Hesabu 22

Hesabu 22

Balaamu aitwa na mfalme wa Moabu

1Waisraeli walianza safari tena, wakaenda kupiga kambi yao katika tambarare za Moabu, mashariki ya mto Yordani, kuelekea mji wa Yeriko.

2Mfalme Balaki mwana wa Sipori, alijua mambo yote Waisraeli waliyowatendea Waamori.[#22:2 Habari zote juu ya Balaki zimo katika sura hizi za 22-24, lakini anatajwa pia katika Yos 24:9; Amu 11:25 na Mika 6:5.]

3Yeye pamoja na Wamoabu wakashikwa na hofu kubwa juu ya Waisraeli. Waliwaogopa hasa kwa sababu ya wingi wao.

4Basi Wamoabu wakawaambia viongozi wa Midiani, “Umati huu punde si punde utaharibu kila kitu kandokando yetu kama fahali alavyo majani shambani.” Kwa hiyo, Balaki mwana wa Sipori, aliyekuwa mfalme wa Moabu wakati huo,

5akapeleka ujumbe kwa Balaamu, mwana wa Beori, huko Pethori, karibu na mto Eufrate, nchini Amawi. Alimwambia Balaamu hivi: “Kuna taifa ambalo limetoka Misri, nalo limeenea kila mahali nchini, tena linatishia kuchukua ardhi yangu.[#22:5 Katika Biblia Balaamu anajulikana kama mtu anayestahili sifa na pia asiyestahili kusifiwa (taz k.m. Hes 31:8,16; Kumb 23:3-6; Yos 13:22; 24:9-10; 2Pet 2:15-16; Yuda 11). Si yamkini mji Pethori ulikuwa wapi. Wengine wanafikiri ni sawa na mji “Pitru” kaskazini mwa Siria ambako kungekuwa umbali wa kilomita 500; lakini wengine wanadhani mji huo ulikuwa mahali fulani karibu zaidi na matukio haya kama vile katika nchi ya Waamoni.]

6Njoo sasa uwalaani watu hawa kwa ajili yangu maana wana nguvu kuliko mimi. Labda nitaweza kuwashinda na kuwafukuza wasiingie katika nchi yangu, kwa maana najua kuwa wewe ukimbariki mtu hubarikiwa, ukimlaani mtu hulaaniwa.”[#22:6 Yaelekea kazi ya Balaamu ilifahamika kuwa ya unabii mahali pengi. Kwa kufuata makala fulani ya karne ya nane K.K. mtu aitwaye Balaamu anatajwa kuwa “nabii wa miungu” naye alipata ufunuo halafu akawajulisha watu ujumbe aliopewa na miungu, labda ni huyu wa sura 22—24. Ling Mwa 12:3; 27:29; Hes 23:7; Kumb 23:4; Yos 24:9; Neh 13:2.]

7Basi, maofisa wa Moabu na Midiani wakachukua ada ya mwaguzi, wakaondoka kwenda kwa Balaamu. Walipowasili, walimpa Balaamu ujumbe wa Balaki.

8Balaamu akawaambia, “Laleni huku usiku huu, nami nitawajulisheni atakayoniambia Mwenyezi-Mungu.” Basi, wazee hao wa Moabu wakakaa na Balaamu.[#22:7-8 Balaamu anaonekana kwamba alifanya huduma zake kama nabii au mwenye kubashiri wa miungu, na kama kawaida aliweza kupewa pesa kwa ajili hiyo. Kubashiri kulifanyika aghalabu kwa kuchunguza viungo vya ndani vya mnyama wa tambiko. Balaamu hakuwa Mwisraeli na kwa sababu hiyo ni jambo la kushangaza anapowaambia hao waliokuja kwake kwamba atangojea ajue Mwenyezi-Mungu atakayomwambia (22:18).]

9Kisha Mungu alimjia Balaamu, akamwuliza, “Ni nani hawa wanaokaa nawe?”

10Balaamu akamjibu Mungu, “Balaki mwana wa Sipori amenipelekea ujumbe kwamba

11kuna watu wa taifa fulani waliotoka Misri, nao wameenea kila mahali nchini. Ameniomba niende kuwalaani watu hao ili pengine afaulu kupigana nao na kuwafukuza.”

12Mungu akamwambia Balaamu, “Usiende pamoja na watu hawa, wala usiwalaani watu hao maana wamebarikiwa.”[#22:12-13 Yamkini hapa katika ndoto (taz aya 8-9,19-20).]

13Basi, asubuhi yake Balaamu aliamka, akawaambia maofisa wa Balaki, “Rudini nchini mwenu, kwa maana Mwenyezi-Mungu hapendi kuniruhusu kwenda pamoja nanyi.”

14Kwa hiyo maofisa wa Moabu wakaondoka, wakarudi kwa Balaki, wakamwambia, “Balaamu amekataa kuja pamoja nasi.”

15Kisha, Balaki akatuma maofisa wengine, wengi zaidi na wa vyeo vya juu kuliko wale wa kwanza.

16Hao walifika kwa Balaamu, wakamwambia, “Balaki mwana wa Sipori asema hivi: ‘Usikubali kuzuiwa na chochote hata uache kuja kwangu.

17Nitakutunukia heshima kubwa, na chochote utakachoniomba nitakutimizia. Njoo uwalaani watu hawa.’”

18Lakini Balaamu akawajibu watumishi wa Balaki, “Hata kama Balaki atanipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, mimi sitaweza kuvunja amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kuhusu jambo lolote, dogo au kubwa.

19Lakini tafadhalini laleni hapa usiku huu kama wale wenzenu, nami nipate kujua atakachoniambia Mwenyezi-Mungu tena.”

20Basi, Mungu akamjia Balaamu usiku huo, akamwambia, “Kama watu hawa wamekuja kukuita, nenda pamoja nao, lakini fanya tu kile nitakachokuambia.”

21Balaamu akaamka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na hao maofisa.

Balaamu, punda na malaika

22Hasira ya Mungu iliwaka kwa sababu Balaamu alikuwa anakwenda; hivyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akakabiliana naye njiani. Wakati huo Balaamu alikuwa amepanda punda wake akiwa na watumishi wake.[#22:22 Kwamba Mungu anakasirika hapa si rahisi kuelewa kwa vile Mungu alikwisha mruhusu kuandamana na hao watu (22:20). Neno “malaika” Kiebrania ni sawa na neno “mjumbe” katika Kiswahili. Katika Biblia “malaika” hufanya kazi kama wajumbe au watumishi wa Mungu. Taz pia Mwa 16:7 maelezo.]

23Basi, punda alimwona malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu amesimama njiani, ameshika upanga uliochomolewa alani mwake. Kwa hiyo aliiacha njia, akaenda pembeni. Balaamu akampiga huyo punda, akamrudisha njiani.

24Kisha malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu akatangulia mbele, akasimama mahali penye njia nyembamba, kati ya mashamba ya mizabibu na kuta pande zote mbili.[#22:24 Mara nyingi mashamba ya mizabibu hasa yale yaliyokuwa kandokando ya barabara yalizungushiwa kuta za mawe ili kuyalinda yasiharibiwe na wanyama na wezi wa zabibu. Mahali hapo palikuwa pembamba mno kwa punda kupita pembeni (aya 26).]

25Punda alipomwona malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu, akajisukumiza ukutani na kuubana mguu wa Balaamu hapo. Kwa hiyo Balaamu akampiga tena huyo punda.

26Kisha malaika akatangulia tena, akasimama mahali pembamba pasipo na nafasi ya kupita kulia wala kushoto.

27Punda alipomwona huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu, akalala chini. Balaamu akawaka hasira, akampiga kwa fimbo yake.

28Hapo Mwenyezi-Mungu akakifunua kinywa cha huyo punda, akamwambia Balaamu, “Nimekutendea nini hata ukanipiga mara hizi tatu?”[#22:28 Jambo la punda kuongea kama mtu ni mojawapo ya vitu vya pekee vinavyoandamana na simulizi hili kusisitiza uwezo wa Mungu katika kuwafanikisha watu wake (taz k.m. punda anamwona malaika lakini Balaamu nabii anawezeshwa tu kumwona baadaye aya 26 na 31).]

29Balaamu akamwambia punda, “Wewe umenidhihaki! Kama ningekuwa na upanga ningalikuulia mbali sasa hivi!”

30Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si yuleyule punda wako aliyekubeba maisha yako yote hadi siku hii ya leo? Je, nimewahi kukutendea namna hii?” Balaamu akajibu, “La.”

31Hapo, Mwenyezi-Mungu akayafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika wa Mwenyezi-Mungu amesimama njiani, ameshika upanga uliochomolewa alani mwake. Balaamu akajitupa chini kifudifudi.

32Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Mbona umempiga punda wako mara hizi tatu? Nimekuja kukuzuia, kwa sababu njia yako ni mbaya.[#22:32 Maneno haya si dhahiri katika Kiebrania. Tafsiri nyingine yamkini: “mwenendo wako unanichukiza”.]

33Punda wako ameniona akaniepa mara hizi tatu. Kama asingaligeuka mbali nami hakika ningalikuua wewe na kumwacha hai punda huyu.”

34Balaamu akamwambia malaika wa Mwenyezi-Mungu “Nimetenda dhambi maana sikujua kwamba umesimama njiani kunizuia. Sasa, kama haikupendezi niendelee na safari hii, basi nitarudi nyumbani.”

35Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Nenda na watu hawa, lakini utasema tu kile nitakachokuambia.” Basi, Balaamu akaendelea na safari pamoja na viongozi wa Balaki.

36Balaki alipopata habari kwamba Balaamu anakuja, alitoka kwenda kumlaki mjini Ari, mji uliokuwa ukingoni mwa mto Arnoni kwenye mpaka wa Moabu.

37Balaki akamwambia Balaamu, “Kwa nini hukuja kwangu mara moja nilipokuita? Je, ulifikiri sitaweza kukutunukia heshima ya kutosha?”

38Balaamu akamjibu Balaki, “Sasa nimekuja! Lakini, je, nina mamlaka ya kusema chochote tu? Jambo atakaloniambia Mungu ndilo ninalopaswa kusema.”

39Basi, Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika mjini Kiriath-husothi.

40Huko Balaki alitoa kafara ya ng'ombe na kondoo, akawagawia nyama Balaamu na maofisa waliokuwa pamoja naye.[#22:40 Au: “tambiko”. Si dhahiri kama Balaki alimtambikia mungu wake au vipi. Yawezekana kuwa Balaki alitoa ng'ombe na kondoo kuwa kafara kwa Mwenyezi-Mungu kufuatana na ushauri wa Balaamu (taz 23:2-3,14).]

Balaamu anawabariki Waisraeli

41Kesho yake, Balaki alimchukua Balaamu, akapanda naye mpaka Bamoth-baali; kutoka huko, Balaamu aliweza kuwaona baadhi ya Waisraeli.[#22:41 Maana yake: “Mahali pa juu pa Baali” na huenda ilihusu vilima ambavyo vilitumiwa kumwabudu mungu Baali. Katika aya hii jambo la kuwaona kwa macho wale ambao walikuwa walaaniwe lilikuwa lazima kwa laana hiyo kuwapata.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania