Hekima ya Solomoni 2

Hekima ya Solomoni 2

1Katika upotovu wao huambiana:

“Maisha yetu ni mafupi na yenye taabu.

Kifo kinapowasili hakuna dawa ya kuepukana nacho.

Hakuna mtu aliyewahi kumtoa mwingine ahera.

2Sisi tulizaliwa kwa bahati tu,

tukisha kufa itakuwa kana kwamba hatukupata kuwapo.

Pumzi yetu ni kama moshi tu unaotoweka;

akili zetu ni ndogo tu zinazowashwa kwa mapigo ya mioyo yetu.

3Cheche hiyo ikizimika, mwili wetu utageuka majivu,

na roho yetu itatoweka kama vile hewa.

4Jina letu litasahaulika punde si punde,

mambo tuliyotenda hayatakumbukwa;

maisha yetu yatatoweka kama nyayo za mawingu;

yatatawanywa kama ukungu unaofukuzwa na nuru ya jua,

unaoshindwa kustahimili joto la jua.

5Siku zetu ni kama kivuli kipitacho.

na tukisha kufa hatuwezi kurudi kutoka humo.

Siku ya kufa imepangwa wala hakuna atakayeweza kuirudisha.

6Hivyo na tujifurahishe kwa chochote kizuri kilichopo;

tuvitumie kabisa viumbe kama wakati wa ujana.

7Tujishibishe divai ya thamani na marashi,

tujichumie maua ya vuli yasitupite.

8Tujivike taji za waridi kabla hayajanyauka.

9Kila mmoja wetu ashiriki tamasha zetu,

tuache alama za anasa zetu zionekane kila mahali.

Maana ndivyo maisha yalivyo! Ndiyo tuliyopangiwa.

10“Maskini, hata akiwa mwema, tutamkandamiza;

naye mjane hatutamhurumia

wala kumjali mzee mwenye mvi.

11Nguvu zetu ndizo mwongozo wa haki,

mnyonge hana faida yeyote!

12Tena, tumvizie mtu mwema;

mtu huyo ni usumbufu kwetu na hutupinga.

Hutukaripia kila tunapovunja sheria;

hutushtaki kila tunapokiuka mwongozo.

13Mtu mwema hujitakia kumjua Mungu

na kujiita mtoto wake Bwana.

14Mtu wa namna hiyo amekuwa kwetu karipio la fikira zetu.

15Hata tu kumtazama ni mzigo kwetu;

maana anaishi tofauti na watu wengine

njia zake ni ngeni kabisa.

16Anatuona sisi kuwa kama madini hafifu;

huziepa njia zetu kama kukwepa uchafu.

Huuthamini kuwa heri mwisho wa mwadilifu,

na hujigamba kwamba Mungu ni Baba yake.

17Haya, na tuone kama maneno yake ni ya kweli!

Tuone yatakayompata wakati atakapokufa.

18Kama kweli yeye ni mwana wa Mungu, Mungu atamsaidia,

na kumkomboa makuchani mwa maadui zake.

19Haya! Tumtendee kikatili na kumtesa,

tuone alivyo mpole,

tuujaribu uvumilivu wake.

20Tutamhukumu kifo cha aibu

maana, kama alivyosema, Mungu atamwokoa!”

Mambo ya nje hudanganya

21Ndivyo wafikiriavyo waovu,

lakini wanajidanganya wenyewe.

Uovu wao umewapofusha.

22Hawajui mipango ya siri ya Mungu;

hawajawahi kutumaini kupata thawabu ya kuishi vema,

wala kulitambua tuzo la watu waishio bila hatia.

23Mungu aliumba watu waishi maisha ya milele

aliwafanya kwa mfano wa hali yake mwenyewe.

24Lakini kwa wivu wa Shetani kifo kiliingia duniani,

na wote walio upande wake hukipata.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania