The chat will start when you send the first message.
1Ole wako mji wa mauaji!
Umejaa udanganyifu mtupu na nyara tele,
usiokoma kamwe kuteka nyara.
2Sikia! Mlio wa mjeledi,
mrindimo wa magurudumu,
vishindo vya farasi
na ngurumo za magari!
3Wapandafarasi wanashambulia,
panga na mikuki inametameta;
waliouawa hawana idadi,
maiti wengi sana;
watu wanajikwaa juu ya maiti!
4Ninewi! Wewe umekuwa kama malaya.[#3:4 Katika ujumbe wa manabii kwa Waisraeli matumizi ya neno “malaya” n.k. ni ya kimfano kuashiria au kudokeza hali ya kumwacha Mwenyezi-Mungu na kuabudu miungu mingine. Lakini hapa, Ninewi ni kama mshawishi mkubwa ambaye mwishowe huishia kwa kuwafanya hao walioshawishiwa kuwa watumwa wake.]
Umewashawishi watu, ewe binti wa uchawi,
uliyeyafanya mataifa kuwa watumwa kwa umalaya wako,
na watu wa mataifa kwa uchawi wako.
5Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema nitapambana nawe;
nitalipandisha vazi lako hadi kichwani,
niyaache mataifa yauone uchi wako,
tawala ziikodolee macho aibu yako.
6Nitakutupia uchafu,[#3:6 Neno la Kiebrania lililotafsiriwa hapa kwa “uchafu” linatumika kwa kawaida kutaja vinyago na mifano mingine ya miungu wa uongo. Taz k.m., Yer 4:1; 16:18; 32:34, ambapo neno hilo limetafsiriwa kwa maneno: “vitu vya kuchukiza”, “miungu ya kuchukiza”, n.k.]
na kukutendea kwa dharau,
na kukufanya uwe kioja kwa watu.
7Kisha wote watakaokuona watakukimbia wakisema,
“Ninewi umeangamizwa,
ni nani atakayeuombolezea?
Nani atakayekufariji?”
8Je, wewe Ninewi, ni bora kuliko Thebesi,[#3:8 Mji wa kale wa Misri uliokuwa yapata kilomita 670 kusini mwa Kairo; huo ulivamiwa na Waashuru mnamo mwaka 663 K.K. Taz Yer 46:25 maelezo na rejea Eze 30:14-16.]
mji uliojengwa kando ya mto Nili?
Thebesi ulizungukwa na maji,
bahari ilikuwa boma lake,
maji yalikuwa ukuta wake!
9Kushi ilikuwa nguvu yake;[#3:9 Eneo kusini mwa Misri. Taz Mwa 10:6-10 maelezo.]
nayo Misri pia, tena bila kikomo;
watu wa Puti na Libia waliusaidia!
10Hata hivyo, ulichukuliwa mateka,
watu wake wakapelekwa uhamishoni.
Hata watoto wake walipondwapondwa
katika pembe ya kila barabara;
watu wake mashuhuri walinadiwa,
wakuu wake wote walifungwa minyororo.
11Ninewi, nawe pia utalewa;[#3:11 Dokezo kuhusu kuleweshwa kwa kikombe cha ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.]
utamkimbia adui na kujaribu kujificha.
12Ngome zako zote ni za tini za mwanzo;
zikitikiswa zinamwangukia mlaji kinywani.
13Tazama askari wako:
wao ni waoga kama wanawake.
Milango ya nchi yako ni wazi mbele ya adui zako;
moto umeyateketeza kabisa makomeo yake.
14Tekeni maji muwe tayari kuzingirwa;
imarisheni ngome zenu.
Pondeni udongo kwa kuukanyagakanyaga,
tayarisheni tanuri ya kuchomea matofali!
15Lakini huko pia moto utawateketezeni,
upanga utawakatilia mbali;
utawamaliza kama nzige walavyo.
Ongezekeni kama nzige,
naam, ongezekeni kama panzi!
16Wafanyabiashara wako waliongezeka kuliko nyota;
lakini sasa wametoweka kama panzi warukavyo.
17Wakuu wako ni kama panzi,
maofisa wako kama kundi la nzige;
wakati wa baridi wanakaa kwenye kuta,
lakini jua lichomozapo, huruka,
wala hakuna ajuaye walikokwenda.
18Ewe mfalme wa Ashuru, wachungaji wako wamelala,
waheshimiwa wako wamesinzia.
Watu wako wametawanyika milimani,
wala hakuna yeyote wa kuwakusanya.
19Hakuna wa kuyapa nafuu majeraha yako,
vidonda vyako ni vya kifo.
Wote wanaosikia habari zako wanashangilia.
Maana ni nani aliyeuepa ukatili wako usio na kikomo?