The chat will start when you send the first message.
1Ahabu akamwambia Yezebeli kila kitu Eliya alichokuwa amefanya na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga.
2Hivyo Yezebeli akamtuma mjumbe kwa Eliya, kusema, “Miungu waniadhibu vikali zaidi, ikiwa kesho wakati kama huu sitakuwa nimeondoa uhai wako kama mmoja wa hao manabii.”
3Eliya aliogopa, na akatoroka kuokoa maisha yake. Alipofika Beer-Sheba katika Yuda, akamwacha mtumishi wake huko,
4lakini yeye mwenyewe akatembea mwendo wa kutwa nzima katika jangwa. Akafika kwenye mti wa mretemu, akakaa chini yake na kuomba ili afe. Akasema, “Yatosha sasa, Bwana , ondoa roho yangu, kwani mimi si bora kuliko baba zangu.”
5Kisha akajinyoosha chini ya mti, akalala usingizi.
Mara malaika akamgusa na kumwambia, “Inuka ule.”
6Akatazama pande zote, na hapo karibu na kichwa chake palikuwa na mkate uliookwa kwenye makaa ya moto, na gudulia la maji. Akala na kunywa, kisha akajinyoosha tena.
7Yule malaika wa Bwana akaja tena mara ya pili, akamgusa na kumwambia, “Inuka ule, kwa kuwa bado una safari ndefu mbele yako.”
8Kwa hiyo akainuka, akala na kunywa. Akiwa ametiwa nguvu na kile chakula, akasafiri siku arobaini usiku na mchana hadi akafika Horebu, mlima wa Mungu.
9Huko akaingia katika pango, akalala humo usiku ule.
Nalo neno la Bwana likamjia, kusema, “Unafanya nini hapa, Eliya?”
10Akajibu, “Nimekuwa nikifanya bidii sana kwa ajili ya Bwana Mungu wa majeshi. Waisraeli wamelikataa agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi peke yangu niliyebaki, sasa wananitafuta ili waniue pia.”
11Bwana akasema, “Toka nje ukasimame juu ya mlima mbele za Bwana , kwa kuwa Bwana yu karibu kupita hapo.”
Kisha upepo mzito na wenye nguvu ukapasua milima ile na kuvunjavunja miamba mbele za Bwana , lakini Bwana hakuwamo katika ule upepo. Baada ya upepo palikuwa na tetemeko la ardhi, lakini Bwana hakuwamo kwenye lile tetemeko.
12Baada ya tetemeko la ardhi moto ukaja, lakini Bwana hakuwamo katika ule moto. Baada ya moto ikaja sauti ya utulivu ya kunongʼona.
13Eliya alipoisikia, akafunika uso kwa vazi lake, akatoka na kusimama kwenye mlango wa pango.
Kisha ile sauti ikamwambia, “Eliya, unafanya nini hapa?”
14Akajibu, “Nimekuwa nikifanya bidii sana kwa ajili ya Bwana Mungu wa majeshi. Waisraeli wamelikataa agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi peke yangu niliyebaki, sasa wananitafuta ili waniue pia.”
15Bwana akamwambia, “Rudi kwa njia uliyoijia, uende kwenye Jangwa la Dameski. Utakapofika huko, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu.[#19:15 yaani Shamu]
16Pia mpake mafuta Yehu, mwana wa Nimshi awe mfalme wa Israeli, na umpake mafuta Elisha mwana wa Shafati kutoka Abel-Mehola awe nabii baada yako.
17Yehu atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Hazaeli, naye Elisha atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Yehu.
18Hata sasa nimeweka akiba ya watu elfu saba katika Israeli, wote ambao hawajampigia Baali magoti, na wote ambao midomo yao haijambusu.”
19Hivyo Eliya akaondoka huko na kumkuta Elisha mwana wa Shafati. Alikuwa akilima kwa jozi kumi na mbili za maksai, na yeye mwenyewe aliiongoza ile jozi ya kumi na mbili. Eliya akamwendea, na kumvisha vazi lake.
20Kisha Elisha akawaacha maksai wake, akamkimbilia Eliya, akamwambia, “Niruhusu nikawabusu baba yangu na mama yangu, halafu nitafuatana nawe.”
Eliya akajibu, “Rudi zako, kwani nimekufanya nini?”
21Basi Elisha akamwacha Eliya, naye akarudi. Akachukua ile jozi yake ya maksai na kuwachinja. Akaipika ile nyama kwa kutumia miti ya nira kama kuni na kuwapa watu, nao wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Eliya, akamtumikia.