Nahumu 1

Nahumu 1

1Kauli ya Mungu juu ya Ninewi. Kitabu cha maono ya Nahumu wa Elkoshi.[#1:1 Huu ulikuwa mji mkuu wa dola la Ashuru ambalo lilijulikana sana wakati wake kwa utajiri na nguvu zake za kijeshi (taz Yona 1:2 maelezo); rejea Isa 10:5-34; 14:24-27; Sef 2:13-15. Ninewi uliangamizwa mwaka 612 K.K.; #1:1—3:19 Taz Isa 10:5-34; 14:24-27; Sef 2:13-15. Mahali panapoitwa Elkoshi hapajulikani.]

Ghadhabu ya Mungu dhidi ya Ninewi

2Mwenyezi-Mungu ni Mungu mwenye wivu, mlipiza kisasi;[#1:2 Huu ni msemo ambao shabaha yake kila mara katika Biblia ni kusisitiza kwamba Mwenyezi-Mungu, kwa kufanya agano na watu wake, hawezi kuruhusu mshindani awe ni yeyote aitwaye “mungu” (wa uongo) au awe ni binadamu. Hawezi kuruhusu mshindani kwa sababu yeye ndiye Mungu peke yake (Kut 20:5-6; Kumb 4:24).; #1:2 Mungu ni mlipiza kisasi kwa sababu yeye daima hutaka haki itekelezwe miongoni mwa watu na hawezi kuacha kuadhibu ukiukaji wa haki.]

Mwenyezi-Mungu hulipiza kisasi na ni mwenye ghadhabu;

Mwenyezi-Mungu hulipiza kisasi kwa adui zake,

huwaka ghadhabu juu ya adui zake.

3Mwenyezi-Mungu hakasiriki upesi, lakini amejaa nguvu,

Mwenyezi-Mungu kamwe hatawaachilia wenye hatia.

Apitapo Mwenyezi-Mungu, huzuka kimbunga na dhoruba;

mawingu ni vumbi litimuliwalo na nyayo zake.

4Huikaripia bahari na kuikausha,[#1:4 Dokezo kwa tukio la Waisraeli kutoka Misri na kuvuka Bahari ya Shamu. Taz Kut 14:16-25; 15:1-19; Zab 106:9.]

yeye huikausha mito yote.

Mbuga za Bashani na mlima Karmeli hunyauka,

maua ya Lebanoni hudhoofika.

5Milima hutetemeka mbele yake,

navyo vilima huyeyuka;

dunia hutetemeka mbele yake,

ulimwengu na vyote vilivyomo.

6Nani awezaye kuikabili ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu?

Nani awezaye kustahimili ukali wa hasira yake?

Yeye huimwaga hasira yake iwakayo kama moto,

hata miamba huipasua vipandevipande.

7Mwenyezi-Mungu ni mwema,

yeye ni ngome ya usalama wakati wa taabu.

Yeye huwalinda wote wanaokimbilia usalama kwake.

8Adui wakiivamia nchi kama mafuriko, yeye huwaangamiza;

huwafuatia na kuwafukuza mpaka gizani.

9Mbona mnafanya mipango dhidi ya Mwenyezi-Mungu?

Yeye atawakomesha na kuwaangamiza,

wala mpinzani wake hataweza kuinuka tena.

10Watateketezwa kama kichaka cha miiba,

kama vile nyasi zilizokauka.

11Kwako kumetoka aliyepanga maovu dhidi ya Mwenyezi-Mungu

aliyefanya njama za ulaghai.

12Mwenyezi-Mungu awaambia hivi watu wake:

“Ingawa Waashuru ni wengi na wenye nguvu,

wao wataangushwa na kuangamizwa.

Ingawa nimewatesa nyinyi watu wangu,

sitawateseni tena zaidi.

13Sasa nitaivunja nira ya Ashuru shingoni mwenu,

na minyororo waliyowafungia nitaikatakata.”

14Mwenyezi-Mungu ameamuru hivi kuhusu Ninewi:

“Hutapata wazawa kulidumisha jina lako.

Sanamu zako za kuchonga na za kusubu,

nitazivunjavunja nyumbani mwa miungu yako.

Mimi nitakuchimbia kaburi lako,

maana wewe hufai kitu chochote.”

15Enyi watu wa Yuda tazameni:

Anakuja kutoka mlimani mtu anayeleta habari njema,

mjumbe ambaye anatangaza amani.

Adhimisheni sikukuu zenu, enyi watu wa Yuda,

timizeni nadhiri zenu,

maana waovu hawatawavamia tena,

kwani wameangamizwa kabisa.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania