The chat will start when you send the first message.
1Laiti ungekuwa kaka yangu,[#8:1 Aya hii inaficha maana mbili: kwanza kusema laiti huyo mpenzi mwanamume angekuwa kaka yake, huyo mwanamke anaonesha hali yake ya kushindwa kukaa karibu naye; pili, katika tamaduni za kale kuonesha ishara za mapenzi kama vile kubusiana hadharani halikuwa jambo lililokubalika hapo kale. Ndivyo pia katika tamaduni za asili katika nchi nyingi za Afrika kwa mfano. Dada angaweza kumbusu kaka yake hadharani, lakini haikufanyika kati ya watu wasio na ujamaa wa karibu sana.]
ambaye amenyonyeshwa na mama yangu!
Hivyo, hata kama ningekutana nawe nje,
ningekubusu na hakuna ambaye angenidharau.
2Ningekuongoza na kukufikisha nyumbani kwa mama mzazi,[#8:2 Kitendo ambacho kingekuwa sawa na kuhalalisha uhusiano wao hadharani. Makomamanga ni matunda ambayo utomvu wake uliweza kutengeneza kinywaji kama cha divai tamu.]
mahali ambapo ungenifundisha upendo.
Ningekupa divai nzuri iliyokolezwa,
ningekupa divai yangu ya makomamanga yangu.
3Mkono wako wa kushoto u chini ya kichwa changu,
na mkono wako wa kulia wanikumbatia.
4Nawasihini, enyi wanawake wa Yerusalemu,
msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi,
hadi hapo wakati wake utakapofika.
5Ni nani huyu ajaye kutoka mbugani,
huku anamwegemea mpenzi wake?
Chini ya mtofaa, mimi nilikuamsha,
pale ambapo mama yako aliona uchungu,
naam, pale ambapo mama yako alikuzaa.
6Nipige kama mhuri moyoni mwako,
naam, kama mhuri mikononi mwako.
Maana pendo lina nguvu kama kifo,
wivu nao ni mkatili kama kaburi.
Mlipuko wake ni kama mlipuko wa moto,
huwaka kama mwali wa moto.
7Maji mengi hayawezi kamwe kulizima,
mafuriko hayawezi kulizamisha.
Mtu akijaribu kununua pendo,
akalitolea mali yake yote,
atakachopata ni dharau tupu.
8Tunaye dada mdogo,
ambaye bado hajaota matiti.
Je, tumfanyie nini dada yetu
siku atakapoposwa?
9Kama angalikuwa ukuta,
tungalimjengea mnara wa fedha;
na kama angalikuwa mlango,
tungalimhifadhi kwa mbao za mierezi.
10Mimi nalikuwa ukuta,[#8:10 Maneno haya yanaonekana kupinga walichosema kaka zake katika aya zilizotangulia, au huenda sasa anatamka kama mtu mzima aliye tayari kuolewa.]
na matiti yangu kama minara yake.
Machoni pake nalikuwa
kama mwenye kuleta amani.
11Solomoni alikuwa ana shamba la mizabibu,
mahali paitwapo Baal-hamoni.
Alilikodisha kwa walinzi;
kila mmoja wao alilipa vipande elfu vya fedha.
12Shamba langu la mizabibu ni shamba langu mwenyewe,[#8:12 Huenda kuna ulinganifu kinyume na aya iliyotangulia: Ingawa Solomoni alikuwa na shamba lake la mizabibu akalikodisha kwa watu wengi, hapa shamba la mzabibu (huyo mwanamke mwenyewe) ni la huyo mwanamume mhusika katika wimbo huu na kamwe hawezi kulikodisha kwa wengine.]
naam, ni shamba langu binafsi!
Basi, Solomoni, wewe ukae na elfu zako za fedha,
na kila mlinzi wa matunda akae na mia mbili zake.
13Ewe uliye shambani,
rafiki zangu wanasikiliza sauti yako;
hebu nami niisikie tafadhali!
14Njoo haraka ewe mpenzi wangu,
kama paa au mwanapaa dume juu ya milima ya manukato.