyo zawadi kuwa takatifu?

20Anayeapa kwa madhabahu ameapa kwa hiyo madhabahu, na kwa chochote kilichowekwa juu yake.

21Na anayeapa kwa hekalu ameapa kwa hilo hekalu na pia kwa yule akaaye ndani yake.

22Na anayeapa kwa mbingu ameapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa huyo aketiye juu yake.[#23:22 Isa 66:1; Mat 5:34.]

23Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu sehemu moja ya kumi, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndio hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine.[#23:23 Sehemu moja ya kumi ya vitu kwa sadaka; taz Lawi 27:30.; #23:23 Mmea mdogo ambao mbegu zake hupondwa na kutumiwa kukolezea chakula.; #23:23 Au, “uaminifu”. Kwa msemo wa namna hiyo juu ya yale ambayo Mungu anawataka watu afanye tazama Mika 6:8.]

24Viongozi vipofu! Mnatoa nzi katika kinywaji, lakini mnameza ngamia![#23:24 Katika wanyama wote waliochukuliwa kuwa ni najisi, miongoni mwa waliokuwa wadogo zaidi alikuwa nzi (Lawi 11:20), na aliyekuwa mkubwa kupita wote alikuwa ngamia (Lawi 11:4).]

25“Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafisha kikombe na bakuli kwa nje, lakini ndani mnaacha kumejaa vitu mlivyopata kwa unyang'anyi na uchoyo.

26Mfarisayo kipofu! Kisafishe kikombe ndani kwanza na nje kutakuwa safi pia.[#23:26 Muhimu ni usafi wa ndani. Usafi wa nje hauwezi kuleta usafi wa ndani.]

27“Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mko kama makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, lakini ndani yamejaa mifupa ya maiti na kila namna ya uchafu.[#23:27 Paulo anatumia picha hiyohiyo katika Matendo 23:3.]

28Hali kadhalika nyinyi mnaonekana na watu kwa nje kuwa wema, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.

Adhabu inakuja

(Luka 11:47-51)

29“Ole wenu waalimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya watu wema.

30Mwasema: ‘Kama sisi tungaliishi nyakati za wazee wetu hatungalishirikiana nao katika mauaji ya manabii!’

31Hivyo mnathibitisha nyinyi wenyewe kwamba nyinyi ni watoto wa watu waliowaua manabii.[#23:31 Au, “wazawa.” Neno lenyewe laweza kumaanisha sio tu uhusiano wa mtoto na mzazi ila pia “mwenye tabia kama ya mtu fulani”. Katika Luka 11:48 ni maana ya pili inayotumika.]

32Haya, kamilisheni ile kazi wazee wenu waliyoianza![#23:32 Yaani, kwa kumuua Yesu pia (21:35-39).]

33Enyi kizazi cha nyoka wenye sumu! Mnawezaje kuiepa hukumu ya moto wa Jehanamu?

34Ndio maana mimi ninawapelekea nyinyi manabii, watu wenye hekima na waalimu; mtawaua na kuwasulubisha baadhi yao, na wengine mtawapiga viboko katika masunagogi yenu na kuwasaka katika kila mji.

35Hivyo lawama yote itawapateni kwa ajili ya damu yote ya watu wema iliyomwagwa juu ya ardhi. Naam, tangu kumwagwa damu ya Abeli ambaye hakuwa na hatia, mpaka ile ya Zakaria, mwana wa Barakia, ambaye mlimuua hekaluni kati ya patakatifu na madhabahu.[#23:35 Mtu wa kwanza aliyeuawa kikatili (taz Mwa 4:8-10).; #23:35 Huenda alikuwa Zakaria mwana wa Yoyada (2Nya 24:20-22); aliuawa hekaluni kwa amri ya mfalme Yoashi. Kwa vile kulingana na orodha ya vitabu vya Biblia ya Kiebrania ambapo kitabu cha 2Nya kati ni cha mwisho, hapo Zakaria ni mtu wa mwisho aliyeuawa kikatili; na kwa kusema hivyo Yesu alimaanisha wote waliouawa bila hatia.]

36Nawaambieni kweli, kizazi hiki kitapata adhabu kwa sababu ya mambo haya.

Jinsi Yesu alivyoupenda mji wa Yerusalemu

(Luka 13:34-35)

37“Yerusalemu! Ee Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako. Mara ngapi nimejaribu kuwakusanya watoto wako kwangu, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka.[#23:37 Picha au mfano wa kutilia mkazo kuhusu ulinzi wa Mungu (taz pia Luka 13:35; ling Kumb 32:10-12; Zab 17:8; 36:7; 57:1; 61:4; 91:4).]

38Haya basi, nyumba yako itaachwa mahame.[#23:38 Yaweza kuwa na maana ya mji wote wa Yerusalemu au maana ya hekalu lenyewe (taz 24:1; Yer 22:5; ling Eze 10:18).]

39Nakuambia, hutaniona tena mpaka wakati utakaposema:

‘Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana.’”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania