Zaburi 98

Zaburi 98

Mungu mtawala wa dunia yote

1Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya,

kwa maana ametenda mambo ya ajabu!

Mkono wake hodari, mkono wake mtakatifu umempatia ushindi.

2Mwenyezi-Mungu ameonesha ushindi wake;

ameyadhihirishia mataifa uwezo wake wa kuokoa.

3Amekumbuka fadhili na uaminifu wake kwa Waisraeli.

Pande zote za dunia zimeuona ushindi wa Mungu wetu.

4Dunia yote imshangilie Mwenyezi-Mungu;

imsifu kwa nyimbo na vigelegele.

5Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa shangwe,

msifuni kwa sauti tamu za zeze.

6Mpigieni vigelegele Mwenyezi-Mungu mfalme wetu,

mshangilieni kwa tarumbeta na sauti ya baragumu.

7Bahari na ivume na vyote vilivyomo;

dunia na wote waishio ndani yake.

8Enyi mito pigeni makofi;

enyi vilima imbeni pamoja kwa shangwe.

9Shangilieni mbele ya Mwenyezi-Mungu,[#98:7-8 Rejea 96:11-12 maelezo.]

maana anakuja kutawala dunia.

Atauhukumu ulimwengu kwa haki,

atawatawala watu kwa uadilifu.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania