Marko 2

Marko 2

Yesu anamponya mtu aliyepooza

(Mat 9:1-8; Luka 5:17-26)

1Baada ya siku kadhaa, Yesu alirudi Kafarnaumu, watu wakapata habari kwamba alikuwa nyumbani.[#2:1 Yamkini nyumbani kwa Petro. Rejea 1:29 na taz 7:17.]

2Basi, wakaja watu wengi sana hata nafasi yoyote ikakosekana mlangoni. Yesu alikuwa akiwahubiria ujumbe wake,

3wakati mtu mmoja aliyepooza alipoletwa kwake akiwa amechukuliwa na watu wanne.

4Kwa sababu ya huo umati wa watu, hawakuweza kumpeleka karibu na Yesu. Basi, wakatoboa sehemu ya paa iliyokuwa juu ya mahali alipokuwa Yesu. Walipokwisha pata nafasi, wakamteremsha huyo mtu akiwa amelala juu ya mkeka.[#2:4 Nyakati hizo, kwa wingi sana, nyumba za huko Palestina paa zake zilitengenezwa kwa kulaza boriti na kuezekwa kisha kufunikwa kwa matope yaliyokaushwa (rejea pia Luka 5:19).]

5Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.”[#2:5 Jambo la kuwa na imani katika A.J. ni muhimu sana. Hapa, hao watu wana imani au tegemeo kubwa kwa Yesu kuhusu uwezo wake wa kuponya, nayo inasababisha Yesu kuchukua hatua: “Mwanangu umesamehewa dhambi zako.” Kwa jumla ugonjwa ulichukuliwa kuwa ni matokeo ya dhambi; Yesu anamwondolea huyo aliyeipooza dhambi zake kabla ya kumponya kimwili, na kuponyeshwa kwa huyo aliyepooza ni hakikisho kwamba Yesu anao uwezo wa kuwaondolea watu dhambi, uwezo ambao ni wa Mungu, kama inavyodhihirika katika aya 7-12 (rejea pia Yak 5:15). Taz pia Luka 7:48; 2Sam 12:13; 2Nya k 7:14; Zab 41:4; 103:3; Isa 38:17; Yer 3:22.]

6Baadhi ya waalimu wa sheria waliokuwa wameketi hapo wakawaza mioyoni mwao,

7“Anathubutuje kusema hivyo? Anamkufuru Mungu! Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake.”

8Yesu alitambua mara mawazo yao, akawaambia, “Mbona mnawaza hivyo mioyoni mwenu?

9Ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kumwambia, ‘Inuka! Chukua mkeka wako utembee?’

10Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anayo mamlaka ya kuwasamehe watu dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza,[#2:10 Jina ambalo Yesu alilitumia mara nyingi kujitaja yeye mwenyewe (2:28; 8:31,38; 9:9,12,31; 10:33,45; 13:26; 14:21,41,62). Kwa maelezo zaidi taz orodha ya maneno.]

11“Nakuambia simama; chukua mkeka wako uende nyumbani!”

12Mara, watu wote wakiwa wanamtazama, huyo mtu akainuka, akauchukua mkeka wake, akaenda zake. Watu wote wakashangaa na kumtukuza Mungu wakisema, “Hatujapata kamwe kuona jambo kama hili.”

Lawi anaitwa

(Mat 9:9-13; Luka 5:27-32)

13Yesu alikwenda tena kando ya ziwa. Umati wa watu ukamwendea, naye akaanza kuwafundisha.[#2:13 Yaani ziwa Galilaya.]

14Alipokuwa akipita, akamwona Lawi mwana wa Alfayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Lawi akasimama, akamfuata.[#2:14 Jina hilo latumika hapa tu na katika Luka 5:27-32. Katika Mat 9:9-13 huyu Lawi anatajwa kama Mathayo.]

15Baadaye, Yesu alikuwa amekaa mezani, nyumbani kwa Lawi, kula chakula. Watozaushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wamemfuata Yesu na wengi wao wakawa wamekaa mezani pamoja naye na wanafunzi wake.[#2:15 Mafarisayo waliwachukulia watu ambao hawakufuata sheria kama wao kuwa watu wenye dhambi; kadhalika na watu ambao walishughulikia mambo ambayo Mafarisayo waliyaona kuwa ni ya sifa mbaya. Kula pamoja nao ilikuwa jambo lisilokubalika kwa vile kula pamoja ni ishara ya umoja na urafiki. Miongoni mwa watu ambao walidharauliwa na Mafarisayo ni watozaushuru kwa vile, licha ya kwamba walishirikiana na wakoloni Waroma, katika shughuli zao za kukusanya kodi hawakuwa waaminifu.]

16Basi, baadhi ya waalimu wa sheria ambao walikuwa Mafarisayo walipomwona Yesu akila pamoja na watu wenye dhambi na watozaushuru, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini anakula pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?”[#2:16 Mafarisayo walikuwa kikundi cha kidini cha Wayahudi ambao walisisitiza kushika sheria katika kila hali ya maisha. Katika Injili hawa wanaonekana mara nyingi kama wapinzani wa Yesu na mahubiri yake (taz 2:18,24; 3:6; 7:1,5; 8:11,15; 10:2; 12:13).]

17Yesu alipowasikia, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, ila wenye dhambi.”

Suala juu ya kufunga

(Mat 9:14-17; Luka 5:33-39)

18Wakati mmoja wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa Mafarisayo walikuwa wanafunga. Basi, watu wakaja, wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wa Yohane na wa Mafarisayo wanafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”[#2:18 Mat 9:14; Luka 7:8-23; 11:1; Yoh 1:35; 3:25-30.; #2:18 Kufunga, yaani kujinyima chakula na kinywaji kwa sababu za kidini, ilikuwa desturi iliyotokana na A.K. (Lawi 16:29; Zek 7:5 na pia Ezra 8:21-23).]

19Yesu akajibu, “Je, walioalikwa harusini hutakiwa kufunga wakati bwana arusi yupo pamoja nao? Wakati wote wawapo pamoja na bwana arusi hawawezi kufunga.[#2:19 Mfano wa harusi na bwana na bibi harusi unatumika pengine katika A.J. kueleza mkataba wa Mungu wa kuwaokoa watu (Mat 22:1-14; 25:1-13; 2Kor 11:2; Efe 5:31-32; Ufu 19:7; 21:2 na katika A.K. Isa 54:4-8; 62:4-5; Eze 16:1-63; Hos 2:19).]

20Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.[#2:20 Yahusu kifo cha Yesu. Baada ya kifo chake wafuasi wake watafunga kama ishara ya maombolezo.]

21“Watu hawakati kiraka cha nguo mpya na kukishonea katika nguo kuukuu. Kama wakifanya hivyo, hicho kiraka kipya kitararuka kutoka hilo vazi kuukuu, nalo litaharibika zaidi.[#2:21-22 Kwa misemo hiyo miwili juu ya kiraka kipya - vazi kuukuu na divai mpya - viriba vikuukuu, Yesu anamaanisha kwamba ujumbe wake mpya unahitaji mtazamo na mwelekeo mpya katika watu na sio mtazamo na mwelekeo wa kale. Taz pia Mat 9:16-17.]

22Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu. Kama wakifanya hivyo, divai itavipasua hivyo viriba, nayo divai pamoja na hivyo viriba vitaharibika. Divai mpya hutiwa katika viriba vipya!”[#2:22 Hivi vilitengenezwa aghalabu kwa ngozi za mbuzi na divai ikahifadhiwa humo. Divai ikichacha hupanua hivyo viriba na kama ni viriba vikuukuu na vimechakaa hupasuka.]

Suala juu ya Sabato

(Mat 12:1-8; Luka 6:1-5)

23Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano. Walipokuwa wanatembea, wanafunzi wake wakaanza kukata masuke ya ngano.

24Mafarisayo wakawaambia, “Tazama! Kwa nini wanafanya jambo ambalo si halali kufanya siku ya Sabato?”[#2:24 Yamkini yahusu katazo la kuvuna siku ya Sabato ilivyo katika Kut 34:21. Kadiri ya ufafanuzi waliotoa Wayahudi kuhusu sheria hiyo wanafunzi walikuwa wamevunja sheria ya Kut 20:8-11.]

25Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa?

26Yeye aliingia ndani ya Nyumba ya Mungu, akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Jambo hili lilifanyika wakati Abiathari alikuwa kuhani mkuu. Na ni makuhani tu peke yao waliokuwa wameruhusiwa kula mikate hiyo. Lakini Daudi aliila, tena akawapa na wenzake.”[#2:26 Kulingana na 1Sam 21:1-6 Ahimeleki (baba yake Abiathari) ndiye aliyekuwa kuhani mkuu (rejea Mat 12:4; Luka 6:4).; #2:26 Law 24:9.]

27Basi, Yesu akawaambia, “Sabato iliwekwa kwa ajili ya binadamu na si binadamu kwa ajili ya Sabato!

28Kwa hiyo, Mwana wa Mtu ana uwezo hata juu ya Sabato.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania