Tito 2

Tito 2

Mafundisho ya kweli

1Lakini wewe unapaswa kuhubiri mafundisho sahihi.

2Waambie wanaume wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu.[#2:2 Hapa maneno “wanaume wazee” yanatumika kwa maana ya wazee wa umri, hali kadhalika pia kama maneno “wanawake wazee” katika aya ya 3, yanavyotumika kwa maana hiyohiyo. Kwa hiyo hapa haihusu wadhifa katika Kanisa. Ni umri gani ulifikiriwa kuwa ndio umri wa mwanzo wa mzee hatuna habari yoyote. Wengine wanafikiri kuanzia umri wa mwaka wa sitini; yawezekana kwamba wale viongozi wa Kanisa waliteuliwa kutoka kundi hilo na ndio maana sifa zinazotajwa hapa ni sawa kwa jumla na zile zinazotajwa kuhusu wale viongozi wanaotajwa katika sura 1.]

3Hali kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe wachongezi au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema,[#2:3 Yaani, wanapaswa kutoa mfano mwema au mashauri mema.]

4ili wawazoezeshe kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto,

5wawe na kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa.[#2:5 Taz Efe 5:23-24 maelezo na rejea 1Kor 14:34; Kol 3:18; 1Tim 2:11-12; 1Pet 3:1.]

6Kadhalika, wahimize vijana wawe na kiasi.

7Katika mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe na uzito katika mafundisho yako.[#2:7 1Tim 4:12; 1Pet 5:2-3.; #2:7 Taz 1Tim 1:10.]

8Maneno yako yasiwe na hitilafu yoyote ili maadui zako waaibike wasipopata chochote kibaya cha kusema juu yetu.

9Watumwa wanapaswa kuwatii wakuu wao na kuwapendeza katika mambo yote. Wasibishane nao,[#2:9-10 Kuhusu utumwa katika A.J. rejea Kol 3:22 maelezo.]

10au kuiba vitu vyao. Badala yake wanapaswa kuonesha kwamba wao ni wema na waaminifu daima, ili, kwa matendo yao yote, wayapatie sifa njema mafundisho juu ya Mungu, Mwokozi wetu.

11Maana neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote.[#2:11-14 Hapa, maneno ambayo yanaweza kuchukuliwa kama ni kanuni au fomula ya Kikristo yanatumiwa kutoa muhtasari wa mafundisho ya Kikristo (taz pia Tito 3:3-7 maelezo).]

12Neema hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi maisha adili na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa,

13tukiwa tunangojea siku ile ya heri tunayoitumainia, wakati utakapotokea utukufu wa Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo.[#2:13 Rejea 1Kor 1:7; Fil 3:20.; #2:13 Baadhi ya hati za kale zina: “Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo” (rejea 2Pet 1:1).]

14Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda mema.[#2:14 1Tim 2:6; rejea Mat 20:28; Marko 10:45; Gal 1:4; 2:20.; #2:14 Kut 19:5; Kumb 4:20; 7:6; 14:2; Eze 37:23; 1Pet 2:9.]

15Basi, sema mambo hayo na tumia mamlaka yako yote ukiwahimiza na kuwaonya wasikilizaji wako. Mtu yeyote na asikudharau.[#2:15 1Tim 4:12.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania