1 Wafalme 13

1 Wafalme 13

Mtu wa Mungu kutoka Yuda

1Kwa neno la Bwana , mtu wa Mungu alifika Betheli kutoka Yuda wakati Yeroboamu alipokuwa amesimama kando ya madhabahu ili kutoa sadaka.

2Akapiga kelele dhidi ya madhabahu kwa neno la Bwana : “Ee madhabahu, ee madhabahu! Hivi ndivyo asemavyo Bwana : ‘Mwana aitwaye Yosia atazaliwa katika nyumba ya Daudi. Juu yako atawatoa dhabihu makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia ambao hutoa sadaka hapa, nayo mifupa ya wanadamu itateketezwa juu yako.’ ”

3Siku hiyo hiyo, mtu wa Mungu akatoa ishara: “Hii ndiyo ishara Bwana aliyotangaza: Madhabahu haya yatapasuka na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.”

4Mfalme Yeroboamu aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, alipopiga kelele dhidi ya madhabahu huko Betheli, akanyoosha mkono wake kutoka madhabahuni na kusema, “Mkamateni!” Lakini mkono aliounyoosha kumwelekea yule mtu ukakauka kiasi kwamba hakuweza kuurudisha.

5Pia, madhabahu yakapasuka na majivu yakamwagika, sawasawa na ishara iliyotolewa na mtu wa Mungu kwa neno la Bwana .

6Kisha mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Niombee kwa Bwana Mungu wako ili mkono wangu upate kupona.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwombea kwa Bwana , nao mkono wa mfalme ukapona na kurudi ulivyokuwa hapo awali.

7Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu, “Twende nyumbani mwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.”

8Lakini yule mtu wa Mungu akamjibu mfalme, “Hata kama ungenipa nusu ya mali yako, nisingeenda pamoja nawe, wala nisingekula mkate au kunywa maji hapa.

9Kwa kuwa niliagizwa kwa neno la Bwana : ‘Kamwe usile mkate wala usinywe maji au kurudi kwa njia uliyojia.’ ”

10Hivyo, akafuata njia nyingine na hakurudi kupitia njia aliyokuwa ameijia Betheli.

11Basi kulikuwa na nabii fulani mzee aliyekuwa anaishi Betheli, ambaye wanawe walikuja kumwambia yote ambayo mtu wa Mungu alikuwa ameyafanya pale siku ile. Pia wakamwambia baba yao yale aliyomwambia mfalme.

12Baba yao akawauliza, “Ameelekea njia gani?” Nao wanawe wakamwonesha ile njia yule mtu wa Mungu kutoka Yuda aliyopita.

13Hivyo akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda.” Walipokwisha kumtandikia punda, akampanda

14na kumfuatilia yule mtu wa Mungu. Akamkuta ameketi chini ya mwaloni na kumuuliza, “Je, wewe ndiwe mtu wa Mungu kutoka Yuda?”

Akamjibu, “Mimi ndiye.”

15Basi nabii akamwambia, “Karibu nyumbani pamoja na mimi, ule.”

16Yule mtu wa Mungu akasema, “Siwezi kurudi na kwenda nawe, wala siwezi kula mkate au kunywa maji pamoja nawe mahali hapa.

17Nimeambiwa kwa neno la Bwana : ‘Kamwe usile mkate au kunywa maji huko au kurudia njia uliyojia.’ ”

18Yule nabii mzee akajibu, “Mimi pia ni nabii, kama wewe. Naye malaika alisema nami kwa neno la Bwana : ‘Mrudishe aje katika nyumba yako ili apate kula mkate na kunywa maji.’ ” (Lakini alikuwa akimwambia uongo.)

19Hivyo mtu wa Mungu akarudi pamoja naye na akala na kunywa katika nyumba yake.

20Walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia yule nabii mzee aliyemrudisha huyo mtu wa Mungu.

21Akampazia sauti yule mtu wa Mungu aliyekuwa ametoka Yuda, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana : ‘Umeasi neno la Bwana na hukushika amri uliyopewa na Bwana Mungu wako.

22Ulirudi, ukala mkate na kunywa maji mahali alipokuambia usile wala usinywe. Kwa hiyo maiti yako haitazikwa katika kaburi la baba zako.’ ”

23Huyo mtu wa Mungu alipomaliza kula na kunywa, nabii aliyekuwa amemrudisha akamtandikia punda wake.

24Alipokuwa akienda akakutana na simba njiani, akamuua na maiti yake ikabwagwa barabarani, huku punda wake na simba wakiwa wamesimama kando yake.

25Watu waliopita pale, waliona maiti iliyokuwa imebwagwa, simba akiwa amesimama kando yake. Nao wakaenda kutoa habari katika mji ambao nabii mzee alikuwa anaishi.

26Yule nabii aliyekuwa amemrudisha kutoka safari yake aliposikia habari hii akasema, “Ni yule mtu wa Mungu aliyeliasi neno la Bwana . Bwana amemtoa kwa simba, ambaye amemrarua na kumuua, sawasawa na neno la Bwana lilivyokuwa limemwonya.”

27Nabii akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda,” nao wakafanya hivyo.

28Akaondoka na akakuta maiti imetupwa barabarani, punda na simba wakiwa wamesimama kando yake. Simba hakuwa amekula ile maiti wala kumrarua punda.

29Basi yule nabii mzee akachukua maiti ya mtu wa Mungu, akailaza juu ya punda na akairudisha katika mji wake, ili amwombolezee na kumzika.

30Kisha akailaza ile maiti katika kaburi lake huyo nabii mzee, nao wakaomboleza juu yake na kusema, “Ee ndugu yangu!”

31Baada ya kumzika, akawaambia wanawe, “Nitakapokufa, mnizike kwenye kaburi alimozikwa huyu mtu wa Mungu; lazeni mifupa yangu kando ya mifupa yake.

32Kwa maana ujumbe alioutangaza kwa neno la Bwana dhidi ya madhabahu huko Betheli, na dhidi ya nyumba zote za ibada katika mahali pa juu pa kuabudia ndani ya miji ya Samaria, hakika utatimia.”

33Hata baada ya haya, Yeroboamu hakubadili njia zake mbaya, lakini mara nyingine tena akaweka makuhani kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia kutoka watu wa aina zote. Yeyote aliyetaka kuwa kuhani alimweka wakfu kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia.

34Hii ilikuwa ndiyo dhambi ya nyumba ya Yeroboamu ambayo iliisababishia kuanguka na kuangamia kwake hadi kutoweka kwenye uso wa dunia.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.