Waroma 5

Waroma 5

Waadilifu mbele yake Mungu

1Sasa, kwa vile tumefanywa kuwa waadilifu kwa imani, basi tunayo amani naye Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.[#5:1 Hati nyingine za kale zina “na tuishi kwa amani”.]

2Kwa imani yetu, yeye ametuleta katika hali hii ya neema ya Mungu ambamo sasa tunaishi. Basi, tunajivunia tumaini tulilo nalo la kushiriki utukufu wa Mungu.[#5:2 Neno “neema” ya Mungu ni fadhili au wema anaowajalia watu bila wao kustahili. Na neno ambalo limetafsiriwa hapa kwa neno “tunajivunia” ni neno analotumia Paulo mara nyingi. Kwa neno hilo mtu anaweza kufikiria “majivuno ya kibinadamu” au hata kuwa na hali ya kujitosheleza kutokana na mastahili ya mtu mwenyewe (Rom 4:2), jambo ambalo halimo kwa mtu yule anayemwamini Kristo. Paulo analitumia kuelezea “furaha” ambayo inategemea au ina msingi wake, si katika uwezo au nguvu za mtu, bali katika nguvu ya Mungu mwenyewe (rejea 2Kor 10:17; Fil 3:3).]

3Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi,

4nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini.

5Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha mimina mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia.[#5:5 Kitenzi hicho cha “kumimina” kinatumiwa mara kwa mara kuhusu Roho Mtakatifu (Mate 2:17). Paulo aliamini kwamba Roho Mtakatifu alikuwa katika maisha ya wafuasi wa Yesu Kristo akiwasaidia kuishi hayo maisha mapya yaliyo na msingi wake katika imani (8:12-17; 1Kor 2:1-11).]

6Tulipokuwa bado wanyonge, Kristo, wakati ulipotimia, alikufa kwa ajili yetu sisi waovu.[#5:6-11 Taz 3:25-26 maelezo; 1Pet 3:18; rejea pia 1Kor 15:3; 2Kor 5:14-15; Gal 1:4.]

7Si rahisi mtu kufa kwa ajili ya mtu mwadilifu; labda mtu anaweza kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema.

8Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

9Kwa kuwa sasa tumefanywa kuwa waadilifu kwa damu ya Kristo, ni dhahiri zaidi kwamba atatuokoa katika ghadhabu ya Mungu.[#5:9 Maneno haya ni namna moja ya kutaja kifo cha Yesu Kristo kilichowakomboa watu. Na maneno “atatuokoa” (kitenzi - wakati ujao), bila shaka yanahusu siku ile ya hukumu ya mwisho.]

10Maana, tulipokuwa bado maadui zake, Mungu alitupatanisha naye kwa kifo cha Mwanae. Na kwa vile sasa tumepatanishwa naye, ni dhahiri zaidi kwamba tutaokolewa kwa uhai wa Kristo.[#5:10 Paulo kamwe hasemi “Mungu alipatanishwa nasi” ila “yeye anatupatanisha naye” (2Kor 5:18-20).]

11Wala si hayo tu, ila tunafurahi pia katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ametupatanisha na Mungu.

Adamu na Kristo

12Kwa njia ya mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, nayo ikasababisha kifo. Hivyo kifo kimeenea katika jumuiya yote ya binadamu, kwa maana wote wametenda dhambi.[#5:12 Mwa 2:15-17; 3:6-19; Hek 2:24; rejea 1Kor 15:22,45-49. Paulo anataka kusema kwamba kuna mshikamano wa namna fulani au umoja kati ya binadamu wote na Adamu, lakini anasema pia juu ya kuwajibika kwa kila mmoja binafsi: wote wametenda dhambi.]

13Kabla ya sheria kuwako, dhambi ilikuwako ulimwenguni; lakini dhambi haiwekwi katika kumbukumbu bila sheria.[#5:13 Taz 4:15 maelezo.]

14Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Mose, kifo kiliwatawala hata wale ambao hawakutenda dhambi kama ile ya Adamu, ya kumwasi Mungu.

Adamu alikuwa kielelezo cha Kristo ambaye alikuja baadaye.

15Lakini kosa la Adamu haliwezi kulinganishwa na neema ya Mungu. Maana, ingawa dhambi ya mtu mmoja ilisababisha kifo kwa wote, kwa fadhili ya mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, Mungu amewazidishia wote neema na zawadi zake.[#5:15 Uhusiano mmoja tu uliopo kati ya uasi au kosa la Adamu na neema ambayo Mungu alitupatia, kama inavyoelezwa katika 5:16-19, ni kwamba kwa kitendo cha mtu mmoja tu binadamu wote waliguswa: Adamu alileta dhambi, hukumu na kifo; Yesu Kristo alileta uadilifu, wokovu na uhai.]

16Kuna tofauti baina ya zawadi ya Mungu na dhambi ya mtu yule mmoja. Maana, baada ya kosa la mtu mmoja, Mungu alitoa hukumu; lakini baada ya makosa ya watu wengi, Mungu aliwapa zawadi yake kwa kuwasamehe.

17Kweli, kwa dhambi ya mtu mmoja, kifo kilianza kutawala kwa sababu ya huyo mtu mmoja; lakini, ni dhahiri zaidi kwamba alichokifanya yule mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, ni bora zaidi. Wote wanaopokea neema na zawadi hiyo ya kufanywa kuwa waadilifu, watatawala katika uhai kwa njia ya huyo mmoja, yaani Yesu Kristo.

18Basi, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta hukumu kwa binadamu wote, kadhalika kitendo kiadilifu cha mtu mmoja kinawapa wote uadilifu na uhai.

19Na kama kwa kutokutii kwa mtu mmoja watu wengi walifanywa wenye dhambi, kadhalika kutii kwa mtu mmoja kutawafanya wengi kuwa waadilifu.

20Sheria ilitokea, ikasababisha kuongezeka kwa uhalifu; lakini pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi.[#5:20 Sheria ya Mose ilikuja muda mrefu sana baada ya dhambi ambayo Adamu aliileta duniani. Tunaambiwa pia hapa kwamba sheria hiyo ilifanya uhalifu kuongezeka 3:20; 4:15; 5:13; Gal 3:19. Mungu hakuwapa Waisraeli ile sheria ili awafanue Wayahudi kuwa waadilifu mbali na watu wa mataifa mengine wenye dhambi, alitaka Waisraeli wafahamu zaidi kwamba kuhusu dhambi wao ni kama watu wote wengine.]

21Kama vile dhambi ilivyotawala kwa kifo, kadhalika neema inatawala kwa uadilifu na kuleta uhai wa milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.[#5:21 Paulo anasema juu ya dhambi hapa kana kwamba ingekuwa nafsi au mtu (taz pia 6:23) na katika sura ya 6 na 7 kama bwana ambaye anawafanya watumwa wote anaowatawala. Hali kadhalika anasema juu ya neema ya Mungu kana kwamba ingekuwa pia nafsi au mtu.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania