Zaburi 23

Zaburi 23

Mungu mchungaji wangu

1Mwenyezi-Mungu ni mchungaji wangu,[#23:1 Picha ya Mungu kama mchungaji ni picha inayotokana na picha nyingine katika mazingira ya Waisraeli kwamba Mungu ni mfalme, na kama mfalme mojawapo ya majukumu yake makuu ni yale ya kuwahifadhi, kuwalinda na kuwalisha watu wake (Eze 34:1-23). Katika A.J. Yesu alijionesha dhahiri kabisa kuwa ni mchungaji wa watu wake (Yoh 10:11,14).]

sitapungukiwa na kitu.

2Hunipumzisha kwenye malisho mabichi;

huniongoza kando ya maji matulivu,

3na kuirudishia nafsi yangu nguvu mpya.

Huniongoza katika njia sawa

kwa hisani yake.

4Nijapopita katika bonde la giza kuu la kifo,

sitaogopa hatari yoyote,

maana wewe ee Mwenyezi-Mungu u pamoja nami;

gongo lako na fimbo yako vyanilinda.

5Umeniandalia karamu mbele ya maadui zangu;

umenipaka mafuta kichwani pangu;

kikombe changu umekijaza mpaka kufurika.

6Kweli wema wako na fadhili zako zitakuwa pamoja nami,

siku zote za maisha yangu;

nami nitakaa nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu milele.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania