The chat will start when you send the first message.
1Jinsi gani yanavyopendeza makao yako,[#84:1 Taz pia Zab 42 na 43 kuhusu namna hii ya kusema. Na kuhusu jina la sifa “Mwenyezi-Mungu wa Majeshi” taz Zab 46:7 maelezo.]
ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi!
2Nafsi yangu yatamani mno maskani ya Mwenyezi-Mungu!
Moyo na mwili wangu wote wamshangilia Mungu aliye hai.
3Hata shomoro wamepata makao yao,[#84:3 Mwanazaburi huyu anaona wivu juu ya ndege ambao wanaruka bila kuzuiwa katika hekalu.]
mbayuwayu wamejenga viota vyao,
humo wameweka makinda yao,
katika madhabahu zako, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu!
4Heri wale wanaokaa nyumbani mwako,[#84:4 Hao au ni maofisa wa hekalu kama vile Walawi au ni njia ya kusema juu ya watu ambao huzoea kuabudu hekaluni.]
wakiimba daima sifa zako.
5Heri watu wanaopata nguvu zao kwako,
wanaotamani kwenda kuhiji mlimani kwako.
6Wapitapo katika bonde kavu la Baka,[#84:6 Mahali penyewe hapajulikani.]
hulifanya kuwa mahali pa chemchemi,
na mvua za vuli hulijaza madimbwi.
7Wanaendelea kupata nguvu zaidi na zaidi;
watamwona Mungu wa miungu huko Siyoni.
8Usikie sala yangu ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi;
unitegee sikio, ee Mungu wa Yakobo.
9Ee Mungu, umwangalie kwa wema ngao yetu mfalme,[#84:9 Jina hili ngao (likiwa na maana ya mlinzi) pamoja na “huyo uliyemweka wakfu” (taz 2:2 maelezo) yote yanamtaja mfalme wa Waisraeli.]
umtazame huyo uliyemweka wakfu kwa mafuta.
10Siku moja tu katika maskani yako,
ni bora kuliko siku elfu mahali pengine;
afadhali kusimama mlangoni pa nyumba yako,
kuliko kuishi nyumbani kwa watu waovu.
11Mwenyezi-Mungu ni jua letu na ngao yetu;
yeye hutuneemesha na kutujalia fahari.
Hawanyimi chochote kilicho chema,
wale waishio kwa unyofu.
12Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
heri mtu yule anayekutumainia wewe!