Sira 36

Sira 36

Sala kwa ajili ya Israeli

1Utuhurumie ee Bwana Mungu wa wote.

2Yafanye mataifa yote yakuogope.

3Inua mkono wako dhidi ya mataifa mengine,

uyafanye yauone uwezo wako mkuu.

4Kama ulivyotutumia kuyaonesha jinsi ulivyo mtakatifu,

vivyo hivyo yatumie kutuonesha utukufu wako.

5Nayo yatajua kama tunavyojua na sisi,

kwamba hakuna Mungu ila wewe, ee Bwana.

6Fanya tena ishara na kufanya miujiza zaidi,

7ufanye mkono wako uwe na utukufu zaidi.

8Onesha hasira yako na kumwaga ghadhabu yako;

9waangamize wapinzani na kuwafuta maadui.

10Iharakishe ile siku na kukumbuka kiapo chako;

wafanye watu wasimulie matendo yako makuu.

11Yeyote atakayeponyoka ateketezwe na ghadhabu yako kali,

na wale wanaowadhuru watu wako wapate maangamizi.

12Uwaponde wakuu wa maadui zako,

ambao husema: “Hakuna mwingine ila sisi wenyewe!”

13Yakusanye pamoja makabila yote ya Yakobo,[#36:13 Kutokana na vurugu katika tafsiri ya Kigiriki ya kitabu hiki aya 14 na 15 hazitumiwi katika sura hii ya 36. Lakini hakuna maneno yaliyokosekana.]

16uwape mali yako kama ulivyopanga mwanzoni.

17Wahurumie ee Bwana watu wanaoitwa kwa jina lako;

Waisraeli uliowaita mzaliwa wako wa kwanza wa kiume.

18Uuonee huruma mji wa hekalu lako,

Yerusalemu, mji wa pumziko lako.

19Uujaze mji wa Siyoni shangwe za matendo yako ya ajabu,

na hekalu lako lijae utukufu wako.

20Uwahakiki watu wako uliowaumba mwanzoni,

na kutimiza unabii uliosemwa kwa jina lako.

21Uwatuze wale wanaokungojea,

na manabii wako waonekane kuwa ni wa kuaminika.

22Usikilize, ee Bwana, sala ya watumishi wako,

kulingana na baraka za Aroni juu ya watu wako.

Hivyo binadamu wote duniani watajua

kuwa wewe ndiwe Bwana, Mungu wa nyakati zote.

Kuchagua mke

23Chakula chochote chaweza kuliwa,

lakini chakula kingine ni bora kuliko kingine.

24Kama ulimi upimavyo mionjo ya aina ya vyakula,

ndivyo na mwenye akili agunduavyo maneno ya uongo.

25Mwenye akili potovu atasababisha huzuni,

lakini mwenye uzoefu wa maisha atamlipa inavyofaa.

26Mwanamke aweza kuolewa na yeyote,

lakini msichana mmoja ni bora kuliko mwingine.

27Uzuri wa mwanamke hufurahisha uso,

na hushinda kila kitu anachotamani mwanamume.

28Kama mwanamke ni mwema na mwenye adabu anapoongea,

mumewe ana bahati kuliko wengine wote.

29Mwanamume akipata mke amepata ubora mkubwa mno,

amejipatia msaidizi bora na nguzo ya msaada.

30Mali isiyolindwa kwa ukuta itaporwa;

ni pasipo mke, mwanamume atatangatanga na kusononeka.

31Nani atakayemwamini jambazi azururaye mji hata mji?

Hivyo hakuna atakayemwamini mwanamume asiye na kwake,

ambaye ana malazi popote usiku unapomkuta.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania